Ni majira ya saa 2 usiku,tupo nje
ya hoteli tuliyofikia kisiwani Mafia,tunaona watu wengi wakipita na mizigo kichwani
na mikononi kuelekea upande mwingine. Tunauliza wenyeji wetu ni wapi walikuwa
wakielekea watu wale. Walitujibu kuwa walikuwa wakielekea bandarini kupanda “chombo”
kuelekea Dar es salaam. Nilidadisi zaidi kutaka kujua hicho “chombo” kilikuwa
ni nini? Nijibiwa kuwa kilikuwa ni “jahazi”. Niligundua kuwa usafiri wa Mafia
kwenda Dar haukuwa ni wa kila siku.
Nilipatwa na udadisi zaidi wa
kutaka kwenda kuona mandhari ya “bandari na chombo” chenyewe mara nitakapopata
nafasi.Baada ya siku kadhaa kulikuwa na usafiri tena. Majira ya saa 2 usiku
tukifuatana na mwenyeji wetu,tukaenda kuona mandhari ya bandari na chombo.
Nilipigwa na butwaa tulivyofika
pale kwani kuna mambo ambayo kwangu hayakukaa sawa.Kwanza, palikuwa giza na
sikuweza kuona chochote. Pili,nilidhani ni bandari kama bandari nyingine
tulizozoea,yaani kuona vyombo ya usafiri vikiwa vimeegesha.Pale hatukuona
kitu.
Kilichotushangaza zaidi ni kuona
watu, wakiwa na mizigo yao, wakielekea baharini. Tulisogea karibu ili kuelewa
nini kilikuwa kinaendelea. Watu walikuwa wakiingia katika boti ndogo wakiwa na
mizigo yao. Boti hiyo ndiyo ilitumika kuwapeleka watu kwenye jahazi ambalo
lilikuwa kwenye maji mengi na halikuonekana katika upeo wa macho yetu. Jahazi
hilo ndilo lingewapeleka Dar es salaam kupitia Kisiju, Pwani, ambapo ndipo wangeshukia.
Haya ndiyo majahazi ya kwenda Mafia,Kisiju, Mkuranga, Pwani.
(PICHA kwa hisani ya tulonge.com)
Nilibaki mdomo wazi na woga ukiwa
umenijaa.Kwani niliona kabisa kuwa safari ya watu wale ilikuwa ni safari isiyo
na uhakika. Niliwafikiria zaidi kina mama na watoto ambao walikuwemo katika
safari ile. Hivi ni kweli, watanzania hawa wanashindwa kupatiwa usafiri wa
uhakika?
Usafiri wa ndege ulikuwepo kwa
ndege ndogo za Coastal Aviation.Ndege inayochukua abiria 12 tu au chini ya hapo.
Na hata hivyo ndege ni gharama kwa wakazi wa Mafia ambao wengi ni wavuvi na
wakulima ambao kipato chao ni kidogo. Sijui kwa wale wa Mafia kama hali hii
imebadilika.
KWELI TEMBEA UONE.
Imeandikwa na Anna Nindi
No comments:
Post a Comment