Monday, 12 August 2013

PONDA MBARONI



Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro alikopekewa baada ya kudaiwa kupigwa risasi mkoani humo juzi. Kulia akiwa amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (MoI), jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutibiwa jeraha katika bega lake la mkono wa kulia.


  Alazwa MOI ana jeraha pegani
  Polisi waimarish lindo wodini


Ofisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi wa MoI, Mary Ochieng, akizungumza na NIPASHE jana alisema, Sheikh Ponda alipelekwa hospitalini hapo jana saa 5:00 asubuhi akiwa na majereha katika mkono wa kulia.


“Bado madaktari wanamchunguza, lakini amepata bullet injury, hali yake siyo mbaya anaendelea vizuri, anaongea na anajitambua,” alisema Ochieng na kuongeza kuwa taarifa za kama majeraha hayo yanatokana na risasi zitatolewa baada ya uchunguzi wa kina wa daktari.

NIPASHE ambayo ilifika MOI ilikuta maofisa wanne  wa polisi waliovalia nguo za kiraia wakiwa wameketi karibu na eneo analofanyiwa uchunguzi Sheikh Ponda huku gari la polisi lenye namba za usajili T 662 APM likiwa na askari wengine likiwa limeegeshwa karibu na lango la mapokezi la MOI.

Awali Kamishina wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam (CP), Suleiman Kova, alisema wamemkamata Sheikh Ponda na kwamba yupo chini ya ulinzi wa polisi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuahidi leo kutoa taarifa rasmi ya tukio hilo.

Mpwa wa Sheikh Ponda, Ishaka Rashid, akizungumza na NIPASHE alisema walimpeleka Ponda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili saa 4:30 asubuhi na baada ya kufika hapo walielezwa kuwa inatakiwa wakapate fomu ya matibabu (PF3) kutoka polisi ndipo atibiwe.

Alisema baada ya kupewa maelekezo hayo, walikwenda katika kituo cha polisi cha Salender Bridge kuomba PF3 na polisi walieleza kuwa watakuwa tayari kutoa fomu hiyo baada ya kumwona mgonjwa huyo.

Rashid alisema baadaye waliongozana na polisi wa kituo hicho ambao walikwenda Muhimbili kumhoji Sheikh Ponda na baada ya kumaliza kuchukua maelezo walitoa PF3.

Alisema Sheikh Ponda alianza kufanyiwa uchunguzi saa 7:00 mchana kwa kufanyiwa X-Ray Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kubainika kuwa mfupa mkubwa umepata madhara kutokana na risasi alizopigwa na baadaye akahamishiwa MoI.

Akizungumzia tukio lilivyotokea mkoani Morogoro, alisema Sheikh Ponda baada ya kumaliza kuhutubia waumini wa Kiislamu kitendo kilichomchukua dakika saba alipanda teksi kuelekea msikiti wa Mungu Mmoja.

Alisema akiwa njiani ghafla magari matatu ya polisi yalifika eneo hilo na kuzuia teksi aliyokuwa amepanda na kupiga risasi hewani kutawanya umati wa watu hali iliyomlazimu Ponda atoke ndani ya gari hilo.

Rashid alisema baada ya kutoka ndipo inadaiwa polisi mmoja aliyekuwa katika gari mojawapo la polisi alimpiga risasi Sheikh Ponda katika mkono wake wa kulia na baadaye polisi waliondoka katika eneo la tukio.

Alisema baada ya tukio hilo, Sheikh Ponda alichukuliwa na waumini wa Kiislamu kupelekwa katika Zahanati ya Islamic Foundation na baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na polisi walipofika hospitalini hapo kulifanyika utaratibu wa kumwondoa.

Rashid aliongeza kuwa baadaye zilisambazwa taarifa nchi nzima kuwa Sheikh Ponda ameuawa wakati siyo kweli na kwamba hali yake inaendelea vizuri.

Alisema kinachoshangaza na kutia mashaka ni kwamba katika tukio hilo, licha ya kwamba kulikuwa na watu wengi lakini askari aliyepiga risasi alimlenga Sheikh Ponda tu.

WAISLAMU WATAKA TUME HURU
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimeitaka serikali kuunda tume ya wazi kuchunguza tukio la polisi kumshambulia Sheikh Ponda kwa risasi, vinginevyo watalazimika kufikiri upya nafasi yao kama Waislamu hapa nchini.

