Thursday, 6 March 2014

Dk.Mengi atunukiwa tuzo ya kimataifa kwa kusaidia wasio na uwezo


Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi (kulia) na Gavana wa Klabu za Lions Kanda ya Tanzania na Uganda, Wilson Ndesanjo wakiwa na tuzo ya juu ya heshima iliyotolewa na klabu za kimataifa za Lions kwa Dk. Mengi. 

Mwenyekiti  Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi ametunukiwa tuzo ya juu ya kimataifa ya heshima kutokana na mchango wake anaoutoa kusaidia jamii hususani kwa watu wasiokuwa na uwezo.
Dk. Mengi alikabidhiwa tuzo hiyo juzi usiku jijini Dar es Salaam na Gavana wa Club ya Lion (Uganda na Tanzania), Willison Ndesanjo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo, Ndesanjo alisema Dk. Mengi ametoa mchango mkubwa kwa jamii, wakiwamo kwa vijana, wanawake na klabu za Lion na kwamba amekuwa na moyo huo kwa muda mrefu.

Tuzo hiyo ya kimataifa anapewa mtu ambaye ametoa mchango mkubwa kwa  jamii katika masuala mbalimbali ili iwe kumbukumbuku ya kumtambua.

Alisema Dk. Mengi ni mfano wa kuigwa na jamii kwa kuwa amefanya mambo mengi ya kusaidia jamii, ikiwamo kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo kwenda kutibiwa nchini India.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo ya heshima, Dk. Mengi alisema mafanikio yake na moyo wa kupenda kuwasaidia watu wenye kuhitaji yanatokana na kumtanguliza Mungu katika kila jambo.

"Huwezi kufanikiwa chochote bila ya kumtanguliza Mungu kwa mambo yako unayoyafanya siku zote" alisema.

Dk. Mengi aliwaambia watu waliohudhuria sherehe hizo kwamba wanachama wa klabu za Lion sio kwamba wana fedha nyingi bali wanawasaidia wenzao kutokana na moyo wao wa upendo na kujali matatizo ya wengine.

“Kuwasaidia wenzako haiangalii una kiasi gani cha fedha bali kinachotakiwa ni mtu kuwa na moyo wa kutoa. Mwenyezi Mungu anataka mtu aliyebahatika kuwa na uwezo kuwasaidia wenzake wenye shida na mahitaji” alisisitiza Dk. Mengi.

Taasisi mbalimbali za kimataifa zimewahi kumtunukia tuzo mbalimbali,  Dk. Mengi kutokana na mchango wake mkubwa anaoutoa kwa jamii hususani kwa watu wenye shida na makundi maalum wakiwamo walemavu.

 
CHANZO: NIPASHE


No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...