Wednesday 11 September 2013

MKAPA ATOA MAPENDEKEZO KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI


Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa

Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, ametoa mapendekezo tisa ya kuboresha mfumo wa umiliki wa ardhi ili kuliwezesha taifa kuondokana na migogoro ya ardhi ambayo inatishia amani na utulivu katika maeneo mbalimbali hususani vijijini.

Mkapa alitoa mapendekezo hayo jana wakati akiwasilisha mada katika kongamano la kimataifa la Haki Ardhi kwa Amani Endelevu, uliloandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastiano Kolowa (Sekomu) linaloendelea jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni upimaji wa ardhi yote, kupeleka mamlaka ya usimamizi ardhi kwa wananchi, kuzingatia haki za wenyeji wakati wa uwekezaji.

Alisema sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania haijasajiliwa na wananchi kuwa na hati miliki, jambo ambalo limekuwa chanzo cha migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji na wananchi na wawekezaji.

Mkapa alisema kuna urasimu kwenye usimamizi na uendelezaji wa ardhi na kwamba upo umuhimu wa kutoa mamlaka kwa viongozi wa ngazi za chini katika usimamizi na endelezaji wa ardhi.

Alisema ni lazima kuwe na mipango mahususi ya matumizi ya ardhi kwa wakulima na wafugaji na si kundi moja kuona lina haki ya kumiliki kuliko kundi jingine.

Alisema ongezeko la migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambayo imesambaa takribani nusu ya mikoa ya Tanzania bara, ni tishio kwa umoja wa kitaifa kwani imesababisha watu kupoteza maisha na uharibifu wa mali.

Mkurugenzi wa Shirika la HakiArdhi, Yefred Myenzi, alimuuliza Mkapa kwanini serikali ilishindwa kutekeleza hayo wakati wa uongozi wake ili kuondokana na migogoro ya ardhi.

Mkapa alisema kwa wakati huo serikai haikuwa na fedha kwa ajili ya
utekelezaji na kwamba ilianzisha mipango mbalimbali kama Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na Mkurabita ili kuwakwamua wananchi na umaskini na kuwekeza katika kilimo.

Awali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka, aliwatoa hofu Watanzania na kusema kuwa hakuna kiongozi yeyote atakayekubali ardhi kuuzwa kama njugu na kwamba sheria za usimamizi na ugawaji wa ardhi kwa wageni zinazingatiwa na kusimamiwa.

Alisema hakuna njia ya kukwepa wawekezaji kwenye ardhi bali cha  kuangaliwa ni jinsi ambavyo jamii itanufaika na uwekezaji na wakati huo mwekezaji akinufaika na ardhi husika.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kongamano hilo, Askofu Dk. Stephen Munga, alisema lengo la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili changamoto za ardhi kwa maendeleo endelevu katika kipindi chenye ongezeko la migogoro ya ardhi.

Kongamano hilo la siku tatu linawashirikisha watafiti, wasomi na wataalam mbalimbali kutoka nchi za Madacascar, Asia, Afrika Kusini, Sweden, Zambia, Zimbabwe, Uganda, Ghana, Kenya, Uingereza na mwenyeji Tanzania.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...