JENGO lenye gholofa 15 lililojengwa kwenye Barabara ya Barack Obama, hatua chache kutoka kwenye Ikulu ya Tanzania jijini Dar es Salaam limeshangaza wengi baada ya waliodaiwa kutoa kibali cha ujenzi kupandishwa mahakamani Jumatano iliyopita.
Jengo hilo lililopo hatua chache kuifikia Hospitali ya Ocean Road limezua maswali mengi kutoka kwa wakazi na wafanyakazi wa mitaa hiyo baada ya ujenzi huo kumalizika na ndipo serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa nchini (Takukuru) ikawapandisha kortini wahusika.
Inadaiwa kuwa, kwa kawaida serikali hairuhusu kujenga majengo marefu umbali wa mita mia kutoka ikulu. Jengo hilo linadaiwa kujengwa ndani ya mita 100 kutoka ikulu.
WALIOPONZWA NA KUTOA KIBALI CHA UJENZI
Jumatano iliyopita, Mtendaji Mkuu na Msanifu Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa vibali hivyo.
Maofisa hao ni Makumba Kimweri (Mtendaji Mkuu) na Richard Maliyaga (Msanifu Mkuu) walifikishwa kortini hapo na kusomewa mashitaka yanayowakabili na Wakili wa Serikali, Leonard Swai mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Sundi Fimbo.
Swai alidai mahakamani hapo kuwa Agosti 6, 2007 Kimweri akiwa Mtendaji Mkuu wa TBA kwa kutumia vibaya madaraka yake alisaini hati ya makubaliano yenye namba TBA/JVA/DSM/ROI/001 kati ya TBA na Kampuni ya Royalle Orchard Inn Ltd akiwa na lengo la kuanzisha ujenzi na wamiliki binafsi wa umma wa ghorofa 15 kwenye Kitalu namba 45 Mtaa wa Chimara, Wilaya ya Ilala bila eneo hilo kufanyiwa upembuzi yakinifu.
WENGI WALIKUWA WAKIJIULIZA KABLA YA WAHUSIKA KUSHTAKIWA
Upo ushahidi mkubwa kwamba, hata kabla ya Takukuru kuchukua hatua hiyo, wakazi wa Jiji la Dar waliokuwa wakupita eneo hilo, swali lao kubwa lilikuwa: Hivi ni kwa nini jengo refu kama hilo limejengwa jirani na ikulu?
Swali hilo lilikosa majibu hadi Jumatano iliyopita ambapo Takukuru iliwafikisha kortini maofisa hao wa TBA.
No comments:
Post a Comment