Maelfu ya wananchi wa Brazil katika mitaa ya Rio de Janeiro wameivamia na kulizunguka gari lilokuwa limembeba Baba Mtakatifu Francis 1 wakati msafara wake ulipopotea njia ulipokuwa ukitokea uwanja wa ndege alipowasili nchini humo kwa ziara.
Katibu wa Usafiri wa Rio Carlos Osorio amesema gari aina ya Fiat alilokuwemo Baba Mtakatifu lilikuwa likitokea uwanja wa ndege kuelekea katikati ya mji, lilipita njia tofauti lilipofika katika mgawanyiko wa barabara 12 unaofahamika kama Avenida Presidente Vargas.
Badala ya kupita njia za upande wa kushoto za mgawanyiko huo ambako hakukuwa na msongamano wa magari, gari hilo lilipita njia za upande wa kulia ambako kuna magari mengi yakiwemo mabasi na teksi nyingi, hatua iliyosababisha gari hilo kusimama.
Maelfu ya watu waliokuwa wamejipanga mitaani walilikimbilia gari hilo na kufika katika dirisha la upande alipokaa , huku wengi wao wakimpiga picha.
Msemaji wa Vatican Padri Federico Lombardi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini amesema Baba Mtakatifu hakuwa na wasiwasi na usalama wake, japokuwa Katibu wake aliyekuwa wamekaa naye aliingiwa na woga.
Imeelezwa kuwa Baba Mtakatifu alitoa mkono nje na kuwapungia watu hao waliokuwa wamezunguka gari hilo.
CHANZO: Mo blog
No comments:
Post a Comment