Jaji Mkuu Mstaafu,Augustino Ramadhani.
Hakuna kiasi cha fedha kinachopaswa kulipwa kwa yeyote anayefanya kazi ya kulitumikia taifa
Kila mjumbe atangulize kwanza maslahi ya nchi
Kila mjumbe atangulize kwanza maslahi ya nchi
Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani , amewataka wajumbe wa Bunge la Katiba kutambua kuwa hakuna kiasi cha fedha kinachopaswa kulipwa kwa yeyote anayefanyakazi ya kulitumikia taifa.
Aliongeza kuwa ni vyema kabla ya kuomba nyongeza ya posho wakalikubali suala hilo kuwa malipo kwa kazi ya utaifa hayana kiwango.
Jaji Mkuu mstaafu, aliyasema hayo jana jijini Arusha, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), unaojadili mchakato wa mabadiliko ya katiba mpya.
Alitolea mfano kwa wanajeshi ambao wanakwenda vitani kupigana vita na baadhi wanapoteza maisha , lakini pamoja na fedha wanayopewa bado haiwezi kulinganishwa na uhai wa maisha yao uliopotea vitani.
Anazungumza hoja hiyo, wakati Bunge Maalumu la Katiba limeunda kamati ya kuangalia uwezekano wa kuongeza zaidi posho ya wajumbe kwa siku kwa maelezo kuwa kiasi cha Sh. 300,000 wanachopewa ni kidogo.
"Lakini Watanzania wengi hawalipwi Sh. 300,000 kwa siku, hivyo kinachotakiwa hapo ni kwa kila mjumbe kutanguliza nchi kwanza,"alisema.
Aliongeza kuwa endapo wajumbe hao wataweka mbele maslahi ya taifa, kazi iliyo mbele yao itakuwa rahisi na pia italeta manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisisitiza tena kuwa mawazo yaliyotolewa kwenye rasimu si ya mtu bali ni maoni ya wananchi hivyo hayawezi kubadilishwa na bunge hilo ambalo lina mipaka.
"Sisi Tume ya Mabadiliko tulifanya kazi kwa kuachana na uchama na kila aina ya kuonyesha maslahi ya mtu au kikundi fulani bali tulizingatia maoni ya wananchi,"alisema.
Kadhalika aliwakumbusha wajumbe wa Bunge la Katiba kusoma kifungu namba 25 cha sheria ya mabadiliko ya katiba ili wayafahamu mambo wanayoruhusiwa na yale ambayo sheria inawazuia kuyazungumzia .
Katika mkutano huo, alisisitiza tena umuhimu wa kuzingatia maoni ya Watanzania na siyo kutanguliza maslahi ya vyama au ya watu binafsi. Alisema jukumu la wajumbe wa bunge hilo ni kuongeza mambo yaliyopungua na siyo kubadilisha misingi iliyopo ambayo imetolewa na wananchi wakati wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba.
"Mimi nawashauri wasome vizuri kifungu cha 25 cha sheria ya mabadiliko ya katiba, waone kama anaruhusiwa au mambo gani wanapaswa kuyafanya,"alisisitiza.
Jaji Ramadhani alishauri ni vizuri kila mjumbe wa bunge hilo akaacha mapenzi kwa vyama vyao na kila kitu na kutanguliza maslahi ya taifa kama wajumbe wa tume ya kuratibu maoni ya katiba walivyofanya na kuwezesha kuandaa rasimu mbili.
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa mabadiliko kwa sasa ni lazima, sababu kila wakati na mambo yake na sasa miaka 50 imepita na hivyo kuna umuhimu wa kupata kitabu kingine cha katiba itakayokwenda na wakati.
Rais wa TLS, Francis Stolla, alisihi wajumbe hao kuongozwa na maoni ya Watanzania na kufahamu vizuri kifungu cha 25 cha sheria hiyo, lakini akidai hajakielewa vizuri kwa sababu hakijafafanua kikamilifu madaraka ya bunge hilo.
Alisema ni vema wakaelewa mwisho wa siku katiba hiyo ikipitishwa na bunge hilo itarudi kwa wananchi ili kuipigia kura, hivyo kama mawazo ya wananchi yameachwa kwa vyovyote wataikataa katiba hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment