Katibu wa Kundi la wabunge wa Afrika Mashariki, kutoka Tanzania,
Shy-Rose Bhanji (Kushoto) na Mwenyekiti wake, Adam Kimbisa,
akionyesha mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Wabunge wanaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wamepongeza msimamo wa Rais Jakaya Kikwete, wa kutojitoa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku wakitaka kuwapo kwa Shirikisho la Kisiasa la EAC kutofanywa haraka haraka.
Mwenyekiti wa wabunge hao, Alhaj Adam Kimbisa, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
“Tunaungana na Watanzania wengi sana wanaounga mkono kuwapo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka hatua hiyo isifanywe haraka haraka bali kwa umakini mkubwa sera ambayo pia serikali ya Tanzania imeipa kipaumbele,” alisema Kimbisa.
Alisema wanaungana na kauli ya Rais Kikwete kwamba Tanzania ni kati ya nchi zinazotaka ngazo zote za mchakato wa utangamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hatua yoyote.
Hatua ya kwanza ni Umoja wa Forodha, ambayo inafuatiwa na Soko la Pamoja, kisha Umoja wa Forodha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Hadi sasa ni hatua mbili zilizotiwa saini; ambazo ni Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja na kwamba mchakato wa kuweka saini Umoja wa fedha unatarajiwa kufanyika baada ya kikao cha juu cha marais.
Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika mjini Kampala Novemba 30, mwaka huu, iwapo masuala yote muhimu ya mchakato huo yatakuwa yamekamilika.
Kimbisa alisema wanaamini kwamba misingi ya utengamano wa kiuchumi ikijengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo, wananchi wote wa Afrika Mashariki watafaidika na hivyo suala la kuruka hatua yoyote ni jambo lisilokubalika.
Aidha, alimpongeza Rais Kikwete kwa kupeleka kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalumu iliyoundwa na Umoja wa Mataifa (UN) ili kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alisema pia wanaamini kwamba suluhisho la matatizo ya nchi za Maziwa Makuu yatapata ufumbuzi wa kudumu iwapo kutakuwa na utaratibu wa kukaa meza moja kwa pande zote husika na kufanya mazungumzo ya kuleta amani.
Pia aliiomba serikali kutolegeza msimamo wake wa kuwarejesha makwao wahamiaji haramu kutoka katika nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, DRC na nchi nyingine ambao walitishia na kuharibu hali ya usalama na mazingira katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita na Kigoma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment