Saturday 30 November 2013

USHAHIDI WA UMILIKI WA ZIWA NYASA WATOLEWA


Watu wa viunga vinavyolizunguka Ziwa Nyasa /Ziwa Malawi wakiendelea na shughuli za uvuvi. Tafiti mbalimbali zimeonyesha wengi wao hawaelewi hasa chanzo cha mtafaruku huu wa mipaka ya Ziwa ulioibuka kati ya Tanzania na Malawi. PICHA | PLATOURS (KWA HISANI) 
Dar es Salaam. Malawi na Tanzania zimewasilisha ushahidi na majibu ya maswali kuhusu umiliki wa maeneo kwenye Ziwa Nyasa, kwa jopo la wasuluhishi linaloongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano.
Wasuluhishi hao walizitaka Malawi na Tanzania kutoa majibu ya maswali manne muhimu, wakati wakiwasilisha ushahidi wao kuhusu umiliki wa ziwa hilo wenye mgogoro.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania kutoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni, kutafuta mafuta katika eneo la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Malawi la  Nyasa Times, msemaji wa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Malawi, Quent Kalichero alithibitisha Jumatano wiki hii kwamba nchi hiyo imewasilisha majibu ya maswali hayo na ushahidi uliohitajika.

“Waziri wetu amewasilisha taarifa maalumu ya maandishi kwa wasuluhishi na kwa sasa yuko nchini Msumbiji, kwa ajili ya suala hilo,” alisema Kalichero juzi.
Makabidhiano hayo yalifanyika mjini Maputo, Msumbiji ikiwa ni siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mazungumzo na wasuluhishi, marais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano na wa Botswana, Festus Mogae jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mkutano huo wa Jumatatu mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe aliwaeleza wanahabari kwamba mazungumzo baina ya Rais Kikwete na wasuluhishi hao yalihusu zaidi ushahidi wa Tanzania katika suala la umiliki wa Ziwa Nyasa.
Pia alithibitisha kwamba Tanzania ilikuwa tayari  kuwasilisha ushahidi wake kwa sekretarieti ya ofisi ya waliokuwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) inayoongozwa na Chissano, Jumatano iliyopita.
Baada ya mkutano huo wa Jumatatu, Membe alieleza kwamba nchi zote husika, yaani Tanzania na Malawi zinatakiwa kuheshimu maagizo na kuwasilisha ushahidi huo kwa wakati, na kuwaachia wasuluhishi kazi ya kupitia na kutekeleza wajibu wao wakiwa wamepewa muda unaofikia mwaka mmoja kupata suluhu.
Wasuluhishi hao wa Sadc, Chissano na Mogae waliwasili jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mgogoro huo, kama walivyofanya kwa Malawi Julai mwaka huu.
Julai mwaka huu, Rais Joyce Banda wa Malawi alinukuliwa akisema kuwa nchi yake haina nia ya kulegeza kamba katika mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na Tanzania.
 Alitoa msimamo huo baada ya kukutana na Chissano wa Msumbiji na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambao ni wajumbe maalumu wa Jumuiya ya Sadc katika mgogoro huo.
Alisema kwamba madai ya Tanzania kuwa inamiliki sehemu ya Ziwa Nyasa, siyo ya kweli na kwamba mpaka uko ufukweni mwa ziwa hilo upande wa Tanzania.
Rais Banda alidai kuwa nchi yake inafuatilia kwa karibu upatanishi wa SADC na kwamba isiporidhishwa na uamuzi ya jumuiya hiyo italiwasilisha suala hilo Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).
Kabla ya hatua hiyo ya Malawi,  Aprili mwaka huu Serikali ya Tanzania iliitaka nchi hiyo kuacha kutapatapa na kuonya kuwa kamwe isithubutu kugusa eneo hilo la mpaka.
Akitoa kauli ya Serikali ya Tanzania Membe alisema: “Nadhani watasikia na kuelewa, Serikali ya Malawi iache kutapatapa, nchi zote ilikoenda kulalamika kuhusu mgogoro huu, Tanzania tumekuwa tukielezwa na hata hao wanaotueleza wanaishangaa sana Malawi.” Kauli hiyo ya Serikali ilifuatia Rais Banda kusema kuwa mgogoro huo sasa utapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kwa madai kwamba juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia zimeshindikana.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Malawi ni kinyume na makubaliano baina ya nchi hizo mbili yaliyofanyika Novemba 7 mwaka jana, jijini Dar es Salaam ambapo zilikubaliana kwamba jopo hilo ndiyo sehemu ya mwisho ya makubaliano.
Katika maelezo yake, Rais Banda alisema nchi yake imejitoa katika mazungumzo ya usuluhishi kwa madai ya kuhujumiwa na katibu wa jopo hilo ambaye ni Mtanzania, John Tesha kwa maelezo kuwa anavujisha taarifa muhimu za Malawi kwa Tanzania kabla ya Tanzania haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo. Alisema kuwa tangu kuibuka kwa mgogoro huo, Malawi imekwenda kulalamika katika nchi za Uingereza, Marekani, Umoja wa Afrika (AU) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).
Hata hivyo, baadaye Julai mwaka huu, Serikali ya Malawi ilitangaza kuwa itaendelea na mazungumzo na Tanzania kuhusu mpaka huku ikieleza kuwa viongozi wa Tanzania hawaelewi mipaka ndiyo maana wanapigania kuwa wao ni sehemu ya ziwa.
Waziri wa Habari wa Malawi, Moses Kunkuyu aliliambia Shirika la Utangazaji la Malawi (MBC) kuwa viongozi wote wa Tanzania wanadhani wanamiliki Ziwa Malawi (Nyasa) lakini watakuja kubaini baadaye kuwa hawana hata tone la umiliki.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...