Saturday 23 November 2013

Wafanyakazi Swissport wadakwa na simu za wizi

Swissport

Wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Wakala wa Mizigo Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam (Swissport ), wanashikiliwa na Polisi wa Viwanja vya Ndege kwa kukutwa na simu zinazodaiwa kuibwa kutoka kwa mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo, imekuja siku chache baada ya baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo kupitia Katibu wa Jumuiya yao, Sued Chemchem, kulalamikia kuibiwa mizigo yao mara kwa mara bila wahusika kuchukuliwa hatua stahiki katika uwanja huo.

Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Renatus Chalya, alithibitisha kukamatwa kwa wafanyakazi hao wawili wakiwa na jumla ya simu 32 mali ya Sued Chemchem.

Kamanda Chalya aliwataja wafanyakazi hao kuwa ni Daudi Mwenga (49), na Jackson Kituka (30), wote wakiwa ni madereva wa kampuni ya Swissport na uchunguzi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Chalya alisema, Novemba 11, mwaka huu majira ya saa 7 mchana baada ya ndege ya Qatar Airways kutua ikitokea China, polisi iliweka mtego kuwafuatilia nyendo za wafanyakazi hao. 

Baada ya muda mfupi, mtego wao ulifanikiwa na kuwakamata wafanyakazi hao na jumla ya simu 32 kwenye magari yao binafsi aina ya Nokia, Sharp na M-Horse zenye thamani ya Shilingi milioni saba.

Kamanda Chalya alisema jeshi la Polisi katika viwanja vya ndege nchini limejipanga kuhakikisha mali za wasafiri zinafika salama zinakotoka ili kutokomeza tabia ya wizi inayofanywa na wafanyakazi wasio waaminifu.

Awali akizungumza na waandishi wa habari, Chemchem ambaye simu zake zimekamatwa, alisema alikuwa amenunua mzigo wa simu 180 zenye thamani ya Sh. milioni 24.
Alisema mwaka jana, jumla ya wafanyabiashara sita waliibiwa maboksi ya simu yenye thamani ya Sh. milioni 240 huku wahusika wakiwa wanatamba bila kuchukuliwa hatua. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...