Rais wa Bunge la Switzerland,Maya Graf,akifurahia zawadi aliyopewa na mwenyeji wake,Spika wa Bunge la Tanzania,Anne Makinda,mara baada ya mazungumzo yao ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Wakistaafu wana hali mbaya
Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema mishahara ya wabunge wa Tanzania siyo mikubwa kulinganisha na wanayolipwa wabunge wa mabunge mengine duniani.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka ufafanuzi kuhusu kauli yake juu ya mpango wa Bunge wa kuwaokoa wabunge dhidi ya hali mbaya ya maisha, ambayo huwakabili wanapokuwa wamestaafu ubunge.
Kauli kuhusu mpango wa Bunge kuwaokoa wabunge wastaafu dhidi ya hali mbaya ya maisha, ambayo huwakabili, ilitolewa na Spika Makinda, wakati wa mazungumzo kati yake na Spika wa Bunge la Uswisi,Maya Graf, aliyetembelea ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana.
Katika ufafanuzi wake, Spika Makinda aliitaja mishahara wanayolipwa wabunge katika orodha ya sababu zinazochangia hali mbaya ya maisha kuwakabili wabunge wanapostaafu ubunge.
Sababu mojawapo aliitaja kuwa ni mabadiliko ya malipo kwa wabunge baada ya kumaliza kipindi chao cha ubunge au kustaafu kazi hiyo, yaliyofanywa katika kipindi cha Bunge lililoshirikisha vyama vingi vya siasa nchini, kuanzia mwaka 1995.
Alisema katika kipindi chote cha Bunge lililokuwa na wabunge kutoka chama kimoja cha siasa (CCM), kulikuwa na utaratibu wa kuwalipa pensheni wabunge wanaostaafu ubunge.
Lakini alisema utaratibu huo uliondolewa baadaye baada ya Bunge la vyama vingi vya siasa kuanza mwaka 1995.
Alisema baada ya Bunge hilo kuanza, uliwekwa utaratibu mpya, ambao wabunge wanaomaliza kipindi chao cha ubunge au kustaafu kazi hiyo hulipwa kiinua mgongo au bahashishi (gratuity).
Alitaja sababu nyingine inayochangia wabunge wastaafu kukabiliwa na hali mbaya ya maisha kuwa ni mishahara midogo wanayolipwa wakati wakiwa kazini.
Alisema licha ya mishahara ya wabunge kutokuwa mikubwa kulinganisha na ile wanayolipwa wabunge wa mabunge mengine duniani, pia hutakiwa katika kile kidogo wanacholipwa wachangie majimboni.
“Mishahara yetu siyo mikubwa kama wenzetu, pia (mbunge) unatakiwa uchangie jimboni,” alisema Spika Makinda.
Wakati Spika Makinda akisema hayo, mbunge mmoja hulipwa mshahara wa Sh. milioni 11 kwa mwezi.
Hiyo ni mbali na posho ya Sh. 330,000 anayolipwa mbunge kwa kuhudhuria kikao kimoja kwa siku. Posho ni Sh. 80,000 za kujikimu akiwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao Sh. 200,000 kwa siku na mafuta ya gari Sh. 50,000, jumla kuwa Sh. 330,000 kwa siku.
Aidha, mbunge mmoja hulipwa ‘gratuity’ (kiinua mgongo au bahashishi) ya Sh. milioni 72 baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano cha ubunge.
Posho ya Sh. 330,000 anayolipwa mbunge kwa siku inazidi kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa serikali wa Sh. 150,000 kwa mwezi.
Aidha, wabunge hupewa fedha za Mfuko wa Jimbo Sh. milioni 30 kila mwaka kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo katika majimbo yao.
Serikali hadi sasa imeshindwa kuongeza kima cha chini kufikia Sh. 350,000 ambacho kilipendekezwa na Shirikisho Huru la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), hali ambayo imekuwa ikisababisha mivutano ya mara kwa mara kati yake na vyama vya wafanyakazi.
Kuhusu kuwaokoa wabunge dhidi ya hali mbaya ya maisha wanapostaafu, Spika Makinda alitangaza mpango maalumu wa Bunge wa kuwaokoa dhidi ya hali hiyo.
Alitangaza mpango huo wakati na baada ya mazungumzo kati yake na Spika wa Bunge la Uswisi, Graf jana na kusema Bunge lina mpango wa kuanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wabunge.
Alisema lengo la mafunzo hiyo, ambayo yataanza wakati wowote ni kuwajengea uwezo wabunge ili watakapostaafu au vipindi vyao vya ubunge vitakapofikia ukomo wasitetereke kimaisha.
Makinda alisema mafunzo hayo yatatolewa wakati wowote na kwamba, programu hiyo itakuwa ya hiari kwa wabunge, hasa wenye kujishughulisha na biashara na shughuli nyinginezo.
Alisema ni vigumu kwa mbunge kuona hali mbaya ya maisha, ambayo huwakabili baadhi ya wabunge wanapokuwa wamestaafu ubunge.
Lakini alisema hali hiyo ameishuhudia mwenyewe baada ya kuchaguliwa kuwa Spika.
“Ukiona waliostaafu ubunge, wana hali mbaya sana, wengine wamekufa,” alisema Spika Makinda.
Alisema baada ya kukalia kiti cha Spika, baadhi ya wabunge wastaafu wamekuwa wakienda ofisini kwake (Spika) ‘kumlilia’ hali mbaya ya maisha na kuomba awasaidie.
Makinda alisema ofisi ya Spika haina bajeti, hivyo amekuwa akilazimika kutumia fedha kutoka mfukoni mwake kuwasaidia wastaafu hao wanaokwenda ofisini kwake ‘kumlilia’ shida za kimaisha.
Alisema kuna siku waliwahi kwenda ofisini kwake wabunge watano wastaafu kumlilia shida.
Lakini alisema kwa bahati mbaya siku hiyo aliweza kuwasaidia baadhi tu.
Alisema hali hiyo iliwafanya wale waliokosa msaada wake siku hiyo kuondoka, huku wakinung’unika.
Makinda alisema Bunge limefikiria kutoa mafunzo hayo kwa wabunge kwa sababu mbalimbali.
Mojawapo ni wabunge wengi wa sasa kuwa vijana na wengine wameingia bungeni wakiwa wametokea shuleni, hivyo wanaweza wasichaguliwe tena ubunge na hivyo, kukabiliwa na hali mbaya ya maisha.
“Ukishakuwa mbunge kazini huendi. Ndiyo maana tukafikiria kufundisha, hasa wabunge wenye biashara na shughuli nyinginezo,” alisema Spika Makinda na kuongeza:
“Tunataka mbunge awe na kazi, aingie bungeni. Ni nidhamu tunataka tuirudishe. Tunataka ifike mahali siasa isiwe ni kazi.”
Alisema athari ya kufanya siasa kuwa ni kazi, ni chaguzi kugeuzwa kuwa ni msimu wa watu kugombana.
“Ndiyo maana chaguzi zetu zimekuwa kama ugomvi, zinakuwa ni kufa na kupona. Tunataka isiwe nongwa,” alisema Makinda.
Naye Graf aliyekuja nchini kwa ziara binafsi, ikiwa ni pamoja na kutembelea miradi inayofadhiliwa na nchi yake, katika mikoa ya Morogoro na Dodoma, aliunga mkono hoja ya Spika Makinda kuhusu mafunzo kutolewa kwa wabunge kwa kuwa hakuna uhakika kwa mbunge kuchaguliwa tena kushika nafasi hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment