PICHA NA GPL
WATU saba wamekufa papo hapo na wengine watano kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao baada ya gari aina ya Noah walilokuwa wakisafiria kutoka Gairo kwenda Morogoro kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania.
Scania hiyo yenye namba za usajili T 129 AGB, ilikuwa ikitokea Morogoro kwenda Dodoma, iligongana na Noah hiyo yenye namba T 502 AUP, katika eneo la Dakawa Ranchi, wilayani Mvomero.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, aliwataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa Noah, Masoud Omary (28) wa Kihonda, Morogoro mjini, Isack Mehele (25) mfanyakazi wa kiwanda cha tumbaku Morogoro (ALLIANCE ONE), Sam Elisha (40), Daktari wa mimea, Maugo Salum (30), Sophia Hassan (20) na Adini Mwisholwa (70), wote wakazi wa Gairo na mwanamume mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.
Shilogile alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11:45 na chanzo chake kilitokana na dereva wa Noah kujaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake na kukutana uso kwa uso na Scania hiyo.
Waliojeruhiwa ni Juma Mohamed (21), Hashim Ally Dafa (42), Junior Msenga, Selemani Hamis (20), Martin Msobi, Festo Paulo na mwingine ambaye jina lake halikutambuliwa mara moja.
Daktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Francis Semwene, alisema majeruhi wawili hali zao ni mbaya na wengine wameumia zaidi maeneo ya kichwani, mikononi na maeneo ya ndani na wanapata huduma za awali.
Akizungumzia ajali hiyo mbali na kuwataka madereva kuzingatia taratibu na sheria za usalama barabarani, Mwenyekiti wa Kijiji cha Wami Sokoine, Marco Ndesse, alisema eneo hilo limekuwa maarufu kwa ajali kutokana na madereva kupuuza sheria.
Aliiomba serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti ajali hizo ikiwamo kuweka matuta na kuongeza doria za polisi wa usalama barabarani.
CHANZO: Tanzania daima
No comments:
Post a Comment