Mzazi na mkazi wa Ubungo, Juma Mkopi anatamani angejaaliwa kupata watoto wa kike pekee.
Tofauti na baadhi ya wazazi wanaofikiri mtoto wa kike hana thamani mbele ya mtoto wa kiume, yeye anatamani angekuwa na watoto wa kike ili aidhihirishie jamii kuwa mtoto wa kike anaweza na hata kuwa msaada mkubwa kwa familia yake na jamii kwa jumla.
Mkopi ana kisa kinachovutia kuhusu maisha yake, kama anavyokisimulia japo kwa ufupi: “Sisi kwetu tulizaliwa wawili; dada yangu na mimi. Niliishia kusoma A level (elimu ya sekondari kwa ngazi ya kidato cha tano na sita), lakini dada aliendelea na kufanikiwa kufika chuo kikuu.
“…mama yetu alikuwa muuguzi serikalini, tofauti na baba yetu, mama alikuwa mstari wa mbele kutusimamia kuhusu elimu. Kweli hakuwa na mchezo na elimu hasa kwa dada yangu.
Wakati mimi alikuwa ananiruhusu kwenda kucheza mara moja moja,dada yangu ama alazimishwe kulala au awe mezani anajisomea, niliyaona kama maisha magumu kwake, lakini leo nashuhudia matunda yake. Hata yeye nadhani anaiona faida ya udhibiti wa mama akiwa msichana.
“Dada amenizidi kila kitu katika maisha haya, nitakueleza kwa nini…Unaiona hii nyumba ninayokaa? (ananyoosha kidole kuelekea darini), siyo yangu kaniachia na familia yangu. Unadhani imegharimu kiasi gani? Ana mengi anayofanya kwangu, kwa ndugu na jamaa...’’
Kwa nini Mkopi anatamani angejaaliwa watoto wa kike pekee? Anasema: “Nimejifunza kwa dada yangu namna alivyo msaada kwa familia yetu. Uwezo wake wa fedha na hata imani ya kuwasaidia wengine, vitu ninavyoweza kusema vimetokana na kusoma kwake, kumemwezesha kusomesha watoto wengi katika ukoo wetu.’’
Anaongeza kusema: “Nina watoto watatu, wote wa kiume, sitarajii kuongeza lakini ninatamani Mungu angenipatia japo mtoto mmoja wa kike nimtengeneze kama alivyo dada yangu.’’
Ushuhuda halisi
Kisa hiki ni kielelezo madhubuti cha ukweli usio na chembe ya shaka kuwa mwanamke ni nguzo ya jamii, ni chachu ya maendeleo ya familia na jamii kama alivyo dada yake Mkopi. Chambilecho msemo…ukimsomesha mwanamke, umeelimisha jamii.
Hata hivyo, ni wazazi wangapi nchini wanaotambua ukweli huu? Kwa nini baadhi ya wazazi hawataki kuamini kuwa mtoto wa kike akiwezeshwa anaweza kuwa kiongozi bora wa familia na jamii, au hata kuwa msitiri wa wazazi wenyewe?
Dunia hasa ile ya kwanza inatambua nafasi na hadhi ya mtoto wa kike, iweje sisi wa dunia ya tatu tuendelee kumdunisha mtoto wa kike hadi kufikia hatua ya kumnyima elimu? Bado kuna mila na desturi potofu, achilia mbali mitazamo tenge ya baadhi ya wazazi wasioona umuhimu wa kusomesha watoto wa kike.
.........Itaendelea kesho
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment