Nairobi. Wakati magaidi wawili wakiwa wameuawa, Serikali ya Kenya imesema idadi ya watu waliokufa katika tukio la kigaidi kwenye maduka makubwa ya Westgate, Nairobi imefikia 62.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mchana, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku alisema watu waliojeruhiwa ni 175 baada ya magaidi hao kuvamia eneo hilo la maduka tangu Jumamosi iliyopita.
Ole Lenku alisema pia kuwa askari 10 wamejeruhiwa katika operesheni hiyo inayowahusisha maofisa wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad), wale wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Alisema askari waliojeruhiwa na raia wanatibiwa katika hospitali mbalimbali za Nairobi.
Magaidi wawili wauawa
Alisema magaidi wawili waliuawa na vikosi vya usalama huku mapambano yakiendelea. Alisema waasi hao wamebanwa baada ya vikosi vya ulinzi na usalama kudhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo.
Magaidi hao wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la Al-Shabaab la Somalia walivamia jengo hilo la ghorofa nne ambalo lina maduka ya kifahari na kuua, kujeruhi na kuwashikilia wengine mateka.
“Tumeua magaidi wawili na wengine kadhaa wamejeruhiwa, tutatoa taarifa nyingine baadaye. Hakuna gaidi hata mmoja ambaye ataondoka,” alisema Ole Lenku na kuongeza: “Ni labda wajisalimishe au wauawe.”
Alisema magaidi hao wamejaribu kuwasha moto katika duka la Nakumatt lililopo katika jengo hilo la Westgate ili kuvichanganya vikosi vya usalama lakini hawakufanikiwa kutokana na vikosi hivyo kuwa imara.
Ole Lenku alisema kazi ya kupambana na magaidi hao imechukua muda mrefu kutokana na vikosi vya usalama kufanya jitihada za kuokoa mateka ambao bado wanashikiliwa.
“Hadi sasa bado hatujui kuna mateka wangapi ndani ya jumba hilo,” alisema Ole Lenku.
Milio ya risasi iliendelea kurindima siku nzima ya jana ndani ya jengo hilo huku askari wengi wakiwa wamelizunguka.
Moto huo uliowashwa jana, ulisababisha moshi mkubwa na kuibua hofu miongoni mwa wananchi.
Mkuu wa Jeshi la Kenya, Jenerali Julius Karangi alisema mapambano dhidi ya magaidi hao yanapaswa kujumuisha dunia nzima.
“Tumedhibiti ghorofa zote na moto uliotokea ni wao wamejaribu kuwasha ili watoroke lakini hakuna njia ya kutoka,” alisema Jenerali Karangi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment