Saturday 17 May 2014

ASILIMIA 96 YA MIKATE MADUKANI HAINA UBORA


Mkate

Chakula anachokula mtu lazima kiwe na muda wa matumizi. Kutokuwa na tarehe ya ukomo wa kutumika ni kukiuka haki ya mlaji. Kama hiyo haitoshi ni lazima kiandaliwe katika mazingira mazuri na kukidhi viwango vya matumizi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Ikumbukwe kwamba asilimia 60 ya Watanzania hasa waishio mijini wamekuwa wakitumia mkate kama kifungua kinywa, hata hivyo chakula hiki kimekuwa kikitengenezwa na watu wengi bila kufuata sheria, lakini vyombo vya sheria vimekaa kimya.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa licha ya uwepo wa matanuru ya kuoka mikate sehemu tofauti za nchi, wafanyabiashara wengi hasa jijini Dar es Salaam wamekuwa wakizalisha bidhaa hiyo uchochoroni na kwenye makazi ya watu, kisha kusambaza katika maduka bila kuthibitishwa ubora wake na taasisi husika za Serikali.
Maduka yakiwamo yale makubwa (supermarkets), baadhi yake yamekuwa yakitengeneza mikate inayolalamikiwa kuwa mibovu. Baadhi yake hulalamikiwa kuwa haina ubora, mingine huwa na ukungu na mingine kuwa migumu kutokana na kukaa kwa muda mrefu dukani.
Mfanyabiashara mmoja anayezalisha mikate na kuisambaza katika mitaa mbalimbali maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam anasema tatizo ni Serikali akidai imeshindwa kuwaongoza.
 “Nilikuwa na wazo la kuanzisha kiwanda cha kawaida kwa kutumia jiko la mkaa kwa ajili ya kutengeneza mikate na kuuza katika eneo ninaloishi. Jiko langu nilinunua kwa Sh350,000, pia ukijumlisha na vifaa vingine ambavyo nilivinunua sambamba na jiko hili ni Sh450,000, nilifanya hivi kwani sikuwa na kazi ya kufanya. Nikaona nijiajiri,” alisema mfanyabishara huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Kuhusu bidhaa zake kukaguliwa na kupitishwa na Shirika la Viwango (TBS), pamoja na kibali cha Mamlaka ya Chakula na Lishe (TFDA), mfanyabiashara huyo anasema: “Sina kibali kwa kuwa niliona utakuwa mzunguko mrefu. Pili sikuwa na kiwanda maalumu, nisingefanya biashara,” anasema mama huyo anayeuza mikate yake kwa gharama ya Sh800 kwa mkate mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa za TBS ya wiki iliyopita ni kwamba asilimia 96 ya mikate inayouzwa nchini haijathibitishwa ubora wake.
Baadhi ya wananchi wanahofia utendaji wa taasisi za TBS na TFDA kama kweli zinafaa kuendelea kuwepo ikiwa zinashindwa kudhibiti biashara hiyo, kiasi cha kuachia zaidi ya asilimia 96 ya mikate kuuzwa bila kuthibitishwa ubora wake.
Muda wa kuharibika
Hili limekuwa tatizo kubwa, mara nyingi katika maduka haya wauzaji huwabambika mikate iliyoharibika watoto na wasaidizi wa ndani.
Adamu Shayo mkazi wa jijini Dar es Salaam anahoji: “Kwanini mikate haina muhuri unaoonyesha muda uliotengenezwa, pamoja na muda wa kuharibika? Binafsi nimeshanunua sana mikate kwenye maduka makubwa (supermarkets), baadhi yake hadi huwa imeota ukungu, ila kwa sababu ya haraka unajikuta umechukua kitu kibovu,” anasema.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...