Monday, 26 August 2013

WAZIRI MEMBE AZUNGUMZA NA TUME YA JAJI WARIOBA KUHUSU URAIA PACHA

Picture

Habari ifuatayo na picha kwa mujibu wa Tagie Daisy Mwakawago na Fatma Salum

“Uwepo wa Diaspora ni lazima utambulike Kikatiba,” asema Waziri Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Waziri Membe aliyasema hayo alipokutana na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo mjini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, viongozi hao walijadili suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship)ambalo linapiganiwa kwa kiasi kikubwa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora).

“Tumekuja kuwasilisha masuala muhimu mawili:  moja, uwepo wa uraia wa nchi mbili katika Rasimu ya Katiba na pili, Katiba mpya iruhusu raia yoyote wa Tanzania aweze kuwa na uraia wa nchi nyingine pasipo kuukana uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.

Alisema kuwa Wizara yake inatambua suala la uraia wa nchi mbili kuwa ni la msingi, ambalo halikugusiwa 
katika Rasimu ya Katiba iliyopo.

“Chimbuko la uraia wa nchi mbili lilitokana na wingi wa Watanzania walioko nje ya nchi ambao wanatafuta fursa ya kuwekeza na kuinua maendeleo ya nchi yao,” alisema Waziri Membe.

Aliongeza pia, “ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 inawatambua Watanzania hao na kutaka wapewe fursa ya kuwa na raia wa nchi mbili katika kuinua maendeleo ya nchi.”

Watanzania hao wamekuwa wakikabiliana na matatizo kadhaa ambayo yanawanyima haki za msingi, kama vile afya, elimu na masuala ya ajira.  “Kilio chao kimekuwa kero kubwa kwa vile wakati mwingine wanatibiwa kwa gharama kubwa sana ambazo hazilingani na kipato chao,” alisema Waziri Membe.

Aidha, changamoto hizo zimekuwa ni chanzo kikubwa cha kuwashawishi Watanzania hao kuchukua uraia wa nchi za kigeni ili kuwawezesha kupata huduma muhimu za kijamii kama vile elimu na afya.
Picture
Mhe. Waziri Membe akiwa katika mazungumzo na Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hivi sasa sheria yetu haimruhusu Mtanzania kuchukua uraia wa nchi mbili pasipo kuukana uraia wa nchi yake,” alisema Membe, na kufafanua kuwa “Ilani ya CCM inamuhamasisha Mtanzania huyo achangie maendeleo ya nchi yake kupitia uraia wa nchi mbili.”

Waziri Membe alisema kuwa Watanzania wakiwa nje wanakosa fursa za kazi zenye kipato kikubwa wasipokuwa na uraia wa nchi hiyo, jambo linalopelekea maisha magumu na kushindwa kujikimu na kuchangia kipato chochote kwa ndugu zao walioko nchini.

“Badala yake, unakuta Watanzania wananaswa na tamaa ya ‘kujilipua’ kwa kubadili uraia wa nchi nyingine zinazokubali uraia wa nchi mbili, kama vile Rwanda, na kuachana na na uraia wa Tanzania,” alieleza Waziri Membe.

Kwa upande wake, Mhe. Warioba alisema kuwa maoni hayo ya uraia wa nchi mbili yamekuwa yakijitokeza katika ukusanyaji wa maoni sehemu mbalimbali.  Na kuongeza kuwa, hofu kubwa ya wananchi ni usalama wa nchi yao endapo uraia wa nchi mbili utaruhusiwa.

Mhe. Waziri Membe alikuwa ameambatana na Balozi Gamaha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara na Balozi Bertha Semu-Somi, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.   Kwa upande wa Mhe. Warioba, alikuwepo Jaji Agostino Ramadhani, Makamu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Salim Ahmed Salim, Mjumbe wa Tume, pamoja na Katibu na Naibu Katibu wa Tume ya Mabadiliko


CHANZO: Wavuti

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...