Sunday, 13 April 2014

Mvua yaleta kizaazaa


Jeshi la Polisi Kikosi cha Uokoaji jana kililazimika kutumia nguvu kuwaokoa wakazi wawili wa Jangwani waliokuwa wamezingirwa na maji, lakini wakigoma kuokolewa.PICHA|MAKTABA 
Dar es Salaam. Vifo, uharibifu wa mali, miundombinu na mafuriko, msongamano wa magari, baadhi ya wakazi wa jiji hilo kukimbia makazi yao, wengine kulala kwenye magari na nyumba za wageni vimewakumba wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku ya nne mfululizo.

Timu ya waandishi wa gazeti hili walifanya uchunguzi maeneo mbalimbali na kushuhudia hali halisi ilivyo, huku wanawake na watoto wakionekana kupata shida zaidi kwa kukaa nje ya nyumba zao, wengine kuhamia kwenye majengo ya shule.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam alisema jana kuwa walikuwa wakiendelea kukusanya taarifa za maafa ikiwamo vifo alivyosema ni vingi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik alisema kuwa yupo kwenye kikao na watatoa taarifa zaidi za maafa baadaye.
Tegeta, Boko na Bunju
Mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne, amefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kujaa maji na kushindwa kujiokoa kutokana na ulemavu, wakati mama yake akiwa kwenye shughuli za biashara.
Majirani wa mtoto huyo walisema tofauti na kawaida yao kumtoa mtoto huyo mvua inaponyesha, jana walimsahau na mama yake aliporejea alikuta maiti ya mtoto wake ikielea chumbani.
Katika mvua hizo takribani kaya 180 zimekumbwa na mafuriko huku wakazi wake wakijikuta hawana pa kwenda.
“Mimi nimekuwa hapa tangu Tanu imezaliwa, nyumba yangu imejaa maji nimeshazeeka sina mtu wa kunisaidia, wala sijui wapi nitakwenda. Nomba Serikali inisaidie,”alisema Hussein Ngaoma ambaye ni mjumbe wa nyumba kumi katika eneo hilo.
Naye Husna Ally ambaye pia nyumba yake imekumbwa na mafuriko alisema: “Nasikitika, maana nimepata hasara kubwa. Mimi ni mfanyabiashara katika eneo hili la Boko, nina duka la kuuzia samani limejaa maji na sijaweza kuokoa chochote. Mzigo wa Sh30 milioni umeharibika wote.”
Jeti Lumo
Katika eneo hilo licha ya kujaa maji, mfanyabiashara ndogondogo amefariki dunia kwa kusombwa na maji alipokuwa akijaribu kuokoa jiko lake la kuchomea mishikaki lililotumbukia kwenye mtaro.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...