Hawa ni baadhi ya majeruhi wakipatiwa huduma ya
kwanza na wasamaria wema , Picha na AFP
Nairobi. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ni
miongoni mwa watu waliopoteza ndugu zao wa karibu katika tukio la mauaji
ya kigaidi lililotokea Jumamosi katika duka kubwa la Westgate jijini
Nairobi.
Rais Kenyatta alibainisha vifo hivyo katika hotuba
yake aliyoitoa kupitia televisheni usiku wa kuamkia jana, iliyolenga
kuwapa pole Wakenya wote waliopoteza ndugu Hata hivyo, Kenyatta hakutaja
majina ya ndugu zake waliopoteza maisha. Katika shambulio hilo
lililohusisha matumizi ya maguruneti na risasi, watu takriban 59
waliuawa na kuacha majeruhi 175. Kikosi cha wanamgambo wa Al-Shabaab
kimekiri kuhusika.
Ndani ya jengo hilo lililopo kilomita 10 Kaskazini
Mashariki mwa kitovu cha Jiji la Nairobi, alikuwepo pia mtoto wa kiume
wa Kenyatta, Jomo Kenyatta na dada wa Kenyatta, Kristina Pratt ambao
waliokolewa bila majeraha yoyote.
Pia Kenyatta alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu
wananchi juu ya shambulio hilo kubwa kuwahi kutokea nchini humu baada
ya lile la kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani na kikundi cha kigaidi cha
Al-Qaeda mwaka 1998 lililoua watu 32.
“Tulishawahi kukumbana na mashambulio ya kigaidi
hapo awali. Tulipigana kishujaa bila kuchoka na tuliushinda ugaidi nje
na ndani ya mipaka yetu. Wakati huu pia tutawashinda. Ugaidi kwa kifupi
ni falsafa ya woga,” alisema Kenyatta katika hotuba yake ya kwanza
kuhusu shambulio hilo la kigaidi.
Hadi kufikia jana jioni, Serikali ilikuwa haijatoa
idadi kamili ya mateka wanaoendelea kushikiliwa na wanamgambo hao
wanaokadiriwa kuwa kati ya 10 na 15 ambao bado wapo ndani ya jengo hilo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment