TUSEME BASI KWA MAUAJI YA ALBINO!
Ninashindwa kuelewa nianzie wapi kuandika hii makala ya leo.Maana
ninaandika mikono ikitetemeka kwa kweli. Nashindwa kuelewa hasa lawama zangu
nizielekeze kwa nani. Sijui kama ni kwa serikali au wananchi,ama kwa wote.
Hivi ni kweli tumeshindwa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi?
Hawa watu wenye ulemavu wa ngozi wanaishi wapi na wanao waua kikatili nao
wanaishi wapi? Je,wanaishi katika nchi tofauti au sayari tofauti? Kama la, je
ni kweli jamii inayoishi katika maeneo husika haijui ni nani wanaotenda vitendo
hivyo? Kama wanajua kwanini wanakaa kimya?
Je, ni kweli serikali ya Tanzania imeshindwa kabisa kukomesha
ukatili huu? Je,tuchukue sheria mikononi na tuanze kuwateketeza waganga wa
kienyeji wote wanaoishi katika maeneo husika?Nadhani hii ndiyo njia pekee maana
bila ya wao haya yasingetokea. Kama serikali yetu imeshindwa kuwalinda watu
wenye ulemavu wa ngozi wananchi tuchukue jukumu hili. Wananchi wa maeneo husika
kuweni sungusungu katika kaya zenu na hususan kama kuna familia zenye watu wa
ulemavu wa ngozi. Watoto hawa kama vile zinavyojengwa maabara basi zijengwe
shule maalum kwaajili yao na ziwe mbali na maeneo hayo wanayoishi ambako
yametawaliwa na hizo imani potofu.
Lakini tujiulize nini chanzo cha imani hizi kwa wananchi wa maeneo
haya.Mimi Napata jibu hili, UJINGA
na UMASIKINI. Wakazi wa maeneo
husika wangekuwa na elimu wasingeamini ushirikina kwani hata hao wanaonunua
viungo hivyo wangeshindwa pa kuanzia.
Umasikini nao unafanya mtu aweze kufanya chochote ili akabiliane na
maisha. Hivi vitu viwili
huenda pamoja na ni adui mbaya sana katika maendeleo.
Serikali pamoja
na taasisi binafsi zisaidie katika kutoa elimu kwa jamii za maeneo haya. Hii
itachukua muda mrefu ila italeta suluhisho la kudumu. Wakati mchakato wa kutoa
elimu ukiendelea, serikali ikishirikiana na jamii katika maeneo husika iwasake
watuhumiwa wa ukatili huu ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Serikali iweke
donge nono kwa wale watakaosaidia kutoa taarifa za wahalifu hawa.Mimi ni imani
kuwa wanajulikana kwani wanaishi katika jamii hiyo hiyo. Wanaofanya hayo ni wanajamii wenyewe yaani baba wa familia, watoto wa familia, jamaa wa familia, jirani wa familia n.k
Na pale watakapothibitika,adhabu
kali ichukuliwe juu yao.
TUSEME BASI KWA MAUAJI YA ALBINO!
Imeandikwa na
Anna Nindi
No comments:
Post a Comment