Na Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
Tumeona, kuwa pale Addis Ababa, na mbele ya ’ Simba wa Yudah’- Mfalme Haile Selassie, Nelson Mandela alitoa hotuba iliyosheheni hoja nzito na iliyowasisimua wajumbe na hata kuwabadili misimamo yao ya awali.
Na hapa ni kipande tu cha maelezo ya hotuba ile;
“ Ndio kwanza nimetoka nje ya mipaka ya Afrika Kusini huku miezi kumi iliyopita nikiwa naishi mafichoni kama mtu ninayetafutwa. Nimekuwa mbali na familia yangu na watoto wangu. Nilipolazimishwa kuishi maisha haya, basi, nikafanya tangazo kwa umma , nikiujulisha, kuwa sitaikimbia nchi yangu, bali nitabaki kuendelea na mapambano nikiwa mafichoni, ndani ya ardhi ya nchi yangu. Nilimaanisha nilichosema na nitaheshimu ahadi yangu hiyo.” – Nelson Mandela.
Baada ya kauli hiyo iliyomaanisha kuwa Mandela alikuwa tayari kurudi nchini mwake kuendelea na mapambano, basi, ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe. Nelson Mandela akawa amefanikiwa kujenga hoja na kuifanya ANC isafishike na ikubalike.
Baada ya hapo, Mandela akakutana na mtihani wa kumshawishi na kumbadilisha kimsimamo Kenneth Kaunda wa Zambia. Kaunda alikuwa bado akiamini katika njia na labda propaganda za PAC. Endelea na simulizi hii...
Mandela anasimulia juu ya kikao chake na Keneth Kaunda akiwa
pamoja na Rais wa ANC, Oliver Tambo. Wakati huo Kaunda alikuwa ni Rais wa chama cha kupigania uhuru wa Rhodesia ya Kaskazini ambayo sasa inaitwa Zambia. Chama alichokiongoza Kaunda kiliitwa UNIP- United National Independence Party of Northern Rhodesia. Na Kaunda, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya viongozi wa Afrika na vyama vya ukombozi kwa wakati huo, hakupendelea sana matumizi ya silaha katika kudai uhuru.
Na kama ilivyokuwa kwa Julius Nyerere, Kaunda naye alihofia hali ya kukosekana kwa muungano baina ya vyama vinavyopigania uhuru Afrika Kusini. Naye Kaunda, kama ilivyokuwa kwa Nyerere, alishauri ANC isubiri hadi kiongozi wa PAC, Bwana Sobukwe atoke gerezani. Ndipo hapo ANC na PAC waunganishe vikosi vyao.
Msimamo ule wa Kaunda ulimdhihirishia Mandela ukweli kuwa PAC walifanikiwa sana kusambaza ’ sumu’ dhidi ya ANC kwa viongozi wengi wa Kiafrika. Maana, Kaunda alimwambia wazi Mandela, kuwa ana mashaka na ushirika wa ANC na Chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini.
Na Mandela alipojitahidi kuweka mezani hoja ya kuwa UNIP ya Kaunda ilipotoshwa na PAC kuhusiana na ANC, Kaunda aliweka mkono wake bebani kwa Mandela na kumwambia;
” Nelson, Speaking to me on this subject is like carrying coals to Newcastle”- Kenneth Kaunda ( Mandela, Long Walk To Freedom, pg. 352)
Kwamba kwa Mandela kumweleza Kaunda juu ya jambo hilo ni sawa na mtu kupeleka makaa ya mawe Newcastle, ambako ndiko yanakochimbwa. Kaunda alitaka kumwonyesha Mandela kuwa analifahamu fika jambo hilo.
Hata hivyo, Kaunda alimthibitishia Mandela kuwa anaiunga mkono ANC na Rais wake Chifu Lithuli. Isipokuwa, kuhusiana na suala hilo, yeye kama Kaunda hakuwa na maamuzi peke yake. Kaunda akawashauri Mandela na Tambo wakamwone Bw. Simon Kapwepwe ambaye ni Makamu wa Rais wa UNIP.
Mandela akamwomba Oliver Tambo wawe pamoja kwenye mazungumzo na Kapwepwe siku ya pili yake, lakini, Oliver Tambo akasita kwa kutamka;
” Nel, you must see him on your own. Then you can be completely frank”
Kwamba Oliver alimwambia Mandela amwone Kapwepwe akiwa peke yake na kuwa angeweza kumwambia kila kitu, na kwa ukweli.
Mandela anasimulia, kuwa alitumia siku nzima kuzungumza na Kapwepwe. Ndipo hapo Mandela akafahamu zaidi hofu iliyopo kwa baadhi ya viongozi wa Kiafrika juu ya ANC. Kapwepwe alimwambia Mandela kuwa ana taarifa kutoka PAC kuwa ANC inashirikiana na Chama cha Kikomunisti na kuwa hata dhana ya ’ Umkhonto we Sizwe’ ni zao la kifikra la chama cha Kikomunisti na Liberal Party- Chama cha Kiliberali. Na kwamba wazo zima ni kuwafanya Waafrika weusi kuwa chambo kwenye mapigano.
Mawazo hayo ya Kapwepwe yalimshangaza sana Mandela, na kwamba hakuweza kuamini ni kwa namna gani kwa akili ya kawaida tu Kapwepwe ameshindwa kubaini kuwa ni tuhuma zisizo na msingi dhidi ya ANC. Kwamba ni tuhuma za uongo. Maana, inafahamika kila mahali, kuwa Chama cha Kikomunisti na Chama cha Kiliberali ni mahasimu wakubwa. Kwamba hawawezi kukaa meza moja na kucheza karata.
Mandela akamalizia kwa kumweleza Kapwepwe juu ya yeye Mandela kusikitishwa kwake na PAC kwa kusambaza uongo huo. Na mwisho wa siku Mandela akafanikiwa kumbadilisha Kapwepwe kimsimamo. Na Kapwepwe akamuahidi Mandela, kuwa, yeye mwenyewe Kapwepwe, kuwa angeitisha mkutano kuitetea hoja ya ANC. Na Kapwepwe akafanya kama alivyoahidi.
Mandela akaondoka Addis Ababa akiwa amepata mafanikio makubwa. Na safari yake katika mataifa ya Afrika ikamfikisha Misri, na hata Sierra Leone, kwa kutaja nchi chache.
Je, unajua nini kilimtokea Mandela alipofika Sierra Leone?
CHANZO: Mjengwa blog
No comments:
Post a Comment