Na Herieth Makwetta, Mwananchi |
Mbunifu wa mitindo nchini aliyewahi kutamba na vazi la ‘Single button’ Martin Kadinda amesema kuwa suala la wanaume kujihusisha ubunifu wa mitindo haihusiani na vitendo vya ushoga kama wengi wanavyodai na kuzungumza.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Starehe Kadinda alisema kuwa mitindo ni sehemu ya maisha hivyo, wavaaji wanahitaji na ni lazima itengenezwe na wabunifu.
“Sisi tunabuni wengine wanavaa, hata mavazi yaliyopo sasa wapo watu walikaa wakabuni; Haina maana kwamba watu hawa wanajihusisha na vitendo hivyo kama inavyoelezwa na wengi. Nadhani ni suala la saikolojia tu hapo,” alisema Kadinda ambaye sasa anawafua washiriki wa Miss Dar City Center inayotarajiwa kufikia kilele Juni mosi mwaka huu.
Martin alisema kuwa awali wanaume walifunzwa kuvaa moja ya aina ya mavazi, lakini kutokana na ubunifu uliopo sasa vijana wengi huvaa kutokana na mitindo ya sasa. “Mwaka jana nilibuni ‘Kima Collection’ hili ni vazi lenye rangi moja iliyokolea na suruali isiyo na mkanda. Hili ni vazi lililopokewa vyema na vijana wa sasa, lakini bado wapo watu wanaokosoa. Nadhani hizi ni fasheni, ni sawa tu na wazazi wetu zamani walivaa suruali pekosi na afro kubwa kichwani ilikuwa fasheni,” alisema.
Martin aliye na mchumba waliyepanga kuoana na kuwa na watoto wawili alibainisha kwamba anatarajia kufungua stoo maalumu kwa ajili ya kutangaza mitindo yake sanjari na kuuza nguo zake aina zote.
Kwa kipindi cha miaka mitatu aliyokaa katika tasnia ya ubunifu, Martin amefanikiwa kumiliki nyumba yake mwenyewe na gari mbali na mafanikio mengine mengi aliyoyataja kuwa ni siri yake.
No comments:
Post a Comment