Friday, 22 November 2013

ZAIDI YAIBUKA KISA CHA MAUAJI YA MAPENZI DAR ES SALAAM


Christina  Newa 

Dar es Salaam. Imebainika kwamba sababu ya shambulizi la risasi lililotokea Ilala Bungoni, Dar es Salaam Jumanne iliyopita na kusababisha vifo vya watu watatu, ni wivu wa mapenzi uliopindukia.
Akizungumza nyumbani kwao Ilala Bungoni jana, mmoja wa majeruhi ambaye ndiye aliyekuwa kiini cha shambulizi hilo, Christine Newa alisema si kweli kwamba sababu ya mchumba wake, Gabriel Munisi kuwashambulia na kuwajeruhi kwa risasi yeye na mama yake mzazi, Ellen Eliezer na kumuua mdogo wake wa kike, Alpha Newa ni kutokana na kusaliti uchumba wao.
Awali, ilidaiwa kwamba sababu ya shambulizi hilo ni Christine kumkataa Munisi, (ambaye pia alijiua baada ya kufanya mauaji hayo) na kuchumbiwa na rubani wa ndege, marehemu Francis Shumila ambaye pia alifariki katika tukio hilo... “Kwanza Shumila hakuwa mchumba wangu kama ilivyoelezwa. Alikuwa shemeji yangu, mume wa dada yangu Caroline Newa. Pia hakuwa rubani wa ndege, bali nahodha wa meli.”
Alisema amekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Munisi katika kipindi kisichofikia mwaka mmoja lakini sehemu kubwa ya maisha yao ikitawaliwa na misuguano iliyowafikisha polisi mara kadhaa.
Alisema katika kipindi cha uhusiano wao marehemu Munisi alikuwa akimpiga, akimkataza kufanya kazi, kusoma na alikuwa na wivu uliopindukia.
Christine kuona hivyo, aliamua kufanya mipango ya kwenda kusoma katika Visiwa vya Cyprus kimyakimya pasi na kumuaga, jambo ambalo alisema lilimkera mchumba wake huyo na kuweka kisasi.
“Nikiwa huko, Munisi alitafuta mawasiliano hadi akayapata na tukawasiliana na siku niliporejea alikuja kunipokea uwanja wa ndege lakini cha ajabu, alinikataza kwenda nyumbani na badala yake akanipeleka moja kwa moja hadi Mwanza eneo la Kitangiri,” alisema na kuongeza: “Tukiwa njiani kuelekea Mwanza, katika maeneo ya Singida, alisimamisha gari akaniambia nishuke, akatoa bastola na kuniuliza kwa nini niliondoka bila ya kumuaga. Je, nataka kumuacha?”
Alisema alimwomba msamaha na kuendelea na safari yao. Anasimulia kwamba baada ya kufika Mwanza, alimpora simu zake zote na kumfungia ndani kwa zaidi ya wiki
 mbili hadi alipopanda kwenye dirisha na kuomba msaada kwa majirani na kuwapa namba za simu za ndugu zake ili wamsaidie kuwapa taarifa.
Ndugu zake walianza mchakato wa kuwasiliana na polisi hatua iliyofanikisha msichana huyo kurudishwa Dar es Salaam... “Hata hivyo niliondoka na khanga na fulana tu. Vitu vyote niliviacha huko.”
Baada ya kurudi Dar es Salaam, anasema Munisi naye aliamua kumfuata lakini safari hii alifikia katika Hoteli ya MM iliyotenganishwa na ukuta wa nyumba yao na akawa anafuatilia nyendo za familia hiyo.
“Alikuwa ananitumia meseji kwamba amemuona dada Caro, mama na Alpha na wakati mwingine anasema ameniona mimi mpaka nguo tulizovaa, tukaanza kupata na wasiwasi,” alisema.
Wasiwasi huo ulitokana na historia  ya maisha yao ya Mwanza na pia tishio ambalo anadai kwamba Munisi aliwahi kulitoa kwamba atahakikisha anaiteketeza familia yote kuanzia Goba anakoishi mama yake (Ellen), Zanzibar anakoishi mdogo wake (marehemu Alpha) na hapo Ilala.
Anasema walikwenda polisi lakini walielezwa kwamba hayo ni masuala madogo ya mapenzi na kwamba yatamalizwa kifamilia.
Siku ya tukio Christine alikuwa akitoka kwenda uwanja wa ndege tayari kwa safari  ya kurudi shuleni Cyprus ndipo Munisi alipotokea na kuanza kumrushia Shumila risasi na baadaye Alpha kisha mama na yeye kabla ya kujiua.
Akizungumzia tukio hilo, Caroline alisema mumewe alitabiri kifo chake kabla kwani baada ya kusikia vitisho vya Munisi, alimtoa shaka Christine akimwambia kwamba atamlinda hata ikibidi kupoteza maisha yake, jambo ambalo lilidhihiri.
Alisema mama yake amepata nafuu na ameruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa na mazishi ya mdogo wake, Alpha ambaye ameacha mtoto mwenye umri wa miezi minane, yamepangwa kufanyika Jumamosi Goba, Dar es Salaam.
Alisema mipango ya mazishi ya mumewe inafanywa huku akidokeza kwamba huenda akasafirishwa kwenda Mombasa.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...