Thursday 24 October 2013

Uswisi sasa kurejesha mabilioni ya mafisadi


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (katikati) akiwa na maafisa wa Serikali ya Uswiss pamoja na timu uchunguzi kufuatilia mabilioni ya fedha zilizowekwa katika benki za nchi hiyo. Picha na Bernhard Reinhold 

Dar es Salaam. Sakata la vigogo kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi, limechukua sura mpya baada ya Serikali ya nchi hiyo kutunga sheria inayowabana walioweka fedha kwenye benki zake kuzithibitisha, la sivyo zitarejeshwa katika nchi husika.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alifanya mazungumzo na Serikali ya nchi hiyo ambayo imemweleza kuwa imebadili sheria zake ili kuwadhibiti wageni wanaoficha fedha nchini humo.
Akizungumza na gazeti hili, Zitto alisema amepata taarifa hizo juzi baada ya kukutana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo ambaye alimwandalia mazungumzo na watalaamu wake.
Alibainisha kuwa tangu kuibuka kwa sakata hilo mwaka 2012 na Bunge kuiagiza Serikali kufuatilia, Serikali haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi kuhusu Watanzania waliohifadhi fedha nchini humo.

“Jana nilikutana na Waziri wa Fedha na akatuacha na mazungumzo na wataalamu wake. Wamesema hadi sasa, Tanzania haijasaini mkataba wa kubadilishana taarifa za kikodi (Multilateral convention on administrative assistance in tax matters),” alisema Zitto na kuongeza;
“Kwa kutosaini, Tanzania inajinyima haki ya kupata taarifa hizi na kutoza kodi kwa watu walioficha fedha huku (Uswisi), maana Sheria ya Kodi ya Tanzania inataka kila Mtanzania popote anapopata kipato halali lazima alipe kodi.”
Zitto alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya Uswisi kubadili sheria zake, kinaiwezesha nchi hiyo kutoa taarifa za benki za watu walioweka fedha nchini humo wakiwamo Watanzania, ambao sasa watatakiwa kuthibitisha kama fedha hizo ni safi au la.
“Kiufupi, Tanzania haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi. Ila Uswisi wamebadili sheria yao na sasa mmiliki wa fedha ndiyo anapaswa kuthibitisha kwamba ni safi, na ikithibitika kuwa hazina mwenyewe wala maelezo, zitarudishwa nchi husika,” alisema.
Zitto alisema mbali na kukutana na watendaji hao wa Serikali amezungumza na Umoja wa Mabenki wa nchi hiyo uliobainisha kuwa Uswisi ina Watanzania wachache wenye fedha.
“Wamesema Watanzania wengi wana fedha Uingereza, Jersey, Cayman Islands na Mauritius. Dubai pia imetajwa sana,” alisema Zitto. Zitto alielezea kuwa umoja huo wa benki za Uswisi umeanzisha mkakati wa kusafisha fedha uitwao ‘clean money strategy’, na wamegundua watu wengi ambao ni wanasiasa, wamezuia akaunti zao na kupeleka majina kwenye Serikali zao.
“Tanzania haijafanya maombi rasmi hapa Uswisi na hivyo wao kama benki hawawezi tu kutoa taarifa bila kuombwa. Sheria yao imerekebishwa ambapo sasa ni wajibu wa mwenye akaunti kusema kama fedha zake ni halali au hapana,” alisema Zitto na kuongeza.
Hivi sasa hawapokei pesa kutoka nchi za Afrika au wanapokea kwa tahadhari sana, maana kuna reputational risk (kupoteza heshima),” alisema.
Wito wa timu ya uchunguzi
Zitto alipendekeza timu iliyoundwa kuchunguza fedha hizo itoe taarifa yake kwenye Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba 29, mwaka huu, akieleza kuwa, “Kuendelea kukaa na taarifa, kutaongeza tetesi za kweli au za uwongo.”
Alisema mpango huo wa kusaka fedha zilizofichwa nchini Uswisi, umelenga zile zilizofichwa na watu binafsi kutokana na rushwa au kuuza dawa za kulevya na kampuni kubwa za kimataifa.
Alibainisha kuwa wengi waliotambulika ni wanasiasa, vigogo wa jeshi na wakuu wa mashirika ya umma na watendaji wa Serikali.
“Katika mabenki ya Uswisi, kuna kiasi cha Dola za Marekani 197 milioni. Fedha nyingi zipo katika benki za Uingereza na visiwa vyake, Dubai na Mauritius,” alisema na kuongeza;
“Wapo watu waliopata fedha kihalali, lakini wanaficha fedha hizo na mali zao nje ili kukwepa kodi. Wengi wa hao ni wafanyabiashara wakubwa nchini. Tanzania inapoteza Dola za Marekani 1.25 bilioni kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hizi.”
Alibainisha kuwa Tanzania lazima itunge sheria ya kufilisi mali ambazo mtu anashindwa kuthibitisha amezipataje.
“Tayari ninafanyia kazi muswada binafsi wa sheria wa kubadilisha sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 1991. Wasaidizi wangu wanafanyia kazi muswada huo ili usomwe kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa Bunge unaonza Oktoba 29 na kueleza kuwa sheria ya sasa ina upungufu,” alisema.
Madai hayo ya Zitto yamekuja ikiwa umepita mwaka mmoja tangu Bunge kuipa Serikali muda wa kuchunguza sakata la vigogo walioficha mabilioni katika benki za Uswisi.
Zitto ndiye aliibua sakata hilo mwishoni mwa mwaka 2012. Kufuatia hoja hiyo, Serikali iliunda timu kutokana na Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Werema ahoji Mwananchi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...