Tuesday 29 October 2013

VIFO VYAONGEZEKA VURUGU ZA KILINDI



Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa

Idadi ya watu waliokufa katika mapigano yaliyoibuka wiki iliyopita baina ya askari Polisi na kikundi cha watu wasiojulikana katika Kijiji cha Lulago wilayani Kilindi, mkoani Tanga wamefikia watatu huku msako mkali dhidi ya watuhumiwa hao ukiendelea.

Katika tukio hilo, askari  Mgambo wa Kijiji cha Lwande, Salum Mgonje, aliuawa kwa kupigwa mapanga huku Mkuu wa Kituo cha Polisi wilaya ya Kilindi, Inspekta Lusekalo Edward, akijeruhiwa kwa risasi.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Kilindi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, alimtaja mtu mwingine aliyeuawa kuwa ni Hamisi Ramadhan mkazi wa Kijiji cha Negero na kwamba marehemu mwingine hakutambulika.

Gallawa alisema watu 44 wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu hizo baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga na Jeshi la Polisi kuweka kambi kwa zaidi ya siku tano kwenye eneo hilo.




Gallawa alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa watu hao aliowaita kuwa ni ‘waasi’ waliweka kambi katika vijiji vya Lulago na Kimamba kwenye kata za Lwande na Negero na kuweka makazi ambayo wanayatumia kutoa mafunzo yakiwamo ya kupigana, kuua na kuharibu uchumi.

Alisema kikundi hicho kimekuwa kikiwanyanyasa wananchi kwenye vijiji huku wakisema kuwa hawaitambui serikali iliyopo madarakani.

“Hawa watu wamefanya mambo mengi ikiwamo kutoa mafunzo kwenye shule yao ya kupigana, kuua na kuharibu uchumi. Shule hiyo ni kuanzia shule ya awali na msingi, sasa tunaendelea na uchunguzi ili kubaini undani wa mambo haya,” alisema Gallawa.

Alisema zaidi ya wanawake 16 wakiwa na watoto walikimbia katika makazi yao na kwamba wamekataliwa kurejea kwenye vijiji vyao.

“Hawa wanawake inaonekana baadhi waliolewa na hawa waasi hali iliyosababisha kutengwa na jamii zao, hata wazazi wamekataa watoto wao wasirudi nyumbani kwa kuhofia usalama wao.

Bado wapo pale Songe katika  Kitongoji cha Madina chenye wakazi zaidi ya 100 na wakati wa mapigano walijifungia kwenye msikiti na ndiyo waliokuwa wakitumia kujificha na kujibazana risasi na Polisi,” alisema Gallawa. 

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, alisema watu hao walikamatwa wakiwa na silaha mbalimbali zikiwamo za moto.

Alizitaja kuwa ni bastola mbili, Shortgun moja, magobole matatu, mapanga 18, shoka mbili, visu 10, baruti pamoja na nguo zinazoaminika kuwa ni za kijeshi.

Massawe alisema kikosi maalum kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na idara mbalimbali za ulinzi na usalama wanaendelea na kuwatia nguvuni wahalifu hao.

Oktoba 23, mwaka huu kikundi cha watu wasiojulikana  kilifanya vurugu kupinga kitendo cha mwenzao kulipishwa ushuru wa ununuzi wa zao la iliki wa serikali ya kijiji na kusababisha mauaji ya mgambo na kumjeruhi kwa risasi mkuu wa kituo cha polisi mbaye aliongoza askari waliokwenda kuwakamata waliohusika kumuua mgambo huyo kwa kutumia bunduki.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...