Wednesday, 24 July 2013

BOMU LANASWA ZIARA YA PAPA FRANCIS NCHINI BRAZIL


Watu wawili walikamatwa nchini Brazil kwa madai ya kuwa vinara wa maandamano ya kupinga gharama za ziara ya Papa Francis nchini humo juzi. 
Aparecida, Brazil. Mbali ya kufurahia mapokezi makubwa nchini Brazil, ziara ya Papa Francis imeingia doa baada ya bomu kugunduliwa chooni katika mji ambao atauzuru leo.
Bomu hilo la kutengenezwa kienyeji liligunduliwa na maofisa usalama likiwa katika choo katika Kanisa la Bikira Maria wa Aparecida katika mji huo mdogo ambao kiongozi huyo atautembelea kama sehemu ya ziara yake kwa kwanza nje ya Vatican.

“Lilikuwa bomu la kutengenezwa kienyeji lenye uwezekano mdogo wa kusababisha maafa,” imeeleza taarifa ya Jeshi la Anga la Brazil.
“Ni tukio linaloshtua, limefanyiwa kazi na wana usalama ambao wamejiandaa vyema kwa ziara hii. Kwa hakika haliwezi kuzua hofu, vikosi vya usalama vimejiandaa kikamilifu kwa matukio kama haya.”
Kulingana na vyombo hivyo, bomu hilo liliteguliwa na kisha kuharibiwa baada ya kugundulika kwake katika mji huo mdogo kwenye viunga vya Rio de Janeiro baada ya mazoezi ya vikosi vya usalama, limeeleza gazeti la Grupo Estado.
Bikira Maria wa Aparecida, ndiye mwombezi wa kiimani wa Brazil, taifa lenye idadi kubwa ya waumini wa Kikatoliki duniani.
Hata hivyo idadi hiyo kwa miaka ya karibuni imeshuka kutoka asilimia 89 ya mwaka 2004 hadi 57 mwaka huu.
Leo, Papa Francis ataendesha misa takatifu nyakati za asubuhi, kukutana na Maaskofu na waseminari.
Mji huo wa Aparecida unatarajiwa kuwa na wana usalama 5,000 wakati wa ziara hiyo ya Papa Francis.
Mapema, mjini Rome, Papa Francis alishangaza wengi wakati wa kupanda ndege ya Shirika la Alitalia baada ya kuonekana akibeba begi lake dogo jeusi kwa mkono wa kushoto huku ule wa kulia akiwasalimia watu maarufu akiwamo Waziri Mkuu wa Italia, Enrico Letta aliyemsindikiza.
Mbali ya tukio hilo, Papa Francis aliwasili salama mjini Rio de Janeiro juzi mchana na kutembezwa kwa gari la wazi 
ambalo madirisha yake yalitoa nafasi kwa maelfu ya waumini wa nchi hiyo na wageni kumwona.
Wengi wao walijitokeza, kulizunguka gari hilo. Baadaye, Papa Francis aliwahutubia wawakilishi wa Serikali ya Brazil na kukutana kwa faragha na Rais Dilma Rousseff.
Katika hotuba yake fupi alisisitiza mahujaji waliowasili nchini humo kwa Siku ya Dunia ya Vijana kuonyesha moyo wa kuwajali wengine, huruma na urafiki kwa wenzao, pia mijadala ya wazi.
Aliongeza kuwa ametua Brazil kwa jina la Yesu, ‘kuwasha moyo wa upendo katika kila moyo.’
Jana, watu wawili walikamatwa baada ya maandamano katika Mitaa ya Rio ambako watu walikuwa wakipinga gharama za ziara hiyo.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...