Friday, 7 June 2013

MBATIA: SERIKALI IACHE KUSAMBAZA VITABU


Debora Sanja,Mtanzania
MBUNGE wa Kuteuliwa,James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ameitaka Serikali kusitisha zoezi la usambazaji wa vitabu kwa shule za msingi vilivyonunuliwa kwa fedha za chenji ya Rada. Mbatia alitoa kauli hiyo jana Mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu udhaifu ulipo katika vitabu hivyo.
Alisema iwapo Serikali itakaidi na kuvisambaza vitabu hivyo, watakwenda mahakamani na kuishitaki Serikali kwa uhujumu wa uchumi.

Alisema tayari kampuni zaidi ya 10, zilikwisha zabuni ya kusambaza vitabu hivyo, tangu Machi mwaka huu, kwa gharama ya Sh bilioni 55.2 na kwamba yeye na wabunge wenzake wa NCCR-Mageuzi hawakubaliani na hatua hiyo.


“Tunataka kabla ya vitabu hivyo kusambazwa liundwe jopo la wataalam na wahariri wa vitabu wavipitie vitabu vyote kabla ya watoto wetu kwenda kulishwa sumu.


“Vilevile namuomba Rais wa Marekani, Barak Obama anapokuja nchini badala badala ya kuwekeza katika sekta nyingine atupe msaada utakaotuwezesha kuwekeza katika sekta ya elimu iliyo bora ili tuweze kupambana na adui ujinga,” alisema Mbatia.


Alisema vitabu hivyo karibu vyote vina makosa na vikiendelea kutumika wanafunzi wa kitanzania wataendelea kulishwa sumu huku elimu ya Tanzania ikiendelea kuporomoka.


“Kwa mfano katika kitabu cha somo la Uraia Darasa la Nne kinaeleza kwamba zao lililopo katika Nembo ya Taifa ni Chai na Kahawa wakati sio kweli bali ni Pamba kwa Tanzania Bara na Karafuu kwa Zanzibar.


“Vitabu vingi vinavyotumika mwandishi ni huyohuyo, mhariri huyohuyo na pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kuidhinisha Machapisho ya Kielimu (EMAC) na kitabu hicho kimepewa Ithibati,” alisema.


Alisema pia mbali na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuivunja EMAC iwachukulie hatua wajumbe wote kwa kuwa wamefanya kosa la jinai na ujambazi.


“Kwa kuwa pia Serikali inazembea katika sekta ya elimu, ninawaomba waheshimiwa wabunge wote tuungane kuisimamia Serikali tuache itikadi zetu kwa kuwa hata wanafunzi wale waliojinyonga kutokana na kufeli mtihani wa Kidato cha Nne walitokea katika majimbo ya wabunge wa CCM,” alisema.


Alisema NCCR–Mageuzi siku zote, ajenda yao ni elimu kwa kuwa elimu ikiwa bora hakutakuwepo hata maadui wengine yaani maradhi na umasikini.

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...