Thursday, 21 November 2013

Mapya yaibuka mauaji ya kutisha Dar

Askari Polisi akichunguza ndani ya gari ambayo ilikuwa imebeba watu waliopigwa Risasi na aliekuwa mfanyabiashara wa magari mkoani Mwanza,ambaye naye alijimaliza kwa risasi.

Familia ya mama na mabinti zake wawili pamoja na shemeji yao walioshambuliwa kwa risasi na wawili kati yao kuuawa na wengine kujeruhiwa, imesema waliokumbwa na masaibu hayo hawahusiki kwa kuwa uhusiano wa kimapenzi kati ya muuaji, Gabriel Munishi (30-35) na ndugu yao, ulikufa tangu mwaka jana.

Aliyeuawa katika tukio hilo linalodaiwa kuwa lilitokana na wivu wa kusalitiana kimapenzi, ni mfanyakazi wa Benki ya Barclays, jijini Dar es Salaam, Alfa Alfred (34) na shemeji yao, Francis Mshumila (41), ambaye ni raia wa Kenya.

Waliojeruhiwa ni Christina  Alfred (35), ambaye ni dada wa marehemu Alfa na Hellen Eliezer (60-63), ambaye ni mama yao mzazi, ambao walikumbana na mkasa huo kabla ya muuaji naye, ambaye ni mfanyabiashara wa magari mkoani Mwanza, kujimaliza kwa risasi.

Tukio hilo lililotokea saa 1:30 asubuhi juzi, wakati mama na mabinti zake pamoja na Francis, wakitoka nyumbani, eneo la Bungoni, Ilala, jijini Dar es Salaam, kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kumsindikiza Christina
 aliyekuwa akisafiri kurudi masomoni katika kisiwa cha Cyprus.

Kaka wa mabinti hao, Nando Newa, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wamekuwa wakishangazwa na madai kwamba, muuaji alifanya unyama huo kutokana na wivu uliotokana na kusalitiwa na ndugu yao kimapenzi.

“Wanaposema amesalitiwa kimapenzi hatuelewi maana yake nini. Kwa sababu kwanza alikuwa hajaoa kwetu, hivyo dada (Christina), hakuwa mke wake, na pili uhusiano wao wa kimapenzi ulikufa tangu mwaka jana,” alisema Newa, ambaye anajulikana pia kwa jina la Lois.

Newa alisema mara ya mwisho aliyoonana na muuaji ilikuwa Juni, mwaka huu, wakati huo Christina akiendelea na masomo katika kisiwa hicho, ambako anachukua Shahada ya Uzamivu ya masuala ya mawasiliano ya simu.

Alisema katika kipindi cha likizo, Christina alikuwa akirudi nchini na kufikia nyumbani kwao, Ilala kwa kuwa bado hajajaliwa kujenga nyumba yake.

Hivyo, akasema haikuwa vigumu kwa muuaji kuifahamu nyumba hiyo na kwenda kutekeleza alilokusudia kwa kuwa siyo mahali palipojificha.

Alisema gari aina ya Toyota Hilux Surf walilolitumia kwa ajili ya kwenda JNIA, lilikuwa likimilikiwa na marehemu Alfa na kwamba, marehemu Francis aliyekuwa akiliendesha, alikuwa shemeji yao, ambaye ameoa kwao. 

MAZISHI YA NDUGU YAO
Kuhusu mazishi ya ndugu yao, Alfa, Newa hakutaja siku rasmi, ingawa alisema yanaweza kufanyika kesho.

Hata hivyo, alisema ni lazima kwanza wapate kibali cha polisi na pia mama yao mzazi, Hellen aruhusiwe kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako anaendelea kupatiwa matibabu.

IDADI YA WALIOUAWA YAONGEZEKA
Katika hatua nyingine, mmoja kati ya majeruhi watatu wa tukio hilo aliyekuwa amelazwa kwenye Taasisi ya Mifupa na Fahamu (MOI), Francis, amefariki dunia.

Meneja wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Mahusiano cha MOI, Jumaa Almasi, alithibitisha kufariki dunia kwa Francis.

Alisema Francis, ambaye alifikishwa MOI juzi asubuhi baada ya kujeruhiwa kwa risasi katika tukio hilo, alifariki dunia jana saa 12:45 asubuhi.

Jumaa alisema Francis alikuwa na majeraha makubwa ya risasi kwenye mkono wake wa kulia na tumboni.

Alisema maiti yake imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha MNH.

Wakati huo huo, hali ya majeruhi mwingine wa tukio hilo, Hellen,  ambaye alilazwa MNH, inaendelea kuimarika.

Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminieli Eligaesha, aliliambia NIPASHE jana kuwa hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri na anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

AMANA WAKATAA KUTO A USHIRIKIANO
Hata hivyo, wakati MNH wakieleza hayo, wenzao wa Hospitali ya Amana jana walikataa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari waliotaka kujua kuhusu miili ya marehemu waliohifadhiwa hospitalini hapo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...