Tuesday 31 December 2013

Jk: Bunge, wananchi wataamua Katiba




Rais Jakaya Kikwete amesema hatua inayofuata baada ya kukamilika kwa Rasimu ya Katiba ni maamuzi ya wananchi na Bunge la katiba ambayo yataifanya ipitishwe na kuwa Katiba kamili.

Kadhalika, Rais Kikwete alisema katika maamuzi hayo, viongozi wa kijamii na siasa wana nafasi kubwa ya kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unafanikiwa kwa kukwepa maslahi ya vyama vyao na makundi wanayotokea na kinyume chake Katiba ya sasa itaendele kutumika.

Rais aliyasema hayo jana wakati wa kukabidhi ripoti ya Tume na rasimu ya pili ya Katiba, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

“Mchakato wa Katiba unaelekea ukingoni tumefika hatua muhimu sana, ya kuwa nayo au kutokuwa nayo, kote tulipotoka ni mapendekezo, hatua ya uamuzi wa sasa, Bunge la Katiba ndipo uamuzi utatokea iwepo au isiwepo na ikiwepo iwe ya aina gani,” alisema Rais Kikwete.

Alisema: “Viongozi wa kiasiasa na kijamii wanayo nafasi maalumu kuhakikisha tunafanikiwa wakiwamo humo ndiyo wana fursa ya kufanya maamuzi , hivyo watimize wajibu wao ipasavyo ili kuvuka salama katika mchakato huo.”

Alisema ni vyema wakafikiria uhai na ustawi wa Taifa kwa sasa na miaka mingi ijayo. Alisema iwapo vyama vya siasa vitatumia mwanya huo kufanya ushabiki wa kisiasa kwa kila mmoja kutaka maslahi yake au ya chama chake kuwamo kwenye Katiba, ni wazi kuwa hatua ya msingi haitafanikiwa na hivyo kushindwa kulivusha Taifa.

Alisema iwapo kutakuwa na mashindano ni wazi kuwa theluthi mbili ya wajumbe hawatapatikana.

“Iwapo mtakwenda kwa ushabiki wa vyama vyenu mjuwe wazi katiba mpya haitapatikana, tukishindwa tujue kuwa nchi lazima iongozwe kwa Katiba hivyo itatumika iliyopo sasa hadi hapo mtakapoanza mchakato mwingine, mjue kutokufanikiwa ni gharama kubwa kwa nchi,” alisisitiza Rais Kikwete.

Aidha, aliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kujadili kwa kuweka maslahi ya Watanzania kwanza na maslahi ya makundi yao na wao binafsi yawe pembeni ili kuweza kulivusha Taifa.

“Iwapo mtajikita kujadili maslahi ya makundi yenu na yasiyo ya Taifa, kuna hatari ya kupata Katiba isiyokidhi maslahi ya Taifa,” alisema.

Alisema alishavitahadharisha vyama vya siasa alipokutana navyo Ikulu, iwapo vitaenda kwenye Bunge la Katiba kwa kuangali nani kapata nani kakosa au nani kapata zaidi wajue Katiba haitapatikana na wajue mivutano yao itasababisha kukosekana kwa theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge la Katiba.

Alisema aliwaeleza iwapo kama wanajiandaa jinsi ya kushindana haitasaidia hivyo ni vyema watafute namna ya kukaa pamoja na kukubaliana namna ya kulivusha taifa na wakienda kwa kutafuta mshindi wote watashindwa.

Kikwete alisema sheria ya mabadiliko ya katiba inamtaka ndani ya siku 30 kuanzia jana kuitangaza katika Gazeti la Serikali, lakini kutokana na urasimu uliopo, aliagiza iwekwe kwenye mitandao ya kijamii ili wananchi waisome na kutoa maoni yao wakati taratibu za kiserikali zinaendelea.

Alisema pia ndani ya siku 21 anatakiwa kuitisha Bunge la Katiba na kumuagiza Mwenyekiti wa Tume kuiwasilisha kwenye Bunge la Katiba.

Alisema sheria inamtaka kuunda Bunge la Katiba ambalo linaundwa na wabunge wa Bunge la Muungano, Baraza la Wawakilishi na makundi maalumu yanayobeba taasisi, wakulima, wafugaji, walemavu na makundi mengineyo.

Alisema mchakato ulianza Desemba 13, mwaka huu na kwamba mwaliko umetolewa kwa taasisi na makundi hayo kupendekeza orodha ya wajumbe wasiopungua wanne na wasiozidi tisa, na kwamba atashirikiana na Rais wa Zanzibar kuwateua wajumbe hao.

Alisema Januari Alhamisi wiki hii mapendekezo yawe yamewasilishwa, hivyo makundi maalumu yawe yamewasilishwa na kwamba Februari 11, mwaka huu Bunge la Katiba litakuwa limeanza.

Aidha, aliwataka wajumbe wa makundi maalumu na wengi watakaowakilisha wananchi kuisoma rasimu hiyo ukurasa kwa ukurasa pamoja na ripoti ya Tume, na wajue kuwa wananchi ndiyo waamuzi wa mwisho. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...