Monday 9 September 2013

WAFANYAKAZI TAZARA WALIPUA `BOMU`

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe akizungumza na wafanyakazi waliogoma wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara, kwenye stesheni ya Dar es Salaam jana.

Wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara) wamewasilisha nyaraka nzito kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harison Mwakyembe ambazo zinaonyesha jinsi  viongozi wa shirika hilo wanavyojinufaisha kitendo kilichomwacha mdomo wazi waziri huyo kwa mshangao.


Nyaraka hizo ziliwasilishwa  na baadhi ya wafanyakazi zikionyesha jinsi bidhaa zinavyosafirishwa kutoka Tanzania kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku kiasi kikubwa cha mapato kikibakia mifukoni mwa vigogo wa Tazara.

Katika mkutano huo, wafanyakazi hao waliwasilisha taarifa za Mkurugenzi mpya wa shirika hilo kuishi katika hoteli ya New Afrika wakati nyumba anayotakiwa kuishi  ikiwa imepangishwa na mkurugenzi aliyemaliza muda wake kwa kumpangisha mtu mwingine.

Kwa mujibu wa wafanyakazi hao, waliwasilisha nyaraka zinazotumika kusafirisha bidhaa kwa kupunguza bei badala ya gaharama halisi inayotakiwa fedha ambazo huzijulikani zinapokwenda. Pia wafanyakazi hao walimueleza Dk. Mwakyembe kuwa Tazara ina madeni makubwa ambayo hayajawahi kuzungumzwa na kuwekwa wazi ili yaweze kulipwa na badala yake wamekuwa wakisingizia kwamba wafanyakazi wanadai.

Wafanyakazi hao pia walimueleza waziri huyo kuwa mameneja saba waliokuwa wamefukuzwa wamerejea kazini na hatua hazijachukuliwa kama ilivyoelekezwa na baraza la mawaziri kuwa wachunguzwe na kuchukuliwa hatua za kisheria na badala yake wameendelea kufanyakazi kwa kuharibu vielelezo na nyaraka nyeti.

Mfanyakazi Amiri Husein alidai kuna mabehewa 26 yalipelekwa DRC lakini fedha zake ziliishia mifukoni mwa wakubwa.

Alisema Juali 25 mwaka huu, treni iliyokuwa imepakia mafuta kutoka Tanzania kwenda DRC  ambapo zaidi ya Sh. bilioni moja iliyolipwa iliishia mifukoni mwa wajanja.

Baada ya kupokea taarifa hizo, Dk. Mwakyembe aliiagiza menejimenti kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma zilizotolewa na wafanyakazi.

Aliwataka wafanyakazi kurejea kazini leo na wafanyekazi kwa ueledi na ufanisi mkubwa ili kufidia hasara ya Sh. bilioni 2.4 iliyotokea wakati wa mgomo.

Waziri huyo alisema Shirika inafanyakazi kwa hasara na inaelekea kufilisika na kwamba Tanzania na Zambia zimekaa pamoja ili kulinusuru.

Alisema mapato ya Shirika hilo kwa mwezi ni Sh.bilioni 2.4 wakati matumizi ni Sh. bilioni 4 na kwamba mambo hayo yanatokana na ufanisi mbovu wa kiutendaji na kutochukua maamuzi mazito.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...