Tamko hilo lilitolewa jana na Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Baraza Kuu), Sheikh Mussa Kundecha, alipozungumza na waandishi wa habari, katika Msikiti wa Mtambani, jijini Dar es Salaam.

Alisema wanaamini kitendo kilichofanywa na polisi dhidi ya Sheikh Ponda, ni sheria kuchukuliwa mkononi, kinyume cha makemeo ambayo yamekuwa yakitolewa na vyombo vya dola dhidi ya raia na kwamba, kwa hatua hiyo, Waislamu wote wako hatarini.

Sheikh Kundecha alisema kama serikali ilikuwa inamtafuta Sheikh Ponda, upo utaratibu wa kufuata, ikiwa ni pamoja na kumwandikia barua na siyo kutumia vyombo vya habari kama ilivyofanya.

Pia alisema hata kama kuna kosa, ambalo halijulikani, lililoifanya polisi kumtafuta Sheikh Ponda, basi adhabu haiwezi kuwa kumlenga shabaha hadharani kwa risasi na kwamba, alikuwa bado hajahukumiwa na mahakama.

“Tuna taarifa kwamba, Sheikh Ponda amepigwa risasi na yuko hospitali…kama serikali iliweza kupeleka jeshi Mtwara kudhibiti vurugu, ilishindwaje kwa Sheikh Ponda, ambaye ni mtu mmoja?” alihoji Sheikh Kundecha na kuongeza:

“Tunataka uchunguzi ufanyike, iundwe tume ya wazi kubaini mashambulizi hayo ya risasi.  Askari aliyehusika achukuliwe hatua.”


POLISI WAUNDA TIMU
Wakati hali ikiwa hivyo, Jeshi la Polisi nchini limeunda timu kuchunguza tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda, itakayoongozwa na Kamishna Issaya Mngulu.

Taarifa ya Msemaji wa Polisi, Advera Senzo, kwa vyombo vya habari jana haikukanusha wala kuthibitisha Polisi kumjeruhi Ponda na badala yake ilieleza kwamba timu hiyo inawashirikisha wajumbe kutoka jukwaa la haki jinai na kwamba imekwisha kuanza kazi.

Taarifa ya Polisi ilieleza kwamba juzi Agosti 10, majira ya saa 8 mchana maeneo ya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, kulifanyika kongamano la Baraza la Idd lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Kiislamu Mkoani Morogoro na kwamba dakika 10 kabla ya kongamano hilo kumalizika, alifika Sheikh Ponda, ambaye alizungumza kwa muda mfupi.
 
Ilieleza kuwa kongamano hilo lilifungwa majira ya saa 12:05 jioni na polisi walizuia gari alilokuwa amepanda Ponda ambaye anatuhumiwa kwa kosa la kutoa maneno ya uchochezi sehemu mbalimbali hapa nchini yenye mrengo wa kusababisha uvunjivu wa amani.

“Baada ya askari kutaka kumkamata, wafuasi wake walizuia ukamataji huo kwa kuwarushia mawe askari.
 
Kufuatia purukushani hiyo, askari walipiga risasi hewani kama onyo la kuwatawanya... hivi sasa imethibitika kuwa Sheikh Ponda yuko katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akitibiwa jeraha katika bega la mkono wa kulia linalodaiwa alilipata katika purukushani hizo.”

Taarifa ya Polisi iliongeza kuwa: “kufuatia tukio hilo, timu inayoshirikisha wajumbe kutoka Jukwaa la Haki Jinai ikiongozwa na Kamishina wa Jeshi la Polisi CP Issaya Mngulu imeanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo. 

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa  wananchi kuwa watulivu wakati suala hili linashughulikiwa kisheria.”

POLISI MOROGORO
Awali, Polisi mkoani Morogoro walisema Ponda alikuwa ametoroka na kumtaka ajisalimishe polisi au ndugu yake akathibitishe kama kweli kiongozi huyo alikuwa amejeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro, Faustine Shilogile, alisema walikuwa na taarifa kwamba Ponda alikuwa amefichwa mkoani Morogoro na kwamba anaendelea kutafutwa akiwa amepigwa risasi au hajapigwa risasi.

Alisema taarifa za kwamba jeshi hilo limehusika kupiga risasi siyo kweli kwa kuwa hajaonekana ili kuonyesha kuwa amepata majeraha sehemu yoyote ya mwili wake.

“Risasi haifichiki, kama amepigwa angejitokeza ili kupewa kibaki cha matibabu,” alisema.
Kamanda Shilogile alisema anashangazwa na taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuwa Sheikh Ponda ameuawa na polisi wakati hawajui alipo.

Hata hivyo, alisema polisi inawashilikia watu wawili ambao hakutaka kuwataja majina kutokana na uchunguzi na kueleza kuwa linawatafuta viongozi watano wa kundi ambalo liliandaa kongamano hilo.

Shilogile alisema waandaji wa kongamano hilo walipewa kibali na jeshi hilo kwa ajili ya kufanya kongamano kwa masharti ya kutotoa matamshi ya uchochezi ikiwa ni pamoja na Sheikh Ponda kutohutubia kwa kuwa anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kufanya uchochezi.

Alisema Ponda alikuwa akitafutwa kutokana na kuvunja masharti ya mahakama kwa kufanya miadhara ya uchochezi katika maeneo mbalimbali.

Alisema wakati wa kongamano hilo, Ponda alipewa dakika tano kuzungumza na alieleza kuwa yeye siyo mzungumzaji kwa siku hiyo na badala yake angezungumza jana katika viwanja vya msikiti wa Jabal Hira.

Alisema baada ya hapo, mkutano ulifungwa na wafuasi wake wakaanza kusukuma gari alilokuwa amepanda katika barabara ya Tumbaku na kwa kuwa alikuwa akifutwa; askari walimfuata kutaka kumtia mbaroni.

Kamanda Shilogile alisema kabla ya polisi kumtia mbaroni wafuasi walianza kurusha mawe kwa askari na ndipo polisi walifyatua juu risasi tatu za baridi ili kuwatawanya, lakini walizidiwa nguvu na wafuasi hao na kufanikiwa kumtorosha kwa njia ya pikipiki.

Alisema baadaye zilizagaa taarifa kuwa amepigwa risasi ya begani na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa na baadaye kutoroshwa kusikojulikana na kwamba polisi hawajathibitisha tukio hilo.

Katika hatua nyingine, watu wanaohisiwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda walivamia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na kufanya uharibifu wa kuvunja vioo katika wodi namba sita ya watoto, wakishinikiza kuonyeshwa Sheikh huyo ambaye ilikuwa ikidaiwa amefichwa na Jeshi la Polisi katika hospitali hiyo.

Baadhi ya wagonjwa waliolazwa na watoto wao katika wodi hiyo, Kibua Michael na Cecilia Clemence ambao ni wakazi wa mjini hapa kwa nyakati tofauti walieleza wafuasi hao walikusanyana nje ya hospitali hiyo walirusha mawe na kusababisha tahuruki kwa baadhi ya wagonjwa.


SKYNEWS NA PONDA
Wakati hali ikiwa hivyo nchini, Shirika la Habari la Sky News, limetoa ripoti inayomhusisha Ponda na mashambulizi ya mabinti wawili wa Uingereza waliomwagiwa tindikali visiwani Zanzibar, wiki iliyopita. 

Ripoti hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Mashambulizi ya tindikali Zanzibar: Mhubiri mtuhumiwa akamatwa’ ilieleza kwamba tukio hilo lilitokana pia na imani za kidini.

Mabinti hao wa Kiingereza, Katie Gee na Kirstie Trup, wote wenye umri wa miaka 18, walijeruhiwa visiwani Zanzibar Agosti 7, mwaka huu na kwa sasa wanatibiwa jijini London, Uingereza na hali zao zimeelezwa kuendelea vizuri.

Taarifa ya Sky News ilieleza kwamba polisi visiwani humo wamekwishahoji watu watano kutokana na tukio hilo.

Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imewataka raia wake wanaokuja Tanzania Bara na Visiwani kuchukua tahadhari ya ziada kwa sababu tukio la kumwagiwa tindikali mabinti hao ‘lilikuwa ni zaidi ya tukio la jinai.’

Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Muhibu Said na Restuta James, Dar; na Ashton Balaigwa, Morogoro.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...