Mitando ya kijamii ilitawaliwa na ripoti iliyodaiwa kutolewa na daktari wa hospitali ya St Hellen ya mjini Johannesburg alikofikishwa Ngwair na mwenzake ikidai kuelezea chanzo cha kifo cha msanii huyo aliyepata umaarufu mkubwa nchini kupitia tungo zake kali zikiwamo za 'Ghetto Langu' na 'Mikasi'.
Ndugu wa M 2 the P pia alidaiwa kupigia simu ndugu zake kutokea nchini Afrika Kusini kuwaeleza kwamba nduguye huyo pia amefariki.
Hata hivyo, daktari aliyemhudumia Ngwair alisema kutokea hospitalini hapo jana kupitia kituo cha radio cha Clouds FM kwamba M 2 the P alikuwa hai na kwamba hadi jana jioni hali yake ilizidi kutengemaa ambapo aliweza kufumbua macho na kujaribu kuinuka japo alikuwa akipumulia mashine.
"Hatujampima damu kujua chanzo cha tatizo lake, lakini (M 2 the P) yuko hai na anaendelea vizuri," alisema daktari huyo huku akisisitiza kuwa Ngwair pia alikuwa bado hajapimwa kujua chanzo cha kifo chake.
Mwili wa Ngwair ulihamishwa jioni ya jana kutoka katika hispitali ya St. Hellen na kupelekwa katika mochwari ya serikali iliyopo mjini hapo na alionekana kwamba alitokwa na damu nyingi puani.
Kenneth Mangweha, kaka wa marehemu, alitoa taarifa ya familia akiomba msiba huo usigeuzwe wa kisiasa kwa sababu ni sherehe ya mwisho ya marehemu duniani na kuwataka kila mmoja ashiriki katika kuulaza mwili wa Mangwair kwenye nyumba yake ya milele.
Alisema tayari wameshawasiliana na ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kwa ajili ya mipango ya kuurejesha mwili huo nchini lakini maamuzi ya mwisho ya kipi kifanyike yalikuwa hayajafikiwa.
Kaka huyo alisema ilikuwa bado haijaamuliwa mwili wa Ngwair upelekwe wapi ukishawasili nchini kwa sababu ndugu wa marehemu walikuwa wanaendelea kuwasili nyumbani kwa mama wa marehemu.
Hata hivyo, alisema ndugu wengi walikuwa wakipendekeza mwili wa Ngwair upelekwe Morogoro kwa mama yake Denisia Mangweha kwavile baba yake tayari alishafariki dunia.
WASANII WAMLILIA
Wasanii mbalimbali wa kizazi kipya walielezea masikitiko yao kufuatia kifo hicho huku MwanaFA na Kalapina ambao walikuwa wakijiandaa kufanya maonyesho tofauti Jumamosi hii, walitangaza kuahirisha maonyesho yao.
"Taarifa hizi zimenistua sana, nimeamua kuahirisha onyesho langu ya 'The Finest' lililokuwa lifanyike Jumamosi. Haiji kufanya onyesho wakati kuna msiba mkubwa namna hii," alisema rapa huyo kwa masikitiko.
Haji Noorah, ambaye alisoma na Ngwair katika sekondari ya Mazengo, Dodoma na ambaye waliunda wote kundi la Chamber Squad, alisema alizungumza na nyota huyo aliyefahamika pia kwa jina la "Cow Boy" ama "Cow Obama" siku chache zilizopita akiwa nchini Afrika Kusini.
"Si unajua mimi naoa wiki hii, nilimpigia simu kumuuliza kuhusu mchango wa harusi, akaniambia nisiwe na wasiwasi kwa sababu alikuwa anajiandaa kurejea na atarekebisha... ni pigo kubwa sana. Hadi sasa bado siamini, nadhani hadi niuone mwili wake," alisema nyota huyo wa nyimbo za 'Vijimambo' na 'Ice Cream'.
Noorah aliongeza: "Hapa Tanzania hamna msanii mwenye kipaji kama Ngwair."
Rapa Dark Master, memba mwingine wa Chamber Squad, aliiambia NIPASHE kwamba ilikuwa naye aambatane na Ngwair Afrika Kusini lakini kuna mambo yaliyomfanya ashindwe kwenda.
"Hapana, siamini kama Cow Boy amefariki. Siwezi kuamini mpaka nitakapouona mwili wake, nimechanganyikiwa kwa kweli," alisema Dark Master aliyeshirikishwa kwenye wimbo mwingine wa Ngwair uliotamba sana wa 'She Got A Gwan'.
Kundini Chamber Squad, Ngwair alikuwa pamoja na Noorah, Mez B, Dark Master na Tony, ambao waliasisi kundi hilo baada ya kukutana na kutambuana vipaji wakati wakisoma katika shule ya sekondari ya Mazengo ya mjini Dododma.
Ngwair alifahamika zaidi shuleni Mazengo kama mkali wa mchezo wa kikapu kuliko msanii, tofauti na ilivyokua baada ya kumaliza shule.
Rapa huyo anayeaminika kama msanii mkali zaidi wa 'freestyle' kupata kutokea nchini, alitamba na nyimbo nyingi zikiwamo 'Ghetto Langu', 'Mikasi', 'She Got A Gwan', 'Nipeni Dili', 'Napokea Simu', 'Kimya Kimya', 'Spidi 120', 'Ndani ya Club', 'CNN', 'Singida-Dodoma' na 'Sikiliza' aliowashirikisha MwanaFA na Lady Jaydee.
Albam yake ya 'Bado Nimo a.k.a Mimi' iliyohusisha nyimbo za 'Ghetto Langu', 'Napokea Simu', 'Mikasi', 'Sikiliza' na 'She Got A Gwan', ilimpatia tuzo ya Kilimanjaro ya Albam Bora ya Hiphop 2005.
Ngwair alijiweka kando ya muziki kutokana na fadhaa aliyoipata baada ya albam yake hiyo iliyokuwa na mafanikio makubwa kutomuingizia chochote.
Alipokuwa akijiandaa kurejea katika gemu mwaka 2007, Ngwair aliiambia NIPASHE: "Wakati nikijiweka kando ya gemu, sikusema kwamba naacha muziki... ila nilisema nakaa pembeni kwa ajili ya kutafuta mbinu za kujikomboa, siyo kuendelea kufanya kazi zinazonufaisha wengine huku mimi nikiendelea kuchoka.
"Iliniumiza kichwa sana kuona mimi mwenye albam bora ya mwaka 2005 nasainishwa na Wadosi nakala 500 tu na kupewa Sh.250,000 ... je hao wengine watapata shilingi ngapi?
"Hii ilinikatisha tamaa na kuona ipo haja ya kujipanga upya.
"Nafahamu kwamba Wadosi wanauza nakala nyingi na wanatudhulumu, lakini isiwe dhuluma ya kiasi kile, ile imezidi... wao wanauwauzia wenye maduka makubwa pamoja na wasambazaji wengine wenye vibanda ambao hununua kwa jumla na kulipa fedha taslimu, lakini wanavyolalamika kuwa biashara haiendi utadhani ni wao wanaotembeza mitaani kuuza nakala mojamoja."
Mungu alilaze pema roho ya Albert Mwangweha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment