Thursday, 8 December 2016

HATMA YA MTU HUPANGWA NA MUNGU NA SI MWANADAMU

DEAR FRIENDS.

Wiki chache zilizopita nilikwenda Bank, nikiwa karibu kuifikia foleni iliyokuwa mbele yangu ghafla alitokea mwanamke mmoja nyuma yangu kwa kasi ya ajabu akanisukuma pembeni ili ajiunge na foleni ndefu iliyokuwepo Bank kabla yangu. Nikiwa bado namshangaa alifanya haraka akajiunga na ile foleni ndefu. Sikumsemesha chochote, alidhani nitaenda kusimama nyuma yake lakini mimi sikuwa nahitaji kuweka wala kutoa fedha bali nilikuwa naelekea "Bulk" wanapoenda watu wanaotoa au kuweka fedha nyingi. Huko hakukuwa na foleni kwahiyo niliingia na kupatiwa huduma kisha nikatoka. Nilipokuwa naondoka yule mwanamke alinifuata kuniomba radhi kwa kunisukuma "Ooh pole na samahani sana kwa kukusukuma, nilidhani na wewe unakuja kwenye foleni nikataka kukuwahi. Kwakweli nisamehe bure." Nikamtoa wasiwasi kisha nikaondoka na kumuacha kwenye foleni.

Tangu wakati huo, kuna somo kubwa sana nimejifunza. Ni Mara nyingi sana hali kama hii inatokea katika maisha yetu ya kila siku. Inawezekana watu ulionao au unaoishi nao kila siku iwe kazini, nyumbani, kwenye biashara n.k wamekuwa na kawaida ya kukusukumia mbali wakijaribu kukuwahi ili wawe mbele yako kwa hila ilimradi tu wakuchelewesha na kukuzuilia usifikie mafanikio na malengo yako. Wengine wamejaribu kuwasukuma mbali wenzao hata katika nyumba za ibada na makazini kwa kuwazushia maneno mabaya yakuwachafua ili wasipewe nafasi au cheo fulani au wafukuzwe kazi. Unachotakiwa kuelewa ni kwamba japo tuko Njia moja ila Hatima na malengo ya safari zetu ni tofauti, na kiongozi wa Safari anayejua hatma ya kila mmoja ni Mungu. Inawezekana wote tunaenda bank Ila hatufanani malengo yanayotupeleka huko, pengine wewe unaenda kuweka fedha wakati mwingine naenda kutoa fedha, Malengo tofauti! Sasa usimsukume mwenzako wakati hujui foleni yake.

Unadhani wangapi umewasukumia mbali ukidhani wanakuja kuvuruga Maslahi yako wakati hawana hata mpango na maisha yako? Wangapi umewasukuma mbali kwa kuwakashifu na kuwazushia uongo ili kuzuia maendeleo yao, kuzuia kustawi wao, kuwaharibia sifa njema na kuchafua majina yao ili tu kulinda maslahi yako? Bado hujamjua huyo unayemsukuma anaelekea wapi! Wakati unamsukuma ukidhani umemkomesha mwenzako anakazana kufanya shughuli zake anamaliza anaondoka anakuacha kwenye Foleni bado unasubiri. Sote tuko kwenye foleni tunasubiri Mungu atubariki kwa njia tofauti, njia Mungu atakayoitumia kukubariki wewe sio njia atakayoitumia kumbariki yule, sasa ukianza kumsukuma mwenzio kwa kumtangaza vibaya, kumzushia uongo na kumgombanisha na watu ili uwe wa kwanza kupata kitu fulani utachemsha! Mungu hana upendeleo wala hapendi Hila na Wivu wa kijinga. Acha kusukuma wenzako kanisani, msikitini, makazini, kwenye biashara, n.k maana hujui Mungu amepanga nini juu ya wale unaowasukuma mbali, atawabariki wao halafu wewe utabaki kwenye foleni unasubiri.

Mungu atatumia kule kukusukuma kwao kuwathibitishia kuwa Hatma ya mtu iko mikononi mwake na sio mikononi mwa wanadamu. Hapo ndipo watakaposhangaa ukiwaacha kwenye foleni wanasubiri. Na vile fimbo ya Mungu ilivyo mbaya atawaaibisha wakiwa bado kwenye foleni.

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...