Mmoja wa wanafunzi (kulia) akionekana kufurahia usafiri wa treni. Picha na Zakaria Osanga
Swali kuu ni je, uwepo wa huduma hii umesaidia kuondoa au kupunguza shida ya usafiri?
Saa 11 kamili jioni, jijini Dar es Salaam, Saida Adam mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari Zanaki na Mery Peter (darasa la tatu) Shule ya Msingi Kisutu wanashuka kwenye treni hapa Tabata Relini.
Hakuna aliyewasukuma kuwazuia wakati wa kupanda wala aliyewazuia wasikae kwenye viti kwenye usafiri huo.
Maumbo yao madogo na wakati mwingine ubabe wa makondakta vingewapa wakati mgumu kuhimili mikiki ya abiria waliochoka wanaowania kupanda daladala.
Watoto hawa ni miongoni mwa abiria wengine karibu 14,000 ambao wanafanya safari zao kwa siku kwa chombo hicho.
Saada na Mery wanaelezea tamu ya usafiri huo ambao unatimiza mwaka mmoja tangu Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alipozindua rasmi usafiri huo.
“Ni usafiri rahisi kwa sababu hauna foleni, kwa hiyo ninawahi kufika nyumbani, sinyanyaswi na nauli yake ni ndogo (Sh100)” anasema Saada.
“Kwa mimi kama ningetumia daladala ningetumia hadi saa tatu ili nifike nyumbani” anasema Mery ambaye anamaanisha kuwa ‘treni ya Mwakyembe’ imewarahisishia kazi.
Kwa mujibu wa takwimu za Dk Mwakyembe, abiria 9000 wanasafiri kati ya Pugu Mwakanga hadi Kurasini kupitia Shirika la Reli kati ya Tanzania na Zambia (Tazara) na 5000 wanasafiri kati ya Ubungo na Stesheni kwa kampuni ya reli(TRL).
Halima Mussa ni mmoja wa abiria hao anasema “Usafiri huu ni mzuri, huduma zao nzuri, wafanyakazi ni wastaarabu nauli yao nzuri (Sh400), na unapunguza msongamano ambao tungeupata kwenye daladala,” anasema.
Furaha ya Halima inaleta kilio kisichokuwa na machozi kwa madereva, makondakta na wamiliki wa daladala.
Emmanuel Peter anamiliki daladala inayofanya safari zake kati ya Ubungo na Mnazi Mmoja kupitia barabara ya Mandela.
Ujio wa treni hiyo ya Mwakyembe uliyumbisha biashara yake na makusanyo aliyokuwa akiyapata kwa siku yalipungua.
“Kuna wakati tulikuwa tukigombana na madereva na makondakta kwa sababu hesabu ya fedha ilikuwa haitoshi,” anasema Peter.
Peter anasema abiria wanaotumia daladala walipungua japo hesabu wanayoitaka ilikuwa inafika lakini ni tofauti na ilivyokuwa hapo awali kabla Mwakyembe hajaja.
Huko Mabibo ambapo treni hiyo ina kituo ndipo kuna mapinduzi makubwa, yanawapa changamoto wenye daladala.
Kondakta wa daladala inayofanya safari kati ya Mabibo na Kariakoo, Ali Said anasema hali ya kibiashara imeshuka tangu usafiri huo wa garimoshi uchukue nafasi.
“Kipindi cha nyuma ulikuwa huwezi kukuta magari yamepangana foleni hivi muda kama huu wa asubuhi” anasema Said akionyesha daladala zilizopanga foleni kusubiri abiria wa kwenda Posta na Kariakoo.
Anaongeza kuwa abiria wanaowapata ni wale wa maeneo ya Manzese na Magomeni ambapo reli haipiti.
Kuhusu kipato, Said anakiri kuwa kimeshuka japo hataki kuweka wazi kimeshuka kwa kiasi gani.
Kondakta huyo anasema magari yanayofanya safari za Mabibo- Kivukoni yamepungua tangu treni hiyo ilipoanza safari zake Oktoba mwaka jana.
Hata hivyo wadau wengine wa daladala inapopita reli ya Tazara wanasema wao hajaathirika sana.
Dereva wa daladala inayofanya safari kati ya Kigogo na Kariakoo, Mohamed Ramadhan anasema hakuna tofauti tangu treni ilipoanza safari zake kutoka Pugu hadi Kurasini.
“Saa 12 asubuhi ikibeba watu kuna wengine wanaoenda sehemu ambazo haipiti kwa hiyo tunawachukua sisi,” anasema Ramadhan.
“Kwa sababu inapita sehemu za ndani ambapo sisi hatupiti inachukua abiria wa huko,” anaongeza Ramadhani.
Katika mwaka mmoja imesaidia mengi, mmoja wa abiria wa usafiri huo wa Mwakyembe, Athuman Mrisho anataka idadi ya mabehewa iongezwe kutoka 8 ya sasa hadi 12.
Mrisho anataka ifanye kazi pia siku ya jumapili ambapo anapendekeza angalau mabehewa matatu yatumike kwa siku hiyo.
Waziri Mwakyembe wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni alisema abiria 14,000 wanaosafiri kwa treni kwa siku, wangehitaji mabasi zaidi ya 467 yenye uwezo wa kuchukua abiria 30 kila moja.
Moja ya mahitaji yanayosubiriwa na usafiri huo ni pale itakapoanzisha usafiri wa kwenda Gongo la Mboto ambapo shida ya usafiri inazidi kuongezeka kila siku.
Huduma hiyo ya treni ilizinduliwa na kuanza kazi rasmi Oktoba 29 mwaka jana, huku wengi wa wananchi wakiwa na matumaini kuwa ingesaidia kupambana na tatizo la usafiri linalonekana kusumbua katika Jiji la Dar es Salaam.
Wananchi wengi waliongea na mwandishi wa makala hii wameshauri Serikali kuangalia namna ya kuiboresha huduma hii ambayo inaonekana wazi kwamba ikiboreshwa inaweza kufanya usafiri kuwa wa uhakika zaidi ya ilivyo sasa.
Aidha wameishauri Serikali kuangalia namna ya kutoa huduma za usafiri wa treni wa ndani ya mikoa na mikoa jirani kwa kadri inavyowezekana ili kuharakisha maendeleo nchini.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment