Thursday, 15 August 2013

MWAKYEMBE AACHA MTIKISIKO AIRPORT DAR



Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, akizungumza na madereva wa teksi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara ya kushtukiza jana 


Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema tatizo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kufanywa uchochoro wa kupitishia dawa za kulevya hautokani na kukosekana kwa vifaa vya kisasa bali ni wafanyakazi wenyewe waliopewa dhamana ya kuusimamia na ameahidi kuwataja leo na hatua walizochukuliwa. 


Dk. Mwakyembe alisema hayo jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza na kubaini kuwa katika uwanja huo kuna mitambo ya kisasa iliyofugwa kufuatilia shughuli zote zinazofanyika ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa mizigo hivyo siyo rahisi kwa mtu kupitisha dawa za kulevya bila kubainika. 

Alisema taarifakwamba yupo afisa mmoja aliyechukuliwa hatua kutokana na sakata la dawa za kulevya ni sawa na utani kwa sababu kwa mujibu wa picha zilizorekodiwa katika mitambo (CCTV) iliyopo uwanjani hapo siku dawa hizo kilo 150 zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 zilipopitishwa Julai 5, mwaka huu kwenda Afrika Kusini  ni wengi wanaostahili kuchukuliwa hatua.

“Tatizo hapa siyo mfumo wa mitambo ni uswahili tu ndiyo unaofanyika hapa, kesho (leo) nitaitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza Watanzania wanaofanya hujuma na hatua walizochukuliwa, nataka kuvisafisha viwanja vya ndege ili dawa za kulevya zisipite tena hapo,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema hatua atakazochukua itakuwa ni historia na kama wapo watu waliozoea kupitisha dawa za kulevya katika viwanja hivyo labda watafute njia nyingine ya kusafirisha kama ya punda.

Alisema haiwezekani dawa za kulevya kupitishwa kirahisi katika uwanja huo wakati kuna vyombo mbalimbali vya serikali kama Usalama wa Taifa, Polisi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji na nyingine na wanalipwa mshahara na serikali.

Dk. Mwakyembe alisema alikaa kimya ili kuvipa muda vyombo vya usalama vijiridhishe na kumpa taarifa kutokana na sakata hilo kwani ni aibu kwa uwanja wa ndege wenye jina la Mwalimu Nyerere na nchi kwa ujumla kuchafuka kimataifa kutokana na watu wachache wazembe.

Kwa upande wake, Meneja wa Usalama wa uwanja huo, Clemence Jingu, alimweleza Dk. Mwakyembe kuwa katika kipindi cha miaka miwili matukio 36 ya kupitisha dawa za kulevya katika uwanja wa JNIA yametokea.

Kauli ya Waziri Mwakyembe inatofautiana na ya Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, ambaye alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa sababu zinazochangia kutobainika kwa dawa hizo wakati wa kupitishwa ni ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kuzibaini kulinganisha na nchi nyingine.

Alisema nchi nyingine zina vifaa vya kisasa zaidi na kwamba wakati sasa umefika kwa serikali kuwekeza katika kupata vitendea kazi zaidi ili kufanikisha mapambano ya dawa za kulevya.

Katika hatua nyingine, uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini  kuwa, siku ya tukio mmoja wa wafanyakazi katika uwanja huo wakati mabegi sita yaliyosheheni dawa za kulevya yanapitishwa, alikuwa anaongea na simu ya mkononi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, picha zilizorekodi nyendo kwenye uwanja huo siku ya tukio, tofauti na utaratibu wa kawaida, mabegi hayo baada ya kupita eneo la ukaguzi, mbwa wa Polisi walipelekwa kuyanusa yakiwa tayari yamepakizwa kwenye gari la kubebea mizigo ya abiria kabla ya kupelekwa kwenye ndege.

Habari zaidi zinaeleza kuwa ndani ya uwanja huo siku hiyo ya tukio mtu mmoja ambaye siyo mfanyakazi wa uwanja huo aliwekwa katika kitengo kimojawapo cha ukaguzi kwa sababu ambazo hazijulikani.
NIPASHE ndilo lilikuwa la kwanza kuripoti taarifa za kukamatwa kwa wasichana wawili raia wa Tanzania waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oriver Tambo uliopo eneo la Kempton Park, Afrika Kusini wakiwa na dawa hizo aina ya Crystal Methamphetamine.

Waliokamatwa, ni Agnes Jerald (25), Melisa Edward (24), ambao wameshtakiwa Afrika Kusini.
Wanawake hao walikamatwa wakiwa na dawa hizo ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’ na baadaye walikabidhiwa polisi na kufunguliwa mashtaka.

Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 wamekamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo. 

Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini na kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani. Wiki moja baada ya tukio la wasichana hao, Watanzania wengine wawili walikamatwa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh. bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai hadi Hong Kong.

Matukio hayo yanatokea wakati wakuu wa uwanja wa ndege wa JNIA zinakopitishwa wakiwa hawana cha kusema juu ya uharamia huo unaotokea kwenye kitovu cha mawasiliano cha nchi.

Jumatatu wiki hii, Waziri Mwakyembe alisema kwamba ndani ya siku 14 wanaojihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya wataanza kukamatwa huku akiahidi kuwabana wafanyakazi wa JNIA.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...