Elimu masafa imesaidia watu wengi kujiendeleza. Mwanzoni watu walikuwa wanashindwa kujiendeleza kwa sababu ya kukosa ruhusa kazini, lakini sasa hilo halipo tena.
Wakati Serikali ya Tanzania ikizidisha jitihada za kuongeza idadi ya wanafunzi katika madaraja ya elimu ya msingi na sekondari, hali siyo nzuri kwa upande wa elimu ya juu.
Ukweli ni kuwa Watanzania wengi wanaikosa elimu hiyo ama kwa kushindwa kumudu gharama au kwa kukosa muda wa kusoma hasa kwa wafanyakazi.
Ufumbuzi wa changamoto hii ni wananchi kusoma kwa kupitia mfumo wa Elimu Masafa,kama anavyobainisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwette, aliyehojiwa na mwandishi wetu hivi karibuni.
Swali: Tueleze historia fupi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania?
Jibu: Chuo hiki kilianzishwa mwaka 1994 kikiwa na wanafunzi 776, ambao baadhi walikuwa wa shahada ya kwanza na wengine waliokuwa katika programu ya maandalizi ya kupata sifa ya kusoma elimu ya shahada.
Mpaka sasa jumla ya wanafunzi 67,103 wameshapitia hapa katika ngazi ya elimu ya shahada, huku tukidahili wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamifu wapatao 13,491 kuanzia mwaka 2001 hadi 2013.
Swali: Baadhi ya watu wana shaka na elimu masafa ambao ndiyo mfumo mnaoutumia chuoni, unawaambia nini?
Jibu: Chuo Kikuu Huria ukilinganisha na vyuo vingine, tuko vizuri kwenye mambo mengi ya kitaaluma na hata mifumo ya uongozi.
Wanaosema elimu yetu haina ubora hawana hoja, sisi ni chuo kikuu huria, pia tunatoa elimu kwa kukutana na wanafunzi uso kwa uso.
Mwanafunzi anaweza kusoma kwa njia zozote za elimu masafa, lakini linapokuja suala la mtihani atasimamiwa na mwalimu.
Kwa sasa kuna njia mbalimbali wanazotumia wanafunzi kujisomea kama vile kutumia mitandao, ukiwamo wetu. Pia tunaandaa masomo katika kanda za CD na kuwapa wanafunzi wetu.
Aidha, tumeanza mchakato wa kuzungumza na baadhi ya kampuni za simu za mikononi, ili tuone namna tunavyoweza kutumia simu za mkononi kutoa mafunzo.
Tunajitahidi elimu yetu iwe bora na kutolewa kwa njia za kisasa kadri tutakavyoweza. Tunataka tufike mahali hizi center (vituo) zetu ziwe college (vyuo). Hili litategemea ushirikiano tutakaopewa na halmashauri za wilaya.
Kikubwa tunachotaka kutoka kwao ni majengo, hii itasaidia hata watumishi ambao kwa sasa wanasafiri kutoka wilayani kwao kwenda mkoani waachane na hilo.
Cha msingi niseme elimu masafa imesaidia watu wengi kujiendeleza. Mwanzoni watu walikuwa wanashindwa kujiendeleza kwa sababu ya kukosa ruhusa kazini, lakini sasa hilo halipo tena. Tumesaidia wengi kupata elimu kwa gharama nafuu.
Swali: Uzoefu unaonyesha moja ya mambo yanayolalamikiwa kwa kiasi kikubwa ni mifumo ya utoaji mitihani yenu, unalizungumziaje hili?
Jibu: Kwa miaka nane niliyokaa hapa, tumeboresha ubora na ulinzi wa mitihani yetu. Kwa mfano, hivi sasa hata mwalimu wa somo hajui ni maswali gani yatatoka kwenye mtihani wake.
Tumefuta mitihani isiyo na tija, mwanafunzi anafanya test (jaribio) moja yenye alama 30 baada ya hapo anafanya mtihani wa mwisho wenye alama 70.
Mfumo huo ni bora zaidi kuliko hiyo inayotumiwa na vyuo vingine. Kwa kuthibitisha ubora wa elimu yetu, Chuo Kikuu Huria ndicho chuo kikuu pekee nchini kilichopewa ithibati mara mbili. Ithibati hii hutolewa kila baada ya miaka mitano na Tume ya Vyuo Vikuu ya Tanzania (TCU).
Swali: Kwa nini kuna idadi kubwa ya watu wanaojiandikisha kusoma chuo kikuu huria, lakini wanakatisha masomo yao?
Jibu: Hali iko hivyo kwa sababu hii ni elimu huria, unaweza kuanza leo kesho ukawa na kitu kinachokubana ukaomba kuahirisha masomo.
Mpaka mwaka wa masomo unaoishia mwaka 2013 tulikuwa na wanafunzi kama 44,000, lakini wanaohudhuria na kufanya mitihani ni kama 37,000.
Hata hivyo, kwa chuo kikuu huria chochote duniani, hiyo siyo idadi ndogo, bado tupo kwenye nafasi nzuri sana.
Swali: Mafanikio gani mnayoweza kujivunia katika miaka ya karibuni?
Jibu: Kwanza ni kuondoa baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanakwaza wanafunzi katika mitihani yetu. Hivi sasa wanafunzi wanafanya mtihani kwa wakati na wanaweza kumaliza masomo bila matatizo.
Chuo hiki kimekuwa mfano wa kuigwa katika kuboresha elimu, tumejikita zaidi kwenye mfumo wa teknolojia. Kwa sasa mwanafunzi wetu anaweza kuangalia matokeo popote pale alipo. Tehama tumeitumia vizuri hata kwenye ngazi ya uongozi.
Pia tumeendelea kukitanua chuo, sasa tuna wanafunzi wanaosoma wakiwa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Namibia. Sisi peke yetu ndiyo tuliothubutu kutoka nje ya mipaka yetu.
Swali: Una wito wowote kwa Watanzania?
Jibu: Ni vyema watu wakatumia fursa ya elimu huria, Mandela (Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandela) shahada zake amepata kupitia chuo kikuu huria, na Mugabe (Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe) ana shahada nyingi na zote kazipata kupitia elimu huria.
Aidha, ni wakati muafaka kama watoto wanataka kusoma kupitia mfumo wa elimu huria waachwe. Hivi sasa watu hawako tayari kumsikiliza mwalimu kwa saa mbili au tatu, lazima na sisi twende na jinsi mabadiliko yanavyokwenda. Wazazi wasiwalazimishe watoto kusoma kama walivyo soma wao.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment