Tuesday 31 December 2013

Wafanyabiashara Mwanza wafunga maduka kupinga mashine za EFDs


Wafanyabiashara wa maduka Jijini Mwanza wakiingia mtaani wakipinga kupinga matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutolea Risiti (EFDs)

Wafanyabiashara wa maduka ya jumla na rejareja katikati ya Jiji la Mwanza, wamefanya mgomo wakipinga kupinga matumizi ya Mashine za Kielektroniki za kutolea Risiti (EFDs), ambazo hutolewa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Mgomo huo ambao ulianza saa 1:30 asubuhi, ulishika kasi katika barabara za Nyerere na Kenyatta kuelekea eneo la Makoroboi linalozunguka soko kuu, katikati ya jiji hilo, huku ukisababisha usumbufu mkubwa kwa wateja , wananchi wa kawaida pamoja na uongozi wa serikali ya mkoa huo.


Mvutano uliongezeka baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuonekana kwenda kinyume na makubaliano yaliyowekwa baina yao ya kutoendelea na shughuli yoyote ya kibiashara kwa ajili ya mgomo huo.

Akizungumza na wafanyabiashara wenzake katika kituo kikuu cha zamani cha mabasi jijini hapa, maarufu kama stendi ya Tanganyika, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Christopher Mangalanga, alisema waliamua kusitisha huduma zao ili waweze kuendelea na mgomo huo ambao alidai hauna kikomo hadi hapo serikali ya mkoa itakapokubali kukutana nao.

Kwa mujibu wa Mangalanga, mashine za EFD ni mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara hao na kwamba zinawasababishia hasara.

“Msimamo wetu wafanyabiashara wa Mwanza tumeamua kufanya maamuzi magumu ya kusitisha huduma kwa sababu mkuu wa mkoa ameshindwa kutukutanisha na TRA ya mkoani hapa, ili tupate fursa ya kueleza kero tulizonazo kuhusu matumizi ya mashine za EFDs, ” alisema.

Aliongeza kuwa, mashine hizo zinanunuliwa kwa gharama kubwa na kwamba baadhi yake hazina ubora kiasi kwamba huharibika mara kwa mara na kusababisha wao watozwe faini na TRA wakati wanaposhindwa kutoa stakabadhi wanunuzi.

Alisema, baada ya kubaini matatizo hayo, mwezi uliopita walimwandikia barua mkuu wa mkoa huo zaidi ya mara mbili wakimuomba awakutanishe na uongozi wa TRA mkoani hapa, na watendaji wa Halmashauri ya Jiji, lakini hakukuwa na utekelezaji wa aina yoyote.

James Kulwa, mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi kutoka mkoani Geita, alisema, mgomo huo uliwasababisha usumbufu hasa walitoka nje ya jiji, kwani itawalazimu kulala au kurudi wakati mwingine kwa ajili ya kufuata bidhaa.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ndalo Kulwijila, alithibitisha kupokea taarifa za kuwapo kwa mgomo huo na kwamba suala hilo lilikuwa linashughulikiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Meneja wa TRA mkoani hapa, Jeremiah Lusana, alilaani na kushangazwa na wafanyabiashara hao waliogoma kwani wengi waliogoma hawajanunua mashine hizo na kwamba hata muda wa mwisho waliopewa kwa ajili ya kununua na kutumia haujafikia mwisho.

Alisema , suala la matumizi ya mashine za EFDs ni la kisheria, hivyo wafanyabiashara hao wanatakiwa kufuata sheria.

Mgomo wa wafanyabiashara mkoani hapa, umetokea yakiwa yamepita majuma machache tangu wafanyabiashara wenzao katika mikoa ya Lindi, Mbeya na Dar es Salaam walipoamua kugoma wakipinga matumizi ya mashine hizo zinazotolewa na TRA. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...