Umoja wa Mataifa Ijumaa utakuwa na mgeni maalum, wakati mwanaharakati msichana wa Pakistan Malala Yousufzai atakapowasilisha kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ombi la msaada kwa watoto wote, hususan wasichana kwenda shule ifikapo mwaka wa 2015.
Malala Yousufzai anasherehekea miaka 16 ya kuzaliwa kwake Julai 12. Ni siku maalum kwake ambayo pengine hakuitarajia, pale wanamgambo wa Taliban walipompiga risasi kichwani akitoka shule kwenda nyumbani yapata miezi 9 iliyopita.
Malala alilengwa kwa sababu alizungumza kuhusu haki ya wasichana kwenda shule nchini mwake Pakistan.Lakini badala ya kupokea zawadi za kheri njema wakati wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwake, anatumaini kutoa mwito wa kusaidia vijana kote duniani kupata haki ya kuelimishwa.
Mwanaharakati huyu wa elimu atamkabidhi katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na ombi lililotiwa saini na zaidi ya watu laki tatu na mia tatu.
Watu hao wanasimama kidete na Malala kuomba Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kugharamia walimu wapya, shule na vitabu na kujitolea upya kuona kwamba kila msichana na mvulana anaingia darasani ifikapo 2015.
Msemaji wa katibu mkuu, Martin Nesirky anasema bw. Ban atamkaribisha msichana huyo jasiri katika Umoja wa Mataifa na kwamba ameshatangaza Julai 12 kuwa ‘Siku ya Malala.’
Kabla ya kuwasilisha ombi lake kwa Ban Ki Moon, Malala atahutubia vijana 500 kutoka kote duniani katika kikao maalum cha Baraza Kuu kwa vijana.
CHANZO: Mdimuz
No comments:
Post a Comment