Thursday, 22 May 2014

UKATILI WA KUTISHA:MTOTO AISHI NDANI YA BOKSI, AWA MLEMAVU


Rashid Mvungi  akimuangalia mtoto wake Nasrah Rashid (4) ambaye ni mlemavu wa viungo aliyefungiwa chumbani na kufichwa kwenye boksi bila ya kufanyiwa usafi tangu akiwa na umri wa miezi tisa. Picha na Hamida Shariff  wa Mwananchi


Mtoto mwenye umri wa miaka minne amenusuriwa na wasamaria wema baada ya kukutwa amefichwa kwenye boksi  bila huduma zozote za msingi, huku akila viporo kwa kipindi chote cha umri wake na kusababisha kuwa mlemavu.

Mtoto huyo alikuwa akilelewa na mama yake mdogo baada ya mama yake mzazi kufariki dunia akiwa na miezi mitatu.

Mtoto huyo (jina linahifadhiwa), aligunduliwa na majirani akiishi katika hali hiyo mtaa wa Azimio, kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro na tukio hilo la mtoto kuishi katika mateso makubwa kuripotiwa polisi.

Inadaiwa kuwa mtoto huyo alikuwa akilelewa na mama yake mdogo na mume wake ambao waliachiwa jukumu la kumlea baada ya mama yake mzazi kufariki dunia.

Walezi hao wanadaiwa kumfungia mtoto huyo ndani ya boksi na kumpa viporo vya chakula, huku wakimnyima huduma muhimu za msingi kama usafi, chanjo, tiba, malazi na mavazi na kumsababishia  hali mbaya kiafya pamoja na ukurutu wa uchafu katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Baada ya polisi kupewa taarifa walifika maafisa wake wa kitengo cha dawati la jinsia pamoja na maafisa ustawi wa wamii na kumkuta mtoto huyo akiwa katika hali mbaya huku akiwa na ulemavu wa viungo ambao inadhaniwa ameupata kutokana na malezi aliyokuwa akipata na kuishi ndani ya boksi.

Baba mlezi wa mtoto huyo na mama mlezi ambaye ni mdogo wa marehemu wa mtoto huyo, walipohojiwa kuhusiana na hali ya mtoto huyo, pamoja na kukiri kumlea na kuishi naye, walidai alikuwa katika hali mbaya tangu walipompokea na kwamba baba yake mzazi alikuwa hamuhudumii kwa kumpatia fedha za chakula na matibabu.

Hata hivyo, walipoulizwa kuhusu uchafu, ukurutu na kushindwa hata kumvalisha nguo, walishindwa kutoa majibu yanayoeleweka.

Majirani walisema walibaini hali mbaya ya mtoto huyo baada ya kusikia sauti ya kikohozi mara kwa mara kutoka chumba walichokuwa wakiishi walezi hao na kuamua kutuma watoto ambao walipenya ndani na kumkuta mtoto huyo akiwa amehifadhiwa ndani ya boksi, akijisaidia haja kubwa na ndogo humo bila msaada wowote.

Baba mzazi wa mtoto huyo,  ambaye ni afisa ufundi katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alikiri kumpa shemeji yake mtoto huyo ili amlee baada ya mama yake kufariki, na kwamba alilazimika kufanya hivyo ili familia yake isijue kuwa alizaa nje ya ndoa, ingawa alishindwa kueleza iwapo alikuwa akimtembelea na kujua hali yake.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...