Thursday, 5 September 2013

KIMBISA: TUMEFANIKIWA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI KUWA TANZANIA

Mwenyekiti wa Wabunge Watanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, Adam Kimbisa.
Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge la Afrika Mashariki imefanikiwa kupata kikao rasmi katika ratiba ya vikao vya Bunge hilo.

Mwenyekiti wa Wabunge Watanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, Adam Kimbisa, alisema Tanzania kama nchi pia imefanikiwa kupata kikao chake.

Kimbisa alisema awali Arusha ambayo ni Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilichukuliwa kwamba iko Tanzania kitu ambacho siyo sahihi.

Alifafanua kwamba ukiongelea Jumuiya ya Afrika Mashariki, Arusha ni Makao Makuu na wadau wote wa nchi wanachama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania wote ni wadau kwa asilimia 100.

Kimbisa alisema azimio lililopitishwa katika Bunge hilo lililomalizika mjini Arusha wiki iliyopita, iliamuliwa kwamba Arusha kama Makao Makuu itapata vikao viwili na Tanzania itapata kikao kimoja sambamba na nchi zingine kikao kimoja kila nchi kwa njia ya mzunguko.

Alisema kikao kitachofanyika Tanzania kinatarajiwa kufanyika Dodoma, Dar es Salaam au Zanzibar kwa vile kuna kumbi za Bunge hivyo kurahisisha mikutano  ya Bunge kufanyika moja kati ya sehemu hizo.

Alisema vikao viwili vitavofanyika Arusha vitakuwa ni vile vya bajeti pamoja na ukaguzi wa mahesabu ambavyo ni vikao muhimu sana katika bunge. 

Wakati huo huo, Kimbisa ametetea uamuzi wa wabunge Watanzania kutoka nje ya Bunge na kupelekea kikao cha bunge kuahirishwa wiki iliyopita huko Arusha na kusema kuwa hatua hiyo ililenga kupinga msimamo wa nchi zingine kutoka nje ya bunge ili kushinikiza hoja zao zisikilizwa bila kufuata kanuni.

Katibu wa Wabunge hao, Shy-Rose Bhanji, alisema uwapo wa vikao hivyo Arusha utasaidia kupunguza gharama ya kusafirisha wafanyakazi na maofisa wa Jumuiya ambao hufuatana na wabunge pale vikao vinapofanyika kwenye nchi mwanachama.

Hatua ya kufikia mwafaka huo ilitokana na wabunge wengi kutoka Uganda, Rwanda, Kenya na baadhi kutoka Burundi kutaka utaratibu wa vikao vya Bunge kuendelea kwa njia ya mzunguko kwa kila nchi kupata vikao.

Alisema hoja ya Wabunge Watanzania kutaka vikao vyote vya Bunge vifanyike Arusha kwa sababu Serikali ya Tanzania ilitoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu na Serikali ya Ujerumani ilifadhili ujenzi wa jengo hilo la kisasa ambalo linahudumia taasisi tatu za Jumuiya.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...