Friday, 13 September 2013

BABY MADAHA: SASA KIMATAIFA ZAIDI


Baby Madaha
MWANAMUZIKI chipukizi hapa nchini, Baby Madaha, amerekodi kibao chake kipya cha ‘Summer Timer’ ambacho kitaanza kusikika wakati wowote katika vituo mbalimbali vya redio.
Tayari kibao hicho kinapatikana katika mitandao mbalimbali ya kijamii na muda si mrefu video yake nayo itaanza kuonekana katika vituo tofauti tofauti vya televisheni hapa nchini na hata nje ya nchi.
Pamoja na uchanga wake, Baby amerekodi kibao hicho kikali, ambacho kinakwenda kimataifa kutokana na midundo yake inayokubalika kimataifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Baby akiwa na Prodyuza wake Mkenya, Joe Kariuki, anasema kuwa sasa ameachana kabisa na muziki wa Bongo Fleva na badala yake anapiga muziki utakaokubalika kimataifa.


“Unajua vibao vingi vya Bongo Fleva ni sawa kama wameiga midundo ya Marekani, hivyo hata ukipiga nje, watu hawashituki, tofauti na midundo yetu tuliyoamua kuipiga inakubalika sana kimataifa,” anasema Baby.
Lebo mpya
Baby, kwa sasa yupo na lebo mpya ya Candy & Candy chini ya Mkurugenzi wake Kariuki, ambaye tayari ameingia naye mkataba wa miaka miwili, ambao utamwezesha kutengenezewa vibao vyake katika studio ya Candy & Candy iliyopo jijini Nairobi.
Mbali na kurekodiwa vibao vyake katika studio hiyo, pia Baby atafanyiwa promosheni ya muziki wake, kupatiwa mavazi ya kisasa kwa ajili ya shoo, kutengenezewa video zake, malazi, usafiri na mambo mengine.
Tayari, studio ya Candy & Candy imempa Baby, ‘sports car’ aina ya Audi yenye thamani ya sh 5,000,000 za Kenya, takriban sh milioni 90 za Tanzania, ambalo litawasili hivi karibuni kutoka Nairobi, Kenya.
Baby akizungumzia lebo yake hiyo mpya baada ya kuachana na ile ya Pilipili Entertainment, anasema kuwa, amefurahi sana, kwani sasa ndio mwanzo wake wa kutoka na kufaidika na kazi yake hiyo ya muziki.
Pilipili Entertainment ilimwezesha Baby kupata tuzo kibao za baadhi ya filamu zake katika tamasha la kimataifa la Ziff na nyingine kupata tuzo nchini Nigeria katika tuzo ya African Magic.
Anasema kuwa ameachana na Pilipili, kwa sababu wenyewe ni wazuri sana katika filamu, wakati yeye sasa ameamua kwenda kimataifa zaidi kwa upande wa muziki, ambako sasa yuko chini ya lebo hiyo mpya.
“Sasa malengo yangu ni kutesa kimataifa kimuziki, hivyo niko chini ya ‘management’ mpya ya Candy & Candy chini ya Mkurugenzi Joe na tayari tumeanza kutoka kimataifa,” anasema Baby
Filamu zilizotesa
Pamoja na sasa kuamua kujikita zaidi katika muziki, Baby alifanya vizuri katika filamu za hapa nchini, ambapo alipata tuzo kupitia filamu zake za ‘Ray of Hope’ iliyoshinda tuzo ya African Magic ya nchini Nigeria.
Wakati zile za ‘Nani’, ‘Ray of Hope’ pamoja na ‘Lost’ ziliibuka kidedea katika tamasha la filamu la kimataifa la Zanzibar (Ziff), kwa miaka mitatu mfululizo ya 2010, 2011 na 2012.
Naye Kariuki akizungumza jijini Dar es Salaam, anasema lebo ya Candy & Candy, imeamua kumchukua Madaha ili kumwezesha kutengeneza nyimbo zitakazouza kimataifa zaidi, badala ya kunyang’anyana soko la Tanzania.
Anasema huyo ni msanii wa kwanza wa kike kuwamo chini ya lebo yake, kwani walikuwa na wasanii wa kiume tu, kitu ambacho wengi walikuwa wakiwauliza.
“Baada ya kusikia baadhi ya nyimbo zake, tulibaini kuwa Madaha ni mwimbaji mzuri ila anachokosa ni baadhi ya vitu na sisi tukaamua kuingia naye makataba wa miaka miwili, ili kumuweka vizuri, ili awe wa kimataifa zaidi,” anasema Kariuki.
Mkataba wake
Akielezea kuhusu mkataba huo, Kariuki anasema kwa kuanzia mkataba huo una thamani ya sh milioni tano za Kenya, takriban sh milioni 90 za Tanzania.
Anasema mkataba wenyewe utamnufaisha sana Baby, kwani Cand & Candy watakuwa wakimfanyia mambo kibao, ikiwamo kupromoti kazi zake baada ya kuzirekodi na kumwandalia hata matamasha.
Wasanii wengine
Anasema wasanii wengine waliopo katika lebo hiyo ni pamoja na Mr. Nice, Top C, For D na Chapter 3.
Anasema kuwa amekuwa akitengeneza muziki wa wasanii hao ambao wengi wao wamekuwa wakifanya vizuri.
Kwa upande wa Mr. Nice, Kariuki anasema kuwa walitoa kibao kimoja ambacho hata hivyo hakikutamba sana, kwa kuwa mwimbaji huyo aling’ang’ania kutia baadhi ya vionjo vya zamani, ambavyo kwa sasa havipendwi na watu.
“Unajua muziki umebadilika sana, sasa Mr. Nice yeye anataka aendelee kutoka na vibao vyake vile vya kale vya ‘Bata Kapanda Baiskeli’, hivyo wakati wake umepita na watu wanataka vitu vipya, lakini yeye amekazana na mambo ya kale, ndiyo maana kibao chake hakijapokewa vizuri,” anasema.
‘Kolabo’ kimataifa
Kariuki anasema baada ya kukamilisha kurekodi kibao hicho cha ‘Summer Time’, sasa wanamtafutia Baby ‘kolabo’ na mwanamuziki wa kimataifa ili aweze kupiga naye.
Anasema, kutokana na muziki anaotengenezewa sasa, Madaha anaweza kupata ‘kolabo’ na wanamuziki wa kimataifa kama kina Liana, Jay L na wengineo.
CHANZO: Tanzania daima

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...