Saturday 30 November 2013

Shahidi aeleza Twiga walivyokuwa wanakamatwa

Mnyama Twiga akiwa katika Bunga ya wanyama
Shahidi katika kesi ya kusafirisha wanyama hai na ndege kwenda Qatar, Indonesia,  Maulid Hamis, ameieleza mahakama kuwa twiga watatu walikufa wakiwa chini ya uangalizi wa mwajiri wake ambaye ni mshitakiwa namba moja, Kamran Mohamed.

Akitoa ushahidi wake mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Simon Kobelo.

Alidai kuwa kwa kipindi hicho yeye alikuwa ni mfanyakazi katika kampuni ya ukamataji wanyama inayomilikiwa na mshitakiwa wa kwanza na alikuwa akikamata wanyama hao na kuwahifadhi katika zizi la wanyama.


Alidai mahakamani hapo kuwa kuanzia mwaka 2009 kazi yake ya kwanza aliyoifanya akiwa na Kamran ni ya kwenda kukamata twiga na walifanikiwa kukamata twiga wanne waliokuwa wakiwawinda kwa kuwatega na kamba na kuwafunga katika maboksi na kuwapeleka katika zizi.

“Siku ya kwanza tukiwa na kibali pamoja na Kamrani, tulikamata twiga watatu na tulitumia siku mbili katika kuwakamata huku siku iliyofuata tukafanikiwa kumkamata twiga mmoja na kwa bahati mbaya alikufa twiga mmoja na baada ya siku kadhaa wa pili na watatu nao pia walikufa…

daktari alipompasua twiga mmoja alisema kuwa  wamekufa kwa sababu ya hofu…tuliendelea na kazi ya kukamata wanyama wengine wakiwamo tompson na grant gazer ambao nao walikuwa wakifa kwa wingi wakiwa zizini,” alidai mahakamani hapo.

Mbele ya Mwendesha mashitaka wa serikali, Evetha Mushi na Stela Majaliwa, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kila twiga alipokuwa akifa walikuwa wakiambiwa wachimbe shimo refu na kumfukia huku wakipewa amri ya kwenda kuwakamata wengine na kufanikiwa kukamata twiga watatu na kufikisha jumla ya twiga wanne ambao walisafirishwa Novemba 25, 2010.

Aidha ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mara baada ya wiki tatu walipewa amri nyingine na mshitakiwa wa kwanza ya kwenda kutafuta wanyama wengine na kuwarudisha zizini ambapo walifanikiwa kukamata nyati, tompson na twiga mmoja lakini hawakuweza kupata nyumbu na pofu.

Shahidi huyo pia alidai kuwa kutokana na twiga huyo kukimbia sana, alikufa mara tu baada ya kufikishwa zizini ambapo madaktari kutoka maliasili walisema amekufa kutokana na kukimbia kwa muda mrefu na kwamba walisafirishwa pofu watatu, nyumbu sita, tompson 32, grant 12 na twiga wanne.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kosa la kusafirisha wanyama hai na ndege kwenda nchini Doha kwa kutumia ndege aina ya C.17 yenye nambari AMA/MAB mali ya shirika la Qatar Airways ambapo waliwapitisha wanyama na ndege hao kwenye geti namba 5A na 5B katika kiwanja cha ndege cha KIA.

Washitakiwa hao ni Kamran Mohamed Raia wa Pakistani, Hawa Hassan, Martin Methew na Michael Disha, wote wapo nje kwa dhamana isipokuwa mshitakiwa wa kwanza. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 21,  mwakani
.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...