Saturday 23 November 2013

ASIMULIA BABA YAO MZAZI ANAVYOWABAKA (Sehemu ya 2)


Badala ya baba kuonekana kuwa ndio mstari wa mbele kuwasisitiza watoto kufanya mazuri, amekuwa akituhumiwa kuwa ndio kinara wa kuwalawiti na kuwabaka watoto wake mwenyewe, kiasi cha kusababisha mke kukimbia nyumba. 

Anasema baada ya yeye kuanza tena unyama dhidi ya watoto wake  walipeleka taarifa kwa kiongozi mmoja wa kanisa ambaye aliitisha kikao na viongozi wa vijiji na ukoo wao kuzungumzia jambo hilo ambapo mwanaume huyo alikiri na kuapa kutorudia tena.
Mwenyekiti wa kijiji
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiria, Doroth Mtui, anasema baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani wa watoto hao, alilazimika kufika nyumbani kwa mtuhumiwa kuzungumza na mtoto huyo ambae alimweleza ukatili anaofanyiwa na baba yake, na ndipo alipopiga “ yowe” kuita wananchi wengine ambao waliandamana kwa pamoja kumkamata mwanaume huyo,na kumpeleka  Kituo cha Polisi Himo.


Baada ya kufika kituo cha polisi Himo, walitakiwa kumpeleka mtoto huyo hospitalini, ili kuthibitisha kama  kweli amebakwa, taarifa iliyotolewa na daktari wa Hospitali Teule ya Kilema, ilionyesha kuwa mtoto huyo ameingiliwa sehemu zote mbili, na kwamba ni kitendo cha muda mrefu kilichosababisha kuota nyama sehemu zake za siri.
Uongozi wa kanisa analosali
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Rauya, Mchungaji Anayesu Ringo alikokuwa anasali mwanamme huyo alikiri kufanya kikao na familia ya mtuhumiwa na kukiri kuishi na wanawe, aliomba kusamehewa na kanisa kushauri watoto hao kwenda kuishi na bibi yao na sio kulala nyumba moja na baba yao.
Mchungaji Ringo anasema anashangaa kusikia bibi aliwarudisha wajukuu zake, kwenye mateso hayo, na kusema jamii inapaswa kutambua kuwa jukumu la kuwatunza watoto  ni la jamii nzima, familia inapaswa kutambua kuwa malezi bora yanaanzia ngazi ya familia.
Wanaukoo wanasemaje?
Mmoja wa wanaukoo (jina tunalo), anasema  wao kama wanaukoo walishakaa na kumuonya ndugu yao lakini ni mkorofi na hamsikilizi mtu na kwamba ukorofi wake  ulisababisha kila mtu kumwacha aishi anavyotaka.
“Huyu ndugu yangu ameonywa sana lakini hasikii wanawake waliungana hapa na wakamchapa viboko ,mchungaji alimwita ofisini tukajadili jambo hili na kukiri kuacha  na sisi tuliamini ameacha, kumbe anaendelea na tabia hii ya uhayawani,” anasema.
Taarifa ya daktari
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dk  S. Berna wa Hospitali Teule ya Kilema mashavu ya sehemu za siri (labia) yana maambukizi na kwamba ana kidonda.
Ripoti pia inaonyesha kuwa licha ya umri wake kuwa mdogo, mtoto huyo si bikira,  jambo ambalo kwa umri huo sio rahisi mtoto kuwa hivyo .
Taarifa hiyo pia inaonyesha sehemu za siri za mtoto huyo zinatoa  majimaji yasiyo ya kawaida yanayoashiria maambukizi sehemu za uzazi huku njia ya kutolea  haja kubwa ikiwa imeathiriwa  vibaya kutokana na misuli yake kulegea.
Mtaalamu  wa watoto anasemaje
Mtaalamu wa masuala ya watoto kutoka Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, Saganda Kapalala anasema mtoto anapofanyiwa ukatili, hupata madhara mbalimbali ambayo huweza kuathiri maisha yake yote.
Saganda anasema madhara apatayo mtoto aliyebakwa ni pamoja na kuathirika kisaikolojia na kuwaona wanaume kuwa watu katili na hata baadaye anaweza asiolewe tena kutokana na kukosa  imani na wanaume.
Maoni ya Wanaharakati
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Valery Msoka akizungumza na mwandishi wa makala haya anasema ni jambo la kusikitisha kuona mtoto anafanyiwa ukatili wa kinyama namna hii lakini ukafumbiwa macho kwa muda mrefu.

Naye Elizabeth  Minde ambae ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na Utetezi wa Haki za Binadamu Jinsia na Watoto (kwieco)  amelaani kitendo hicho na kusema kamwe hawatalala hadi haki itendeke.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert  Boaz alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba wameshamkamata mtuhumiwa,  atafikishwa mahakamani wakati wowote uchunguzi utakapokamilika.
Kamanda Boaz anasema jambo hili limemsikitisha sana kutokana na ukweli kwamba mzazi ndiye alipaswa kuwa mlinzi wa familia, sivyo kama ambavyo sasa anatuhumiwa kwamba amekuwa akiwaharibu watoto wake.
“Huyu mtu tuko naye, tumemkamata, bila shaka sheria itachukua mkondo wake, lakini kwa kweli ni jambo linalosikitisha,” anasema Kamanda Boaz.
MWISHO
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...