Sunday, 13 October 2013

Harambee kusomesha wakunga yakusanya mil.700/-


Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, ameongoza harambee kusaidia kusomesha wakunga kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini ambapo zaidi ya Sh. milioni 700 zimekusanywa.
Fedha hizo zilikusanywa juzi usiku katika Chakula cha Hisani kwa ajili ya kampeni inayujulikana kwa jina la ‘Stand up for Tanzania Mothers Campaign’ ambapo fedha hizo zitasomesha wakunga 3,800 wa nchini.
Shirika la Tafiti na Dawa Afrika (AMREF) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikwamo ITV na The Guardian Limited, walifanikiwa kukusanya Sh 719,320,000 katika harambee hiyo.
Akizungumza katika halfa hiyo, Bilal ambaye alikuwa ni mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dk. Jakaya Kikwete, alisema kukosekana kwa wataalamu wa kutosha hasa katika maeneo ya vijijini kunachangia kutokea kwa vifo hivyo.
“Kukosekana kwa wakunga wenye utaalamu ni moja ya sababu inayochangia vifo hivyo kwani Tanzania ina upungufu wa wakunga, hivyo tunatakiwa kuongeza idadi ya wataalamu hao,” alisema Dk. Bilal.

Alisema jitihada za pekee zinahitajika kupunguza vifo vya mama na mtoto ikiwa imebaki miaka miwili kufikia malengo ya milenia ya kupunguza vifo hivyo.
Alisema kuna upungufu wa wakunga kwa asilimia 40, hivyo kusomeshwa kwa wataalamu hao kutasaidia kupunguza tatizo hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alisema vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa asilimia 47 tangu kufikia mwaka 2010 kutoka vifo 870 mwaka 1990 hadi 454 katika kila vizazi hai 10,000.
Alisema mikakati iliyopo ni kuvipunguza vifo hivyo hadi kufikia idadi ya 193 katika kila laki moja jambo ambalo wanaamini watalifikia.
Naye mke wa Rais Kikwete, Mama Salma aliwataka Watanzania kuchangia kampeni hiyo kwa kila mmoja kutoa hata Sh 100 ili kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza maisha kwa kuleta uhai au mtoto anayekosa uhai.
Alisema kila mmoja ana wajibu wa kujitolea ili kuokoa vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi.
Mkurugenzi wa AMREF Tanzania, Dk. Festus Ilako alisema wanashirikiana na serikali ya Tanzania katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Milenia ya kuboresha huduma za afya hasa kwa kinamama na watoto.
Alisema ili kufikia malengo hayo, wakunga wa kutosha wanahitajika kuimarisha masuala ya uzazi salama ili kufanikisha malengo ya millennia.
Miongoni mwa waliochangia katika kampeni hiyo ni pamoja na Benki M Sh. milioni 125, Benki ya NMB Sh.milioni 25, Benki ya CRDB Sh. milioni 20, Makamu wa Rais Sh. milioni tano pamoja na Taasisi ya Wama Sh. milioni 2.5 na wengineo wakiwamo NSSF mil 2/-
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...