Ndege,meli za kivita zaanza kuwasili Dar
Kutokana na hali hiyo, wakazi wa pembezoni mwa Jiji hilo na wanaotoka mikoani wasio na shughuli muhimu wameshauriwa kutokwenda katikati ya Jiji katika kipindi chote cha ziara ya rais huyo.
Ushauri huo ulitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alipokuwa akizungumzia ziara ya Rais Obama kupitia kipindi cha kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam.
“Tunatarajia Jiji la Dar es Salaam kusimama katika kipindi hiki kwa kuwa baadhi ya barabara zitafungwa kwa ajili ya kurahisisha misafara ya ugeni wetu,” alisema Waziri Membe na kuongeza:
“Kwa hiyo niwaombe wananchi wanaoishi pembezoni mwa Jiji na wale wanaotoka mikoani ambao hawatakuwa na shughuli katikati ya Jiji kubakia nyumbani katika kipindi hiki hadi ugeni utakapoondoka.”
NDEGE YA KIJESHI YA MAREKANI YATUA DAR
Wakati huo huo, ndege kubwa ya kivita kutoka Marekani ilitua jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) ikiwa na idadi kubwa ya wanajeshi wa nchi hiyo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wakati wa ziara ya kiongozi huyo wa taifa kubwa duniani.
Akizungumza na NIPASHE, mmoja wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwa kuwa siyo msemaji wa mamlaka hayo, alisema kuwa ndege hiyo ikiwa imebeba helikopta mbili, ilitua uwanjani hapo jana asubuhi ikiwa na askari ambao idadi yao haikujulikana.
Kwa mujibu wa mfanyakazi huyo, ndege hiyo ni kubwa kiasi kwamba tangu aanze kufanya kazi katika mamlaka hiyo hajawahi kuona ya namna hiyo ikitua uwanjani hapo.
Aliongeza kuwa wanajeshi wa Marekani walikuwa wakifanya gwaride kwa ajili ya kujiandaa kuimarisha usalama.
Mashuhuda wengine wakiwamo wafanyakazi wa TAA, walisema kuwa takribani kipindi cha mwezi mmoja uliopita, mambo mengi yamebadilika uwanjani hapo ikiwamo ulinzi mkali kwa ajili ya ziara ya Rais Obama huku ndege za taifa hilo kubwa kiuchumi na kijeshi duniani zikiwa zinatua na kuondoka kwa ajili ya kuhakikisha usalama.
Waliongeza kuwa wanajeshi wa Marekani tayari wamekwisha kuweka minara mbalimbali ya mawasiliano ya kiusalama uwanjani hapo.
NIPASHE lilishuhudia minara hiyo na iliyokuwa ikiendelea kujengwa jana.
Kutokana na unyeti wa ziara hiyo, iliwawia vigumu kwa waandishi wa habari waliofika uwanjani hapo kuingia uwanjani hapo kutazama ndege hiyo baada ya viongozi wa TAA kuwaeleza kuwa haiwezekani kufanya hivyo.
Maofisa wa TAA hawakuwa tayari kutoa taarifa kwa vyombo vya habari wakisema wahusika walikuwa kwenye kikao.
MAENEO YA HOTELI
Pia NIPASHE lilizungukia maeneo mbalimbali ya hoteli kubwa jijini Dar es Salaam ikiwamo Kilimanjaro Hyatt Regency na kushuhudia maboresho katika maeneo mbali ya hoteli hiyo vikiwamo bustani za maua, mabango ya matangazo kwenye lango kuu na hali ya usafi kwenye mabwawa yaliyopo mbele ya hoteli hiyo.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa waandamizi wa hoteli hiyo alikataa kuzungumzia chochote kuhusu ugeni huo kwa madai kwamba hajaruhusiwa kuzungumza.
IKULU, OFISI YA WAZIRI MKUU
Jana NIPASHE lilishuhudia baadhi ya ukuta wa uzio wa Ofisi ya Waziri Mkuu ukiwa umepakwa rangi mpya.
Pia lilishuhudia mafundi walikuwa wakiendelea kutengeneza kuta hizo ikiwa ni pamoja na zile zilizo karibu na lango la upande wa Mashariki wa Ikulu.
NYUMBA ZA TANESCO ZAKARABATIWA
Nyumba za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) zilizo mkabala na Ubalozi wa Marekani nazo zimepakwa rangi.
NIPASHE lilishuhudia nyumba hizo zikiwa zinang’aa kwa kupakwa rangi nyeupe huku ukuta unaozunguka nyumba hizo nao ukiwa umepakwa rangi ya kijivu.
UBALOZINI
Nao na wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani walikuwa wakifanya usafi kwenye bustani iliyopo nje ya ubalozi.
Aidha, mafundi ujenzi walionekana wakiifanyia ukarabati barabara ya Mwai Kibaki na ile inayopita kwenye ubalozi kwa kuziba mashimo na kuweka vitofali vidogo vidogo kwenye eneo la waenda kwa miguu.
DARAJA LA SALENDER
Vile vile, NIPASHE lilishuhudia daraja la Salender likiwa limepakwa rangi na kupendeza.
Kadhalika, katikati ya jiji hali ni tofauti sana, kwani linaonekana kuwa safi hakuna uegeshaji hovyo wa magari na pikipiki.
Wamachinga, mafundi viatu, wapaka rangi na mama lishe wameondolewa mitaani katikati ya Jiji huku mgambo wa Jiji wakizunguka maeneo mbalimbali kuwadhibiti.
MAANDAMANO YA CUF MARUFUKU
Wakati huo huo; Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF) kuanzia katika Ofisi za chama hicho hadi Ikulu, keshokutwa.
Amri hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na ziara ya Rais Obama na mkutano wa kimataifa wa ushirikiano kwa manufaa ya wote (Smart Partnership Dialogue -SPD).
Kwa mujibu wa Kova, CUF iliomba kibali kwa Jeshi la Polisi kuruhusiwa kufanya maandamano hayo kwa lengo la kupinga masuala ya gesi.
“Baada ya kupokea maombi hayo, tumetafakari na kufuatilia kwa makini juu ya ombi hilo. Tumeona haiwezekani kutokana na sababu kama hizi,” alisema Kova.
Alisema Tanzania itakuwa na wenyeji wa mkutano huo, ambao utahusisha ugeni wa marais 14 na wajumbe wengine mbalimbali, hivyo, maandamano hayo yataingiliana na ugeni huo.
Kamanda Kova alisema licha ya ugeni huo, kutakuwa pia na ziara ya Rais Obama anayetarajia kuwapo nchini Julai Mosi, hivyo maandamano hayo yataingiliana na maandalizi ya ziara hiyo.
Pia alisema barabara, ambayo wanatarajia kutumia kwa ajili ya maandamano, ni Buguruni Petro Station kupitia Barabara ya Uhuru, ambayo itatumika katika msafara wa marais.
Alisema Jeshi la Polisi linazuia maandamano hayo kwa nia nzuri na endapo watakiuka agizo hilo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao, na kama hawataridhika wakate rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa mujibu wa Kova, Jeshi la Polisi limepata taarifa za kuaminika kuwa kuna chama cha siasa na taasisi, ambazo zimejiandaa kusambaza vipeperushi au kujitokeza na mabango ghafla barabarani wakati wa ujio wa Rais Obama.
Alisema kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za usalama.
Alisema uchunguzi wa hali ya juu unafanyika kuwabaini wahusika na kwamba, endapo mtu yeyote atajaribu kutenda kitendo hicho, atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
ULINZI WAIMARISHWA SENEGAL
Hali ya ulinzi katika Jiji la Dakar nchini Senegal imeimarishwa baada ya mashushushu wa FBI na CIA kutoka Marekani kufanya doria muda wote kwa kulizunguka jiji hilo siku nzima jana huku mawasiliano ya simu za mikononi yakiwa hayapatikani.
Rais Obama aliwawasili katika mji mkuu wa nchi hiyo, Dakar jana usiku kuanza ziara ya kuzitembelea nchi tatu za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Gazeti la The Guardian la Uingereza lilielezea hali halisi iliyopo nchini Senegal muda mfupi kabla ya kuwasili kwa rais huyo.
Afua Hirsch, mwandishi wa gazeti hilo, alisema maafisa wa FBI na CIA walilizunguka Jiji la Dakar kuhakikisha hali ya usalama kwa kiongozi huyo inakuwapo.
Alisema hadi kufikia jana mchana, wakazi wa jiji hilo pamoja na ofisi zilizopo karibu na ubalozi wa Marekani jijini Dakar zilikuwa hazipati mawasiliano yoyote ya kimtandao hususani simu za mezani na mikononi.
Naibu mkuu wa ushauri wa ulinzi, mawasiliano na uandishi wa taarifa wa Ikulu ya Marekani, Ben Rhodes, alisema Rais Obama alitarajia kuwasili Senegal majira ya usiku kwa saa za nchi hiyo.
Alisema akiwa Senegal, Obama atatembelea kisiwa cha Goree kilichokuwa kinatumika kupokea watumwa na kwamba mke wa Obama, Michelle, atafanya mazungumzo na mke wa Rais wa Senegal, Marieme Faye Sall.
Alisema baada ya mazungumzo hayo, Michelle na Marieme watakwenda katika shule ya wasichana ya Martin Luther King.
Baada ya hapo Rais Obama atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Macky Sall, na atakaa nchini humo kwa siku mbili hadi hadi leo.
OBAMA KUKUTANA NA MAJAJI
Aidha, Rhodes alisema Rais Obama akiwa Senegal atakutana na majaji wakuu 11 kutoka barani Afrika na kufanya nao mazungumzo yanayohusu wajibu wa mahakama katika demokrasia.
Taarifa kutoka Kenya zinaeleza kuwa Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Dk. Willy Mutunga, atakuwa ni miongoni mwa majaji wakuu watakaokutana na Rais Obama.
Gazeti la The Star la Uingereza lilieleza kuwa ubalozi wa Marekani nchini Kenya umejitolea kugharimia safari nzima ya Jaji Mutunga.
Gazeti hilo lilimnukuu balozi ya Marekani nchini Kenya, Robert Godec, akisema: “Ubalozi wa Marekani utagharimia safari yote ya Jaji Mtunga akiwa Senegal hadi atakaporudi nyumbani.”
Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Isaya Kisimbilu, Gwamaka Alipipi, Samson Fridolin, Enles Mbegalo na Neema Haule.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment