Picha zinaonyesha mwonekano wa jiji la Stockhol,Sweden |
By
Othman Miraji, mwananchi
Sweden
ni nchi iliyoko kaskazini ya Ulaya ambayo inasifika kwa neema na uchumi wake
kung’ara, licha ya kodi kubwa ya mapato wanayotozwa raia.
Ina mfumo wa kijamii unaojali maslahi ya
walalahoi pamoja na siasa ya kigeni isiojiingiza na kuonyesha misuli katika
migogoro ya kimataifa. Wiki iliopita nchi hiyo ilipata mshtuko wa kujionea
michafuko.
Wakazi
wenye asili ya kigeni walifanya fujo, wakayatia moto magari barabarani na
kupambana na polisi. Ile sifa ya Sweden kama mfano wa nchi ya kupigiwa mfano
duniani, ambako watu wote wanapatiwa nafasi sawa, kwa ghafla ikawekewa alama ya
kuuliza.
Wenyewe
Waswidi wakaanza kuulizana; kulikoni ? Polepole wanaanza kugundua kwamba siasa
inayofuatwa na Serikali yao ya kuwachanganya wahamiaji wapya ndani ya jamii
inashindwa kutoa tija.
Pale
wanasiasa wa Sweden wanaposafiri kwenda katika mikutano ya kimataifa ili
kumwaga sifa juu ya nchi yao, njiani wanapoelekea katika kiwanja cha ndege cha
mji mkuu wa Stockholm wanaupita mtaa wa Husby ulio na matatizo mengi ya
kijamii.
Bila
shaka, wanapopita hapo nafsi zao husononeka. Katika miaka ya sitini kulijengwa
nyumba nyingi za bei nafuu katika eneo la Husby ili kukabiliana na uhaba wa
makazi. Lakini kila miaka ilipopita
wazawa walilihama eneo hilo na mahala pao pakachuliwa na watu wenye
asili ya kigeni, wengi wakitokea nchi zilizomo vitani, kama vile Syria, Iraq,
Afghanistan, Somalia na iliyokuwa Yugoslavia.
Kwa
siku kadhaa wiki iliopita machafuko na ghasia zilizoanzia Husby zilienea katika
sehemu nyingi pembezoni mwa jiji la Stockholm. Ni kutokana na hali hiyo watu
sasa wanaanza kutambua kwamba siasa inayoendeshwa na Serikali ya Sweden ya
kuwachanganya watu wenye asili ya kigeni katika jamii ina mushkeli, haifanyi
kazi vizuri. Wageni katika nchi hiyo wanaishi katika ulimwengu tofauti kabisa,
wanaishi katika maeneo ya madongoporomoka, wakiwa hawana ajira wala matumaini.
Hii
sio mara ya kwanza kutokea ghasia za aina hii huko Sweden, lakini mara hii
chanzo kilikuwa ni kuuliwa kwa mkazi mmoja wa Husby, anayesemekana alikuwa na silaha ya panga.
Imetajwa kwamba askari polisi waliomuua
walidai alihatarisha usalama wao.
Polisi
pia inalaumiwa kutumia mabavu makubwa wakati wa kuyavunja maandamano ya vijana
yaliofuata tukio hilo. Katika siku hizo za fujo vijana wa kigeni waliofunika nyuso zao waliyatia moto
magari na mapipa ya kuwekea taka, huku wakiwatupia mawe polisi.
Shule na kituo cha polisi vilitiwa moto. Waandamanaji
kadhaa walikamatwa. Pia ilidaiwa polisi nao walitumia maneno machafu ya
kibaguzi kuwatusi wahamiaji wa kigeni, na kuwatisha watu waliojitokeza katika
maeneo ya fujo kutaka kujua zaidi juu ya mkasa huo. Madai dhidi ya madai, na
yote hayo sasa yanachunguzwa.
Baadaye hali ilitulia kutokana na vikundi vya wazee
kuwapa nasaha vijana wapunguze mori na jazba, na pia polisi kubadilisha mbinu
zao. Badala ya kualika mapambano, polisi wakawa tayari kutafuta watu wa
kuzungumza nao miongoni mwa waandamanaji.
Ukosefu wa nafasi za kazi katika eneo la Husby ni mkubwa,
na ni asilimia 50 tu ya watoto katika mtaa huo humaliza shule za sekondari. Hata wale wanaomaliza wanakuwa na matokeo mabaya, hivyo wanashindwa kuendelea na masomo
ya juu.
Madai siku hizi yamezushwa kwamba hakuna usawa katika
Sweden, kinyume na vile baadhi ya watu wanavojaribu kuichora sura ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi ni kwamba
mwaka 2011, asilimia 16.5 ya wahamiaji
walikuwa hawana ajira ukilinganisha na asilimia 5.7 ya wazawa wa Kisweden.
Wahamiaji hujaribu kuomba nafasi za kazi na hukataliwa kutokana na majina yao,
sura zao au kwa sababu wanaishi katika mitaa fulani.
Hasira za kukosa matumaini ni mambo ambayo mara nyingi
yanasababisha machafuko. Mwaka 2008
zilizuka ghasia kama hizi mjini Malmo, miaka miwili baadae Rinkeby, mtaa ulio
umbali na vituo vichache vya basi kutoka hapo.
Waziri Mkuu wa Sweden, Fredrik Reinfeldt, amekiri kwamba
kuna pengo la mapato linalozidi baina ya raia,
na kwamba kipindi hiki cha mpito ni kigumu kwa nchi yake, lakini katika
kipindi kirefu kijacho Serikali yake itashinda katika kuyatanzua matatizo ya
kijamii yaliyoibuka sasa.
Hata
hivyo, anasema kuichoma moto gari ya
jirani yako sio njia ya kuelezea maoni yako na kufikisha ujumbe, bali ni uhuni
tu. Anajinata kwa kusema kwamba Sweden ni nchi inayopokea makundi makubwa ya
watu kutoka mataifa mengine, na yeye ana fahari juu ya jambo hilo.
Haikataliki
kwamba hisia za Wasweden wenyewe kuelekea wahamiaji pia zimebadilika, kutokana
na mmiminiko mkubwa wa wageni katika nchi hiyo mnamo miaka ya karibuni.
Asilimia 15 ya Waswidi milioni 9.5 ni watu waliozaliwa nje ya nchi hiyo,
ukilinganisha na asilimia 10 miaka kumi iliopita.
Kwa
mfano, theluthi mbili ya wakazi wa Husby wana
asili ya kigeni. Kinyume na Denmark ambayo ilifungua milango yake kwa
wahamiaji walio maskini. Sweden bado
inapokea wakimbizi wengi, hasa kutoka nchi zilizokumbwa na vita.
Serikali
ya nchi hiyo humpa mtu anayeomba hifadhi ya ukimbizi nyumba, samani mpya na
karibu Euro 2,000 kila mwezi. Licha ya
hayo, nchi hiyo bado inapata shida ya kuwachanganya katika jamii watu hao ambao hawaambatani na mila na desturi za watu
wa Skandinavia.
Machafuko
na ghasia za karibuni nchini Sweden ni mtihani kwa Serikali ya Waziri Mkuu
Reinfeldt, ambayo baada ya kuweko madarakani kwa miaka saba, hivi sasa inalaumiwa sana kwa
kushindwa kuyatanzua matatizo ya kijamii.
Pia
ghasia hizi zimekipa hoja chama cha
Democratic kwamba kuzidi sana idadi ya wahamiaji nchini humo, ndio mzizi wa fitina na matatizo. Lakini
isisahaulike kwamba matatizo mengi
yalioyoonekana baada ya kumiminika wahamiaji kutoka nchi zinazoendelea hivi
sasa, yanaweza kuonekana kutokana na
kuwepo pia wahamiaji kutoka nchi za
Umoja wa Ulaya.
No comments:
Post a Comment