PICHANI: Mwimbaji Lady Jaydee ambaye ni balozi wa Fistula nchini,kwa kushirikiana na CCBRT anafanya kazi ya kusaka wanawake wenye matatizo ya fistula akiwa kama Balozi. Hapa akizungumza na mmoja wa wagonjwa kutoka Mkoani Tanga.
Fistula ni ugonjwa unaowasumbua akina mama wajawazito pindi wanapokaribia kujifungua.
Fistula obsterikia ina maana ya tundu linalotokea wakati mwanamke anapojifungua katika
misuli kati ya uke na kibofu cha mkojo au kati ya uke na njia ya haja kubwa au vyote
viwili. Katika nchi zinazoendelea sababu ya fistula ni kutokana na uzazi pingamizi unaohusiana na hali ambayo nyonga ya mama ni ndogo na hivyo hushindwa kuruhusu kichwa
cha mtoto kupita salama. Katika mazingira yenye kuwa na huduma za dharura za uzazi,
hususani watoaji wa huduma za upasuaji wa kutoa mtoto, wanaweza kudhibiti matukio
mengi ya uzazi pingamizi. Wakati ambapo huduma ya upasuaji wa kumtoa mtoto
haipatikani au haitolewi kwa wakati unaofaa, msukumo wa kichwa cha mtoto unaweza
kusababisha misuli ya uke ishindwe kufanya kazi na hivyo kujiachia na matokeo yake ni
mama kupata fistula, au tundu kwenye misuli. Karibu kwa kila tukio la fistula, uzazi
pingamizi pia unasababisha kifo cha mtoto aliyeko bado tumboni.
Ugonjwa huu hufahamika kama ugonjwa ambao muathirika huwa anatokwa na haja ndogo mara kwa mara bila kutegemea.
Zaidi ya hivyo, wanawake waliopo katika hali hiyo, mara nyingi wanaishi katika mazingira ambayo afya yao wenyewe hawaipi kipaumbele na huduma zilizopo hazitoshelezi. Matatizo ya fistula ni makubwa.
Wanawake wenye fistula wanapata matatizo mengi ya kitiba ikiwa ni pamoja na kushindwa kudhibiti mkojo na/au kinyesi (ufukunyungu),maambukizo ya kibofu cha mkojo, vidonda kwenye uke. Pia kati ya wanawake watano, mmoja anaugua ugonjwa wa “ulemavu wa kanyagio” unaosababisha kuharibika kwa mishipa katika mguu
mmoja au yote na kusababisha ulemavu wa kutembea.Kwa wanawake wengi mzunguko wao wa hedhi huathirika na wengine wanapoteza
uwezo wao wa kushika mimba. Kijamii kuna matatizo makubwa zaidi. Kimsingi mwanamke mwenye fistula anaweza kukataliwa na mume wake kutokana na kutokwa na mkojo na/au kinyesi bila kujizuia na hali ya uchafu alionayo. Wakati mwingine hata familia yake alikozaliwa wanakataa kumchukua. Anakuwa ametengwa na jamii na anaweza kudhihakiwa au kulaumiwa kwa yaliyomtokea. Pamoja na matatizo hayo, wanawake wanaomudu kuishi na tatizo la fistula huwa wana ujasiri mkubwa na ni imara.
Je, fistula inatibika?
Fistula inaweza kutibiwa kwa upasuaji hata ikiwa miezi au miaka kadhaa baada ya kutokea, na dalili nyingi au zote zinaweza kuondolewa na mama anaweza kurudia hali ya utu wake na kuishi maisha ya kawaida.Upasuaji wa fistula unahitaji saa moja hadi saba
Je,fistula inazuilika?
Ili kuzuia fistula, upatikanaji wa huduma ya afya ni muhimu. Kunahitajika mchanganyiko wa huduma bora kabla ya kujifungua ikiwa ni pamoja na uchunguzi, kuwepo na wakunga wenye ujuzi wakati wa kujifungua, na kutolewa kwa matibabu ya haraka inapotokea dharura na huduma bora baada ya kujifungua, yote haya yanaweza kuokoa maisha ya kina mama na kuzuia ulemavu wa aina nyingi ikiwa ni pamoja na fistula obstetrikia.Katika kukusanya kwangu habari,nimeona kuwa matibabu ya fistula yanatolewa bure katika hospitali ya Bugando iliyopo Mwanza na CCBRT iliyopo Dar es salaam.(Mnaweza kusahihisha kama kuna hospitali nyingine zaidi ya hizi).
Tusaidie kuwaelekeza kwenda katika hospitali hizi wakina mama wenye matatizo haya na wapo tu nyumbani wanateseka na kunyanyapaliwa wakati tatizo lao linatibika kabisa.
No comments:
Post a Comment