Rais Jakaya Kikwete akiwa katika mazungumzo na marais; Paul Kagame (kushoto) wa Rwanda, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na Rais Yoweri Museveni (wa pili kulia) wa Uganda wakati wa mkutano wa
Rais Jakaya Kikwete amekutana kwa faragha na Rais wa Rwanda, Paul Kagame katika mazungumzo yanayoelezwa kuwa yalikwenda vizuri.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana ilisema kuwa mazungumzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya saa moja, yaliwaridhisha viongozi hao.
“Viongozi hao wamekutana kwa zaidi kidogo ya saa moja katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, nje kidogo ya mji wa Kampala, Uganda, “ ilisema taarifa ya Ikulu.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Rais Kagame wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kujenga uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Kikwete na Kagame wapo Uganda kuhudhuria Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Kimataifa wa Maziwa Makuu – “International Conference on the Great Lakes Region (ICGLR)” uliofanyika jana katika Hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort.
Viongozi wengine ambao walihudhuria Mkutano huo ni pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa ICGLR na mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
Rais Kikwete na ujumbe wake aliwasili Kampala jana asubuhi akitokea mjini Dodoma ambako aliwaapisha Makatibu Wakuu watatu na Naibu Makatibu Wakuu wawili iliyofanyika Ikulu Ndogo, Dodoma.
Hata hivyo, taarifa ya Ikulu haikufafanua zaidi kama mazungumzo hayo yaligusa nini mahususi hasa juu ya ushauri wa Rais Kikwete juu ya Rwanda kuzungumza na waasi, na hali ya mapigano ndani ya DRC yanayoendelea sasa ambayo waasi wa M23 wanaodaiwa kusaidiwa na Rwanda wamefurushwa na vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa vinavyoongozwa na wanajeshi wa Tanzania.
Tangu Rais Kikwete ampe ushauri Rais Kagame kuwa afanye mazungumzo na waasi wa nchi hiyo waliokimbilia DRC kumekuwa na hali ya kuzorota kwa uhusiano kati ya Rwanda na Tanzania.
Ushauri wa Rais Kikwete umekuwa ukilaumiwa na baadhi ya viongozi wa Rwanda na hata kufikia vyombo vya habari vya nchi hiyo kumtusi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment