Friday 30 August 2013

Kikwete amlilia Askofu Kulola asema Tanzania imepoteza Mtumishi wa Mungu

Marehemu Dr. Moses Kulola



THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


Coat of Arms
PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Kiongozi wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu Mkuu Moses Kulola ambaye ameaga dunia , Alhamisi, Agosti 29, 2013 katika Hospitali ya AMI iliyoko Masaki mjini Dar Es Salaam akiwa na umri wa miaka 84.

Rais kikwete ameelezea mshtuko na huzuni yake katika Salamu za Rambirambi alizomtumia Katibu Mkuu wa Kanisa hilo Bwana Brown Mwakipesile kufuatia kifo cha Askofu Mkuu Kulola. 

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mtumishi wa Mungu wa muda mrefu na Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Marehemu Moses Kulola kutokana na maradhi yaliyomfanya wakati fulani apelekwe hadi India kupatiwa matibabu” amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Askofu Moses Kulola kwa miaka mingi wakati wa enzi za uhai wake, kama Mtumishi Hodari wa Kiroho aliyejitoa vilivyo katika kuwahudumia Waumini wa Kanisa lake ambapo mahubiri yake yametoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani za Waumini wake na kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu.

Aidha Rais Kikwete amesema kifo cha Askofu Mkuu, Moses Kulola kimeacha pengo kubwa siyo tu kwa Waumini wa Kanisa lake hapa nchini, bali pia miongoni mwa wapenda amani kote nchini na kwingineko duniani kwa vile enzi za uhai wake, Marehemu aliweza kufikisha ujumbe muhimu wa kiimani kupitia mahubiri yake kwa watu wa mataifa mbalimbali ndani na nje ya  Bara la Afrika.

“Kwa niaba yangu mwenyewe na Serikali ninayoingoza, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa Kanisa la Evangelical Assembies of God Tanzania, Bwana Brown Mwakipesile na Waumini wote wa Kanisa hilo Salamu za Rambirambi  kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza Kiongozi muhimu wa Kiroho.  Ninawajulisha kuwa niko nanyi katika wakati huu mgumu kwa sababu msiba wenu ni msiba wetu pia. Sala na mioyo yetu iko nanyi wakati wa maombolezo ya kifo cha Kiongozi huyo shupavu wa dini. Nawaomba wote muwe wavumilivu na wenye subira kwani yote ni Mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.

“Vilevile kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu, Askofu Mkuu, Moses Kulola kwa kumpoteza Baba, Kiongozi Shupavu na Mhimili wa familia.  Natambua fika kwamba hiki ni kipindi kigumu sana kwao cha maombolezo.  Natambua machungu yenu wakati huu na naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke peponi roho ya Marehemu Moses Kulowa. Amina.”

Mazishi ya Marehemu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) yatafanyika mjini Mwanza Jumatano ijayo tarehe 4 Septemba, 2013.  Heshima za mwisho kwa mwili wa Kiongozi huyo zitatolewa siku ya Jumamosi tarehe 31 Agosti, 2013 katika Kanisa la EAGT karibu na Hospitali ya Temeke kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.00 mchana.   

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Agosti, 2013

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...