Sunday 29 December 2013

Wazaramo: Kabila lenye sherehe lukuki, usipochangia, kushiriki unatengwa

watoto wakipongezwa na wazazi baada ya kutoka jandoni katika mkoa wa pwani. Picha ya Maktaba 

Tanzania ni nchi iliyojaliwa kuwa na makabila zaidi ya 120, yaliyounganishwa na lugha moja ya taifa ambayo ni Kiswahili. Miongoni mwa makabila hayo ya Tanzania, limo Kabila la Wazaramo, ambalo linapatikana katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Wazaramo wametapakaa katika Wilaya za Kisarawe, Bagamoyo, Kibaha, Mkuranga na Mafia.  Jijini Dar es Salaam, wengi wanaishi katika maeneo ya Buguruni, Magomeni, Ilala, Kariakoo na Msasani.
Wengi wa Wazaramo wanaabudu katika madhehebu ya dini za  Kiisalamu, Kikristo na madhehebu mengine  kwa uchache.
Mbali na swala la dini, katika masuala ya chakula na mavazi, wengi wao hupendelea kula wali, ugali wa muhogo, sembe kidogo, chapati na maandazi.
Upande wa mavazi, wanawake wa Kizaramo hupendelea kuvaa zaidi magauni marefu na mitandio (madira), khanga mbili kwa kufunga moja kiunoni nyingine kujitanda hasa kwa wasichana ambao tayari wameshavunja ungo(wamebalehe).
Kabila hili linasifika kwa kupenda sherehe, ambapo katika makala haya Mwananchi Jumamosi lilifanikiwa kuzungumza na Mwajabu Akide ambaye ni ajuza, mkazi wa  Kijiji cha Mengwa wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani  anayeelezea mtiririko wa sherehe za Kabila la Wazaramo. Mwajabu anaelezea pia utamaduni, mila, desturi, sherehe za Wazaramo na maana yake, tangu mtoto anapozaliwa hadi anapokuwa na familia yake, naye kupata watoto wake.
 Kwa mujibu wa Mwajabu, mtoto anapozaliwa katika familia ya Kizaramo, ndugu na jamaa wanapewa taarifa ambapo hutafutwa sheikh au mtu yeyote mwenye upeo katika dini ili kumfanyia adhana mtoto husika. Kitendo hiki hufanyika kama ishara ya kumkaribisha duniani na kumkumbusha wajibu wake kama binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu na anachotakiwa kufanya katika maisha yake.
Anasema kuwa baada ya hapo  mama na mtoto huendelea kukaa ndani kwa muda wa siku saba, kabla ya mtoto huyo kutolewa nje.
“Siku ya saba, mtoto huyo hutolewa nje huku kukiwa na ungo mdogo maarufu kwa jina la Kitunga na hapo mtoto anatolewa mara moja ili kuona upepo wa nje. Baada ya hapo hurudishwa ndani na mama yake mpaka siku  ya arobaini,” anasema Mwajabu.
Sherehe ya kwanza
Mwajabu anabainisha kuwa, ikifika siku ya arobaini kwa wale wenye uwezo, huitisha sherehe ya Maulid ili mtoto anyolewe nywele za utoto na hapo dua ya kumshukuru Mungu kwa kumfikisha hatua hiyo husomwa, huku wengine wakiitisha ‘rusha roho’ kwa ajili ya kusherehekea siku hiyo baada ya Maulidi (Maulidi ni neno la Kiarabu lenye maana ya kuzaliwa).
Anaongeza kuwa, baada ya arobaini, mtoto wa Kizaramo akifikisha umri wa miaka miwili kwa wenye uwezo huwafanyia ‘Hakika’ au wengine huandaa sherehe ya kuzaliwa (birthday).
“Katika sherehe hii ya hakika huchinjwa mbuzi na kupikwa pamoja vyakula vingine. Pia hufanyika dua maalumu ya kumwombea mtoto,” anasema Mwajabu.
Sherehe ya tatu
Mwajabu anafafanua kwamba, mtoto akifikisha umri wa miaka mitatu na kuendelea, ikiwa ni wa kike huachwa, lakini wa kiume hupelekwa kupewa sunna (kutahiriwa).
Anaongeza kuwa, katika tukio la kutahiriwa kunakuwa na sherehe ya mkusanyiko wa watoto wa rika moja, ambao hufanyiwa sunna wakiwa porini.
“Lakini ndugu, jamaa na marafiki nao hujumuika na watoto katika sherehe huko porini. Kunakuwepo na ngoma za kiasili mbalimbali kama Vanga , Tokomile na Mdundiko na hapo wazazi hutunza pesa, huku watu wakila, kunywa na kufurahi,” anasema mwanamke huyo.
Sherehe ya nne
Mwajabu anaendelea kusimulia akisema kuwa, baada ya sunna na sherehe ya tatu, katika sherehe ya nne watoto huenda jandoni ambapo hukaa huko wakipewa mafunzo kwa siku kadhaa na baada ya kupona huitishwa sherehe nyingine ya kuwatoa jandoni wali hao.
Anaeleza kuwa katika sherehe hiyo  kila mzazi huja na familia yake na kumchezea ngoma mtoto wao kwa kumtunza nguo, vitu mbalimbali na hapo watu hula na kunywa kwa furaha.
“Sherehe hiyo inamuimarisha mtoto wa kiume kujijua na kuwa na heshima kwa wazazi hasa mama na baba yake. Katika sherehe hiyo kunakuwepo na ngoma za kienyeji na rusha roho ili mradi watu wafurahi,” anasema na kuongeza:
“Ukiachilia mbali suala muda wa siku saba na kuelekezwa mila na desturi kwa kufundishwa namna ya kujiweka msafi na kuwa na heshima,” anasema.
Anafafanua kuwa katika sherehe hiyo ndogo, mtoto wa kike hununuliwa nguo na kupikwa chakula kidogo siku ya kutoka ambapo watu wakasherehekea na kumpa maneno machache yaliyo mwongozo wa kujiheshimu na kujilinda.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...