Monday, 23 September 2013

‘Hukumu ya kina Masogange haitawanusuru watumishi JNIA’


Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, Agosti  17, mwaka huu, Dk Mwakyembe alitoa agizo la kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi, Koplo Juliana Thadei, Jackson Manyoni, Yusuph Daniel Issa, Koplo Ernest na Mohamed Kalugwan.               


Dar es Salaam. Licha ya Watanzania wawili, Agnes Gerald (Masogange) na Melisa Edward kuachiwa huru, wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam waliobainika kushiriki kuwapitisha wataendelea kuchunguzwa.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki alisema jana kwa simu kuwa wafanyakazi hao, wataendelea kushtakiwa kwa sababu walikiuka maadili ya kazi yao.
“Hata kama hao waliowasaidia wameachiwa huru au walichokibeba hakikuwa dawa za kulevya lakini kwa kuwa wafanyakazi hao walivunja kanuni za kazi, wataendelea kushtakiwa kisheria,” alisema Malaki.
Mkurugenzi huyo alisema uongozi wa uwanja huo wa ndege una ushahidi wa kimazingira wa jinsi wafanyakazi hao walivyoshiriki kuwasaidia kina Masogange kupitisha mzigo huo na kwa ushahidi huo, watashtakiwa kwa kukiuka maadili ya kazi zao.
“Sheria za kazi zikisema usiongee na simu kazini, wewe ukaongea, basi tayari umevunja kanuni. Hao wafanyakazi wameshiriki kuupitisha mzigo huo na Mahakama ya Afrika Kusini haikuwaachia hao wasichana huru kwa kuwa hawakuonekana na kosa, walihukumiwa na mmoja wao amelipa faini ndiyo maana wapo huru. Mmoja wao alipatikana na kosa,” alisema Malaki.
Malaki alisema uongozi wa uwanja wa ndege utawachukulia hatua wafanyakazi watakaobainika kushiriki kwa namna moja au nyingine.
Mahakama ya Kempton ya Afrika Kusini wiki iliyopita ilimhukumu Masogange kifungo cha miezi 30 au kulipa faini ya Randi 15,000 (sawa na Sh2.4 milioni). Alilipa na kuachiwa huru. Melissa aliachiwa huru baada ya kuonekana hana hatia.
Baada ya Masogange na Melisa kukamatwa, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliagiza uchunguzi wa kina ufanyike kwenye uwanja huo ili kujua namna wasichana hao walivyopitisha mzigo huo.

Uchunguzi wa Mwakyembe kwa msaada wa kamera za CCTV ulifichua tukio zima la Masogange na Melissa kupitisha mzigo wao uwanjani hapo na jinsi baadhi ya wafanyakazi wa JNIA walivyoshiriki kuwasaidia kuupitisha.
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, Agosti  17, mwaka huu, Dk Mwakyembe alitoa agizo la kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi, Koplo Juliana Thadei, Jackson Manyoni, Yusuph Daniel Issa, Koplo Ernest na Mohamed Kalugwan.
Hukumu yaishangaza Tume



Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania imesema imeshangazwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kempton ya Afrika Kusini dhidi ya Watanzania hao na mazingira ya dawa hizo kubadilika na kuwa kemikali.
Msemaji wa tume hiyo, Florence Mlay alisema, itatoa tamko rasmi leo kuhusu hukumu hiyo, huku akisisitiza kwamba inashangazwa ni kwa namna gani watuhumiwa hao wameachiwa huru kwa kutozwa faini ndogo huku mzigo walioubeba ukigeuka kemikali badala ya dawa.
“Hatuwezi kuzungumza sana kuhusu hili lakini ni lazima sisi kama tume tuangalie ni kwa nini ule mzigo awali ulionekana ni dawa za kulevya aina ya methamphetamine na sasa zimegeuka kuwa ni kemikali,” alisema Mlay.
Hata hivyo, Msemaji wa Kitengo cha Kusimamia Makosa ya Jinai wa Afrika Kusini, Kapteni Paul Ramaloko alisema Mahakama imeamua kuwa watu hao walibeba kemikali na si dawa za kulevya na wanaheshimu uamuzi huo.
Alisema hata kama watuhumiwa hao wameachiwa huru kwa faini au hukumu ndogo, jambo muhimu kwao ni kwamba angalau walipatikana na hatia.

“Kazi yetu kubwa ni uchunguzi wa makosa ya jinai, tuliwakamata watu hawa uwanja wa ndege kwa kosa la kubeba dawa za kulevya. Mahakama imeona kuwa si dawa, bali ni kemikali na sisi hatuna la kufanya zaidi ya hapo,” alisema.
CHAZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...