Katika baadhi ya jamii nchini, mtoto wa kike anaishi kwenye mazingira magumu, Hata wale wanaobahatika kupata fursa ya kusoma, bado safari yao imesongwa na vikwazo kedekede. Wachache ndio wanaofika mwisho wa safari tena baada ya kuruka viunzi visivyo na idadi. Kwa wanaoishia njiani, wengi wanakosa kabisa matumaini ya kujiendeleza maishani.
Faida ya elimu kwa mtoto wa kike
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (Unesco), Irina Bokova anasema elimu siyo tu ni haki yao ya msingi watoto wa kike, lakini ni nyenzo muhimu ya kustawisha maisha ya jamii zao kwa jumla.
“ Elimu ni haki yao ya msingi... Ni kwa kupitia elimu wasichana na wanawake wanaweza kuwa na uhuru wa kuchagua, kuandaa mustakbali wa maisha yao na kujenga jamii jumuishi na zenye haki,’’ anasema na kuongeza:
“ Kusiwe na visingizio iwe vya kitamaduni, uchumi au kijamii vya kuwazuia wasichana kupata fursa ya elimu. “
Nalo chapisho la shirika la HakiElimu liitwalo ‘Watoto wetu waendelee na masomo baada ya kujifungua’ linaweka bayana faida kadhaa za kumsomesha mtoto wa kike. Kinachovutia ni kuwa faida hizi zinamhusu msichana mwenyewe, familia yake, Serikali na jamii kwa jumla.
Kwa mfano, chapisho linasema wasichana wakisoma, watajengewa uelewa mpana wa haki zao kama binadamu, kwani kujua haki zao ni ushindi mkubwa kwa mwanamke.
“Linaongeza kusema: “Ni ukweli ulio wazi kwamba wanawake wasiojua haki zao ndiyo wanaoendelea kukandamizwa. Elimu itawajaza uelewa huu. Pia itawahimiza kutetea haki za wengine na kubaini sheria na sera zinazowakandamiza na zile zinazowatetea.’’
Ujenzi wa familia bora na yenye tija ni faida nyingine kubwa ya kumwelimisha mtoto wa kike, kama chapisho linavyosema: “…mwanamke aliyesoma ana uwezekano mdogo wa kuzaa watoto wengi ambao hawezi kuwapatia mahitaji yao ya msingi.’’
Linaongeza: “Wakirudi shuleni kutachangia kwa asilimia kubwa kuokoa uhai wa watoto wengi, kupunguza utapiamlo na kupunguza vifo vya kinamama na watoto , maana msichana aliyesoma atakuwa mama wa watoto anayejua kanuni za afya, lishe ya mtoto na uzazi bora, hivyo atalinda afya ya familia yake kwa umakini zaidi.
Chapisho pia linasema wanawake waliosoma ni muhali kunyonywa au kukandamizwa. …’’ Ni vigumu kwa wanawake waliosoma kunyanyaswa na wanaume katika jamii na taasisi zinazoendeleza mfumodume na ukandamizaji wa wanawake.
Faida nyingine ni kuwa wakisoma na kuelimika, watapata fursa zaidi za kujiajiri na kuajiriwa; watakuza moyo wa uzalendo, wataweza kufanya uamuzi sahihi, wenye mantiki na tija; kukuza uwezo wa kufikiri na kujiamini; kuwa na uelewa mpana wa rasilimali za Taifa na namna ya kuzitumia ili kujiletea maendeleo na kutumia na kutengeneza fursa zilizopo kwa maendeleo yao. Inaendelea ukurasa wa 22.
MWISHO
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment